• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
Gharama ya maisha yasukuma wanafunzi wa vyuo vikuu kugeukia ukahaba

Gharama ya maisha yasukuma wanafunzi wa vyuo vikuu kugeukia ukahaba

NA RICHARD MAOSI

GHARAMA ya juu ya maisha imewasukuma baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu Nakuru kugeukia biashara ya ukahaba.

Kufuatia uchunguzi wa Taifa Leo Dijitali, jijini Nairobi, Naivasha, Thika na Nakuru imebainika shughuli yenyewe inaendeshwa kwa siri kubwa nyakati za mchana na waziwazi ifikapo ifikapo usiku.

Safari yetu katika baadhi ya ngome zao eneo la Gusii Street na Three Ways Nakuru mjini, ilikumbana na changamoto tele baadhi yao wakitimua mbio kila tulipojitahidi kutafuta fursa ya kuzungumza nao.

Tunafanikiwa kukutana na mwendeshaji bodaboda katika barabara ya Kanu Street viungani mwa mji wa Nakuru ambaye anatufichulia kuwa wateja wengi wanapendelea makahaba ambao ni wanafunzi wa vyuo kwa sababu wanaitisha hela kidogo.

Anasema biashara huwa nzuri kila siku ya Ijumaa shughuli za uchukuzi katika steji zinazopakana na vyuo vikuu huwa zimejaa wanafunzi wanaoelekea Nakuru mjini au Salgaa.

Wakati mwingi, waendeshaji bodaboda ndio wamekuwa wakiwaelekeza kwa wateja wao na sio rahisi kugundua endapo bishara hii inaendelea labda uwe makini sana.

Anasema makahaba wengi ambao ni wanafunzi wa vyuo wenye umri kati ya miaka 19 na 24, hutumia kumbi za burudani kunasa wateja, hata ingawa wakati mwingine biashara yenyewe huwatumbukiza hatarini ikizingatiwa kuwa huendeshwa nyakati za usiku na baadhi ya wateja huwa na nia mbaya.

Miezi miwili iliyopita Naivasha – eneo la Maai Mahiu na Giligil zilishuhudia ongezeko la idadi ya makahaba wachanga, ambao baadhi wamekuwa wakiungama ni wanafunzi, hii ikitokana na kiwango cha juu cha umaskini na ukosefu wa ajira.

Baadhi yao wamehitimu na wengine wanaendelea na masomo

Wahusika wakuu ni wanafunzi kutoka vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, ambao wamekuwa wakimiminika katika sehemu hizi za kitalii kutafuta wazungu.

Paul Tarus (sio jina halisi) ambaye ni mwendeshaji lori la masafa marefu kutoka Mombasa hadi mpaka wa Rwanda, anasema sio mara moja wamekuwa wakishuhudia visa vya makahaba wachanga kung’ang’ania wateja na wale wakongwe.

Anasema maeneo mengine yaliyoathirika ni Kihoto , Elementaita , Kikopey na Karagita ambapo anawalaumu wazazi kwa kuwapatia watoto wao uhuru mkubwa kupita kiasi.

 

  • Tags

You can share this post!

Mwanafuzi aliyeshambuliwa na mpenziwe achangiwa bili ya...

Azimio yakashifu serikali ikiihusisha na utekaji nyara wa...

T L