• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
GWIJI WA WIKI: Tabitha Manzi

GWIJI WA WIKI: Tabitha Manzi

Na CHRIS ADUNGO

USIOGOPE kukosea. Kupotea njia ndiko kujua njia. Jaribu tu. Ipo siku ambapo mghafala utaisha. Zidi kumulika uendako kwa hekima na tabasuri. Utaziona fanaka foko ukivuta subira na kujiamini.

Wengi wanaotaka kuogelea katika bahari pana ya uandishi hutishwa na maji marefu. Huogopa papa na nyangumi wasijue kuwa maji hayabagui.

Mawimbi pia huwatisha wengi wakabaki tu kuchungulia. Je, ni nani asiyejua kuwa mchungulia baharini si msafiri? Sote twajua kuwa penye mawimbi ndipo penye milango – milango ya baraka belele.

Kuandika kwahitaji utafiti na utafitafi mwingi, kusomasoma kwingi na mazoezi mengi ya uandishi. Masuala chungu nzima ya kuandikwa yanajianika katika jamii yetu kila siku. Yatumie kuvitunga visa kwa ubunifu. Soko ni kubwa. Wajibika, jitume na mambo yatajipa.

Siri kubwa ya mafanikio ni kujitolea sabili katika uchapakazi. Kataa ugoigoi na uzembe. Kumbatia bidii ili ufue dafu katika hicho unachokifanya.

Upekee ni muhimu sana katika uandishi. Zama hizi kunao ukuruba mkubwa baina ya kazi zilizochapishwa awali, zichapishwazo na labda zijazo. Huko ni kuonesha jinsi uigaji wa kikasuku unavyotutawala katika ulingo wa uandishi. Nadhani chanzo cha hayo ni tamaa.

Tamaa ya kutaka kuwa jina kubwa kabla ya wakati kuwadia. Tamaa ya kutaka kukimbia kabla ya kutambaa. Tamaa ya kujiweka kwenye hadhi ya juu kabla ya kupanda ngazi hatua kwa hatua.

Kabla ya kuandika, jiulize wataka kuandika nini? Wataka kuandikia nani? Wataka kuandika vipi? Wataka kuandika kwa sababu gani?

Huu ndio ushauri wa Bi Tabitha Mawia Manzi – mwanafasihi chipukizi na mlezi wa vipaji ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika Chuo cha Kimataifa cha Mafunzo ya Ualimu cha Kitengela, Kaunti ya Kajiado.

MAISHA YA AWALI

Manzi alizaliwa mnamo Mei 20, 1996 katika kijiji cha Ngungani, eneo la Mwingi, Kaunti ya Kitui. Ndiye mtoto wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto saba wa Bi Rosemary Manzi na Bw Timothy Manzi.

Safari yake ya elimu ilianzia katika Shule ya Msingi ya Ngungani alikosomea kati ya 2001 na 2006 kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya St Francis Kamuwongo Academy, Kitui mnamo 2007 akiwa mwanafunzi wa darasa la tano.

Alama nzuri alizozipata katika Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mnamo 2010 zilimpa nafasi katika Shule ya Upili ya Kangaru Girls, Kaunti ya Embu mnamo 2011. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) mwishoni mwa mwaka wa 2014. Manzi alisomea ualimu (Kiswahili na Dini) katika Chuo Kikuu cha Kenyatta kati ya Septemba 2015 na Julai 2019.

Zaidi ya wazazi wake, mwingine aliyemshajiisha maishani na kumhimiza ajitahidi masomoni ni kaka yake Bw Christopher Kitheka ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya Nyanyaa, Kitui.

Manzi anakiri kuwa ukubwa wa mapenzi yake kwa taaluma ya ualimu ni zao la kuhamasishwa na aliyekuwa mwalimu wake wa Kiswahili katika shule ya msingi, Bw Michael. Kariha na ilhamu zaidi ilichangiwa na Bi Kalange wa Kangaru Girls pamoja na wahadhiri waliotangamana naye kwa karibu sana, kumpokeza malezi bora ya kiakademia na kupanda ndani yake mbegu zilizootesha utashi wa kukichangamkia Kiswahili akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Hawa ni pamoja na Dkt Hamisi Babusa, Dkt Miriam Osore, Dkt Timothy Arege, Dkt Joseph Gakuo, Dkt Jacktone Onyango, Prof Kitula King’ei na Prof Ireri Mbaabu.

