• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
‘Ground’ mbovu waziri Linturi naye akidai hakuna Mkenya anayelala njaa

‘Ground’ mbovu waziri Linturi naye akidai hakuna Mkenya anayelala njaa

NA MWANGI MUIRURI

WAZIRI wa Kilimo Mithika Linturi amewashtua wengi kwa kudai kwamba hakuna Mkenya anayelala njaa kwa kukosa chakula hapa nchini.

Akiongea katika eneobunge la Igembe ya Kati katika Kaunti ya Meru, waziri Linturi alitangaza kwamba “hakuna shida hiyo ambayo watu wanasema”.

“Mvua ambayo imenyesha imesaidia familia nyingi kupata mimea aina ya mboga na nafaka,” akasema Bw Linturi.

Bw Linturi alisema kwamba hali ngumu ya maisha inayokadiriwa kuvuma nchini imebuniwa na waliobobea katika ‘fani ya kulalamika’.

“Tusiwe watu tu wa kulalamika… hali si mbaya jinsi inavyosemwa na mvua tuliyopata kwa msimu jana na wa sasa imesaidia kuzidisha mavuno ya mahindi,” akasema.

Bw Linturi aliongeza kwamba kuanzia Januari 2024, bei ya unga huenda iteremke hadi Sh100 kwa kuwa mpango wa bei nafuu wa fatalaiza umesaidia kuzidisha mavuno ya mahindi katika maghala ya kitaifa.

Waziri wa Kilimo na Ustawishaji wa Mifugo alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo na Ustawishaji wa Mifugo mnamo Novemba 20, 2023. PICHA | DENNIS ONSONGO

Wakenya ambao huishi katika miji walijibu kwa ghadhabu katika mitandao ya kijamii wakishindwa kuelewa kana kwamba Bw Linturi anafahamu kwamba mijini kwa kiasi kikubwa, hakuna wakulima.

“Mtazamo wa Bw Linturi ni duni na usiofaa kwa mtu wa hadhi hiyo ya waziri. Dunia inatazamia kusaidiwa na walio na nyadhifa kama huyo Bw Linturi kupata jibu la janga la njaa linalokodolea binadamu macho halafu anajitokeza akiongea hivyo,” akasema Bw Morris Waweru kutoka Murang’a Mjini.

Bw Waweru alimtaka waziri aelewe kwamba mjadala wa maisha kuwa magumu hauzingatii mambo ya lishe peke yake.

“Tunaongea kuhusu suala pana la bajeti. Suala la pato na mfumko wa bei. Hata tukila, tunahitaji karo, pesa za kodi ya nyumba, mahitaji mengine kama ya uchukuzi, afya, mavazi… na wakati tunajaribu kugharimia hayo yote ndani wa ushuru hasi wa serikali hii kwa bidhaa muhimu na pia kwa waajiri hakuna mjadala kwamba hayo yote yanatishia uthabiti wetu kimfuko na maisha yanaishia kuwa magumu,” akasema.

Wengi katika majukwaa ya mitandao ya kijamii waliwataka maafisa wa serikali ya Kenya Kwanza inayoongvozwa na Rais William Ruto wazingatie umakinifu wa kimaongezi hadharani na waelewe kazi waliyo nayo ni kubwa kuliko ya kurandaranda wakiongea visivyo kwa njia ya kukera na kukejeli wananchi wanaohangaika.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Pochettino adai Chelsea sasa imeiva kutambisha Carabao

Namna ya kuandaa nyama ya mutura kulika msimu wa Krismasi

T L