• Nairobi
  • Last Updated October 1st, 2023 9:40 PM
Gaucho: Uhuru hajaninunulia gari

Gaucho: Uhuru hajaninunulia gari

Na WINNIE ONYANDO

RAIS wa Bunge la Mwananchi Calvince Okoth almaarufu Gaucho amepuuzilia mbali madai kuwa Rais Mstaafu, Uhuru Kenyatta alimnunulia gari.

Akizungumza na Taifa Leo, Gaucho ambye alikuwa katika mstari wa mbele wakati wa maandamano ya Azimio la Umoja alisema kuwa hajapokea ‘zawadi’ ya Bw Kenyatta.

“Sijanunuliwa gari na Bw Kenyatta. Nilifaa kukutana naye ila sijaenda,” akasema Gaucho.

Haya yanakuja siku chache baada ya picha kuibuka mtandaoni kuwa Bw Kenyatta amemzawadi Gaucho gari aina ya Toyota Land Cruiser V8.

Alisema kwamba alijadiliana na Kiongozi wa ODM Raila Odinga kuhusiana na hilo na wakakubaliana kuwa atamtembelea Bw Kenyatta wiki ijayo.

“Bw Odinga ni kiongozi wangu. Hii ndio maana lazima nijadiliane naye kwanza kabla ya kumtembelea Bw Kenyatta. Tulikubaliana kuw nitaenda kumuona wiki ijayo,” Gaucho akaambia Taifa Leo.

Wiki jana wakati wa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wa Chama cha Jubilee lililofanyika katika uwanja wa Ngong Racecourse, Bw Kenyatta, ambaye ni kiongozi wa chama hicho, aliahidi kumnunulia Gaucho ‘chakula cha mchana’ kwa kusimama naye na kutetea chama cha Jubilee.

“Niliskia wakisema natembea na watu kama Gaucho, wewe ni mtu mzuri sana Gaucho. Umeshinda wengi kwa sababu ulinisaidia kutetea chama cha Jubilee. Wakati mwingine tukikutana, nitakununulia ‘lunch’,” Bw Kenyatta alisema kwenye mkutano huo.

Katika mahojiano ya hapo awali, Gaucho alimtaja Bw Kenyatta kuwa rafiki yake mkubwa.

“Yeye (Bw Kenyatta) alikuwa rais wetu. Mimi pia ni rais wa Bunge la Mwananchi. Sisi sote ni viongozi na ndiyo maana namwita rafiki yangu,” Gaucho alisema.

 

  • Tags

You can share this post!

Mswada wachanganya Wabunge upande wa UDA

Kituo cha kwanza kuchajia magari ya umeme Nakuru

T L