Kwa hakika, ufanisi unaojivuniwa sasa na Manzi katika Kiswahili umechangiwa pakubwa na tukio la yeye kufundishwa na watu ambao ni wabobevu na wapenzi kindakindaki wa lugha hii.

UALIMU

Kabla ya kuajiriwa na Chuo cha Kimataifa cha Mafunzo ya Ualimu cha Kitengela mnamo Januari 2020, Manzi alikuwa pia amefundisha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Mwihoko, eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu. Alihudumu huko kwa kipindi kifupi kati ya Januari na Aprili 2019.

Anashikilia kwamba, kufaulu kwa mwanafunzi katika somo lolote hutegemea mtazamo wake kuhusu somo husika na mwalimu anayemfundisha darasani.

UANDISHI

Manzi anaamini kuwa safari yake ya uandishi ilianza alipokuwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Ni katika kipindi hicho ambapo nyingi za insha alizoziandika zilimvunia tuzo za haiba kubwa kutoka kwa walimu wake wa Kiswahili.

Alitunga pia idadi kubwa ya mashairi yaliyofana katika mashindano ya viwango na ngazi mbalimbali kiasi cha kumpa fursa ya kupanda majukwaa tofauti ya makuzi ya Kiswahili.

Kufikia sasa, Manzi anajivunia kuandika na kuchapishiwa hadithi fupi kadhaa katika diwani mbalimbali. Ameshiriki pia uhariri wa kazi kadhaa za kibunifu za mwandishi Dominic Maina Oigo pamoja na kitabu cha Gredi ya Nne kilichoandikwa na Dkt Arege mnamo 2019 kwa minajili ya Mtaala Mpya wa Umilisi (CBC).

Baadhi ya hadithi ambazo Manzi amechangia vitabuni ni ‘Kifo cha Rehema’ katika diwani ya ‘Kilele cha Mambo na Hadithi Nyingine’ iliyochapishwa na African Ink Publishers, ‘Msafiri’ katika diwani ya ‘Mapenzi ya Pesa na Hadithi Nyingine’ iliyochapishwa na Williams Publishers Ltd na ‘Hali Yangu’ katika mkusanyiko wa ‘Siwezi Tena na Hadithi Nyingine’ uliofyatuliwa na Chania Publishers.

Hadithi nyinginezo ni ‘Wema Hauozi’ katika diwani ya ‘Mtoto wa Dhahabu’ iliyochapishwa na Bestar Publishers na ‘Bamkwe’ katika diwani ya ‘Mkaguzi wa Shule na Hadithi Nyingine’ iliyotolewa na kampuni ya Education Distinction. Ameandika pia kazi nyingi bunilizi zitakazochapishwa hivi karibuni.

Mbali na Bw Oigo na Bw Timothy Omusikoyo Sumba, mwingine aliyemwamshia Manzi ari ya kutunga kazi za kibunifu kwa Kiswahili ni marehemu mjomba wake, Bw Eric Kyallo. Wengine ni Bi Viola Wambui na Bi Linah Ntinyari waliokuwa wanafunzi wenzake katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

DRAMA

Zaidi ya kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa somo la Kiswahili miongoni mwa wanafunzi wake, Manzi amekuwa akiwashirikisha wanafunzi hao wa kiwango cha stashahada (PTE) na diploma (DTE) katika mashindano mbalimbali ya kuigiza.

Yeye mwenyewe aliwahi kushiriki mashindano mengi ya muziki na drama akiwa mwanafunzi wa shule ya upili na akaongoza Kangaru Girls kutawazwa mabingwa wa kitaifa katika tamasha hizo kati ya 2012 na 2014.

Chini ya uelekezi wa Bi Kalange, Manzi alishiriki pia mashindano ya kutoa hotuba na akawa miongoni mwa wanafunzi walioigiza riwaya ya ‘Kidagaa Kimemwozea’ (marehemu Prof Ken Walibora) iliyowahi kutahiniwa katika shule za sekondari nchini Kenya kati ya 2014 na 2017.

JIVUNIO

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai ndoto za kuwa profesa, mwandishi maarufu na mhadhiri wa chuo kikuu, Manzi anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala waandishi wengi chipukizi ambao wametangamana naye katika makongamano mbalimbali ya Kiswahili.

You can share this post!

Hazina za wanawake, vijana kuunganishwa

Broadways yazindua mkate usio na sukari