• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
GWIJI WA WIKI: John Kinyua

GWIJI WA WIKI: John Kinyua

NA CHRIS ADUNGO

SENETA Maalumu, Bw Isaac Mwaura, alipoondolewa kwa muda kwenye orodha ya maseneta mnamo Mei 2021 baada ya chama cha Jubilee kumtimua, Bw John Kinyua Nderitu wa Laikipia aliteuliwa kujaza pengo lake katika jopo la maseneta wanne wasaidizi wa spika.

Kuteuliwa kwa Bw Kinyua aliyeungana na Bi Rose Nyamunga, Bw Steve Lelegwe na Bi Judith Pareno katika jopo hilo ambalo husaidia spika na naibu wake kuendesha vikao vya bunge la seneti, kulichochewa zaidi na ukubwa wa uwezo na upekee wa umilisi wake wa Kiswahili.

Bw Mwaura aliyerejea Seneti mnamo Disemba 2021 baada ya Mahakama ya Juu kubatilisha maamuzi ya awali ya Jubilee kumtimua, alikuwa kivutio cha wengi kutokana na hatua yake ya kuendesha vikao vya bunge kwa Kiswahili.

“Ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili katika seneti iliamshwa na Bw Mwaura – spika wa kwanza aliyetumia lugha hii kupitisha sheria mnamo Oktoba 2020. Nami niliegemea zaidi upande wa Kiswahili wakati wa vikao vya seneti,” anasema Bw Kinyua.

“Wakenya wengi wamekuwa wakifuatilia matukio katika seneti kwa kuwa wanaelewa kinachoendelea kwenye mijadala. Kuzungumza Kiswahili bungeni ni ishara ya viongozi kumjali mwananchi wa kawaida.”

“Ni kinaya kwa maseneta kutotumia Kiswahili bungeni kwa kisingizio cha kuogopa kuboronga lugha. Mbona sasa wanakitumia kuomba kura msimu huu wa uchaguzi? Haja kubwa hapa si lafudhi wala ufasaha, bali ni kujieleza,” anasisitiza.

Kinyua alilelewa katika kijiji cha Kiamariga, eneo la Rumuruti, Kaunti ya Laikipia. Ndiye wa nne kuzaliwa katika familia ya watoto saba wa Bw William Nderitu na Bi Lucy Wanjogu.

Kwa pamoja na mkewe Bi Phoebe Kirigo, wamejaliwa watoto wanne – William Nderitu, James Kegundu, Luciana Wanjogu na Francis Ngatia.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Kiamariga kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Gatero iliyoko Ng’arua, Nyahururu.

Ingawa alitamani kuwa mwalimu au mwanahabari, alisomea Biokemia katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Alirejea baadaye chuoni humo kusomea shahada ya uanasheria (2013-2022).Mbali na Bw Kuria aliyempokeza Kinyua malezi bora ya kiakademia shuleni Kiamariga, walimu wengine ambao walimtandikia seneta huyu zulia zuri la Kiswahili ni Bw Gicheru na Bw Wachiuri waliomfundisha katika shule ya sekondari.

Baada ya kuhitimu chuoni, Kinyua alipata kibarua cha kufundisha katika shule ya upili ya Mutara, Rumuruti (1998-2002). Aliajiriwa baadaye kuwa mfamasia katika kampuni ya Europa Healthcare, Nairobi (2003-2005) kisha Laborex Kenya Ltd, Nairobi (2005-2013).

Alichaguliwa kuwa Seneta wa Laikipia mnamo 2017 baada ya kutofaulu katika jaribio la kwanza 2013.

“Kiswahili kilichangia pakubwa kuchaguliwa kwangu. Nilifuta kasumba ya wengi waliochukulia Kiswahili kuwa lugha ya watumwa na watu ambao hawajasoma. Natumia akili zaidi kuongea kwa Kiingereza na moyo wangu zaidi kuzungumza kwa Kiswahili,” anasisitiza.

Bw Kinyua anahimiza Wakenya kukumbatia Kiswahili kwa sababu mawanda yake katika soko la ajira yamepanuka.

“Kiswahili kimekua na kupiga hatua kubwa kimataifa. Vyuo vikuu nchini Kenya vinafaa kuweka misingi ya kufundisha lugha hii kwa hadhi na viwango vitakavyokabiliana na kasi ya ukuaji wake duniani,” akashauri.

Anasema Kiswahili kinastahili kuchangamkiwa na wabunge wote bila kujali sehemu wanakotokea.

“Hakujawahi kutokea spika ambaye amekumbatia sana matumizi ya Kiswahili bungeni. Hata spika wa kwanza wa seneti, Timothy Chitasi Chokwe, aliyehudumu kati ya 1963 na 1966, hakutumia Kiswahili kuendesha shughuli na vikao vya bunge licha ya kuwa mzaliwa wa Pwani,” anaongezea.

  • Tags

You can share this post!

Watetezi washinikiza Gachagua, viongozi 13 wazuiwe kuwania

Kura: Baadhi ya kampuni Industrial Area zaruhusu...

T L