• Nairobi
  • Last Updated October 1st, 2023 9:40 PM
Gaucho amlilia Uhuru Kenyatta amjengee nyumba

Gaucho amlilia Uhuru Kenyatta amjengee nyumba

Na WINNIE ONYANDO

RAIS wa Bunge la Mwananchi Calvince Okoth almaarufu Gaucho sasa anataka Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta amjengee nyumba.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Gaucho alisema kuwa hana haja na gari.

“Ombi langu kubwa ni kujengewa nyumba. Hakuna haja niendeshe gari kubwa ilhali sina nyumba ya kuishi,” Gaucho alisema.

Mwanasiasa huyo alisema kwamba amechoka kulipa kodi ya nyumba na anatamani tu kuwa na nyumba nzuri jijini Nairobi.

“Ningependa kuishi katika nyumba nzuri. Kwa sasa gari sio la muhimu kwangu.”

Wakati wa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wa Chama cha Jubilee (NDC) katika uwanja wa Ngong Racecourse, Nairobi mnamo Mei, 22, 2023, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta aliahidi kumnunulia Gaucho chakula cha mchana ‘lunch’ kwa ukakamavu wake kusimama naye kupigania chama cha Jubilee.

Hatua hiyo ilizua hisia tofauti katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

Siku chache tu baada ya NDC ya Jubilee, Gaucho alikamatwa kwa madai ya kueneza maneno ya uchochezi.

Aliachiliwa saa chache baada ya vigogo wa Azimio la Umoja One Kenya kutoa makataa aachiliwe Mei 24, 2023.

Gaucho ambaye amekiri kwamba ana nia ya kuwania kiti cha ubunge Lang’ata mwaka wa 2027, amekamatwa mara kadhaa katika muda wa miezi mitatu iliyopita.

Mbunge wa sasa Lang’ata ni Felix Oduor maarufu kama Jalango, aliyechaguliwa mara ya kwanza Agosti 2022 kupitia tikiti ya ODM.

Gaucho ni mfuasi sugu wa Kiongozi wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga na amekuwa katika mstari wa mbele wakati wa maandamano ya muungano huo.

  • Tags

You can share this post!

Kituo cha kwanza kuchajia magari ya umeme Nakuru

Nakuru yapokea mitungi ya Oksijeni kuboresha huduma za afya

T L