• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 AM
GK, mbunge wa Ndia apiga jeki Mswada wa Fedha 2023

GK, mbunge wa Ndia apiga jeki Mswada wa Fedha 2023

NA SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Ndia, Kirinyaga, George Macharia Kariuki almaarufu GK ametangaza kuunga mkono Mswada tata wa Fedha 2023.

Kulingana na mbunge huyo, upitishaji mswada huo utasaidia serikali ya Kenya Kwanza kutekeleza miradi ya maendeleo kama alivyoahidi Rais William Ruto wakati wa kampeni 2022.

Akipigia debe mswada huo, Bw Kariuki pia amesema utafanikisha ulipaji madeni yanayokodolea nchi macho.

“Ninaomba Wakenya wakubali tulipe ushuru, ili kuiwezesha serikali kufanya maendeleo na kulipa madeni,” mbunge huyo alisema mnamo Jumapili, Juni 4, 2023.

Alisema hayo wakati akizungumza katika ibada ya misa Kanisa la KAG, Sagana, Kaunti ya Kirinyaga, ambayo ilihudhuriwa na Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki.

Bw Kariuki ni mwenyekiti kamati ya uchukuzi bungeni, na alisema anapitia wakati mgumu akijikuna kichwa jinsi madeni yanayodaiwa na wanakandarasi waliopewa tenda kuunda barabara nchini yatakavyolipwa.

“Kibarua tulichonacho katika kamati ya uchukuzi bungeni ambayo ninaongoza kama mwenyekiti ni namna ya kulipa madeni,” alisema mbunge huyo wa UDA.

Mswada wa Fedha 2023 umesababisha mjadala moto nchini Wakenya wakipinga kupitishwa kwa mapendekezo yaliyomo.

Mswada huo aidha unapendekeza nyongeza ya ushuru (VAT) wa mafuta ya petroli, kutoka asilimia 8 ya sasa hadi 16.

Vilevile, unapendekeza wafanyakazi kutozwa aslimia 3 ya mshahara , fedha hizo Rais William Ruto akisema zitaelekezwa katika mpango wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu.

Kinara wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga aliye pia kiongozi wa ODM, ameapa kushawishi wabunge wa upinzani kuangusha mswada huo.

Bw Kariuki hata hivyo anasema upinzani unahadaa Wakenya wasipate maendeleo.

“Msisikilize yale upinzani inasema, inahadaa wananchi kuhusu Mswada wa Fedha 2023.”

Endapo mswada huo utapitishwa, gharama ya maisha inatarajiwa kuongezeka mara dufu.

  • Tags

You can share this post!

Wahalifu Mlima Elgon kuona cha mtema kuni

Waziri Kindiki aapa Mackenzie ataozea jela

T L