• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 12:26 PM
Gachagua: Ni heri nipoteze umaarufu kuliko kuruhusu vijana waangamizwe na pombe haramu   

Gachagua: Ni heri nipoteze umaarufu kuliko kuruhusu vijana waangamizwe na pombe haramu   

NA SAMMY WAWERU

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amesisitiza kuwa kamwe hatalegeza kamba msimamo wake mkali dhidi ya pombe haramu na dawa za kulevya.

Bw Gachagua ameapa ni heri apoteze umaarufu wake kisiasa na uongozini, kuliko aachilie vijana waangamizwe na pombe haramu.

Akizungumza katika mkutano na viongozi wa kisiasa kutoka Bonde la Ufa na wakuu wa askari, Nakuru, Jumatatu, Mei 29, 2023 naibu rais alisema yuko tayari kuenda nyumbani 2027 endapo vita dhidi ya pombe haramu na dawa za kulevya ndicho kigezo kitakachotumika kupima utendakazi wake.

Gachagua amekuwa katika mstari wa mbele kupambana na pombe haramu hasa Mlima Kenya, akisema alitwikwa jukumu hilo na bosi wake, Rais William Ruto.

Eneo la Kati limetajwa kama mojapo ya maeneo yaliyoathirika pakubwa kutokana na pombe haramu na hatari.

“Nina nyumbani ninakotoka, kwa Mama Gachagua, na ikiwa msimamo wangu kuhusu vita dhidi ya pombe haramu ndio utaninyima umaarufu na kazi, niko tayari kurejea kwetu,” alisema Bw Gachagua.

Akielezea kusikitishwa kwake na jinsi kero ya pombe iliovyoathiri vijana nchini, naibu rais alisema atazidi kuonyesha makali kwa wauzaji wa vileo hatari na wanaovitengeneza.

Gachagua aidha alitoa onyo kali kwa maafisa wakuu wa polisi, akisema yeyote atakayelemewa kukabiliana na pombe haramu, serikali ya Dkt Ruto haina nafasi yake katika kikosi cha polisi nchini.

“Hatutahamisha shida kutoka kaunti moja hadi nyingine au eneo moja hadi lingine. Ukishindwa kuzima pombe eneo lako, tutakuondoa kikosini tuwape wengine kazi walio tayari,” alielezea akionya maafisa wakuu wa polisi na machifu.

Oparesheni dhidi ya pombe haramu na mihadarati ilianza na Mlima Kenya, na sasa imeingia Bonde la Ufa Bw Gachagua akiahidi kuwa itakuwa zoezi la kitaifa.

“Rais Ruto, mimi Gachagua, Prof Kithure Kindiki (Waziri wa Usalama wa Ndani na Mikakati ya Serikali) na Inspekta Jenerali Mkuu wa Polisi, IG Japhet Koome, sote hakuna anayekunywa pombe wala kutumia dawa za kulevya. Sioni sababu ya pombe haramu kukosa kuisha.”

Naibu rais alitahadharisha kwamba endapo kero ya pombe haramu haitakabiliwa, siku za usoni huenda viongozi wanaomezea mate viti vya kisiasa wakakosa kura.

Gachagua amewataka magavana kuwa makini wanapotoa leseni za mabaa, vilabu na vituo vya burudani.

  • Tags

You can share this post!

Vijana wa kurandaranda mtaani watupa mwili katika lango la...

Machifu na wakuu wa askari watakaoshindwa kuzima pombe...

T L