• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 12:59 PM
GWIJI WA WIKI: Abdurahim Ali Bakathir

GWIJI WA WIKI: Abdurahim Ali Bakathir

Na CHRIS ADUNGO

WATAALAMU wa lugha wanakadiria kuwa idadi ya wazungumzaji wa Kiswahili kote ulimwenguni imefikia watu milioni 150. Hata hivyo, lugha hii hutumiwa na watu wengi bila kujua ilikotokea.

Zipo nadharia kadhaa kuhusu asili ya Kiswahili – kuwa Kiswahili kimetokana na Kiarabu; kuwa ni mchanganyiko wa Kiarabu na lugha za Kibantu; na kuwa ni lugha ya Kibantu iliyoathiriwa sana na Kiarabu kimsamiati. Wengine wamedai kuwa Kiswahili kilitokana na mchanganyiko wa lugha kadhaa za Kibantu zilizokuwa katika upwa wa Afrika Mashariki.

Nadharia kuwa Kiswahili kilitokana na Kiarabu inaegemea sana wingi wa maneno yenye asili ya Kiarabu na dini ya Kiislamu. Inadaiwa kwamba kwa kuwa Kiswahili kilianzia pwani, na kwa kuwa idadi kubwa ya wakazi wa pwani ni Waislamu, na kwa kuwa Uislamu uliletwa na Waarabu; basi Kiswahili nacho kinashabihiana na Kiarabu.

Abdurahim Ali Bakathir ni miongoni mwa wataalamu na watafiti wa lugha wanaosema madai haya hayana mashiko yoyote kwani Kiswahili ni lugha kamili ya Kibantu iliyokopa maneno kutoka Kiarabu, Kiajemi, Kireno, Kihindi, Kijerumani, Kiingereza n.k kutokana na mawasiliano ya karne nyingi kati ya wenyeji wa pwani na wafanyabiashara wa kigeni.

“Mabadiliko yalihusu msamiati tu wala si maumbo ya maneno au miundo ya tungo za Kiswahili. Kiswahili kilitumia maneno mengi kutoka lugha za Kibantu kwa kuwa wasemaji wengi wa Kiswahili ni Wabantu,” anasema.

“Lugha kuwa na maneno mengi ya kukopa kutoka lugha fulani si ithibati kwamba lugha moja imetokana na nyingine. Inabidi kuzingatia zaidi msingi wa lugha kwa vigezo vya kiisimu – fonolojia, mofolojia, sintaksia na semantiki,” anasisitiza.

Vipengele ‘vinavyohalalisha’ nadharia kuwa Kiswahili ni Kibantu ni ushahidi wa kiisimu na wa kihistoria. Kiisimu, Kiswahili kina utaratibu maalumu wa sauti za irabu na (au) konsonanti katika kuunda silabi, maneno, nk.

Kwa mujibu wa Bakathir, watu wa kwanza kufika pwani ya Afrika Mashariki ni makabila mawili ya jamii ya Wangozi – Wabarawa (Wamiini) waliotumia lahaja ya Chimbalazi na Wabajuni (Watikuu) kutoka Shungwaya.

Wangozi walitokea mjini Harar, Ethiopia Mashariki. Walianza kuitwa Waswahili baada ya kufikiwa na mgeni Muhammad Ibn Battuta aliyesema “hawa watu ni wa fukwe za pwani” akilenga Wa-Amu kwamba ndio wenye lugha ya Kiswahili.

“Kwa hivyo, si kweli kwamba Waswahili wamezaliwa na Wamijikenda kwa sababu Wamijikenda walitokea Afrika ya Kati na wakakaribishwa na Waswahili pale Shungwaya,” anasema kwa kusisitiza kuwa nchi ya Waswahili (Swahililand) ni maili 12 kutoka ufukwe wa pwani kupanda juu bara na kuanzia Lunga-Lunga hadi mji wa Mogadishu, Somalia.

“Waswahili ni jamii ya makabila 17 ambayo yamepasua kingo kutoka pwani na kuenea katika sehemu mbalimbali kisha kupanua mawanda na maana ya ‘Mswahili’. Sasa tuna Waswahili asili, wazawa na waridhiwa wanaoelewana kilahaja.”

Bakathir alizaliwa 1946 mtaani Pumwani, Nairobi katika familia ya Bw Ali Mahfudh na marehemu Bi Somoye Abubakar.

Amezuru zaidi ya mataifa 20 ya Uarabuni pamoja na bara Ulaya, Asia na Afrika kwa minajili ya utafiti na kuchangia mijadala ya kitaaluma kuhusu asili ya Kiswahili. Amejaliwa watoto watatu – Farid, Fateh na Muhammad.

You can share this post!

Jinsi Spika Justin Muturi alivyosherehekea na akina mama...

Korti yaombwa imtimue msimamizi wa Mumias Ramana Rao

T L