NA MERCY KOSKEI
WANANDOA walio na ulemavu wa kuskia (viziwi) na kuzungumza (bubu) kutoka Kaunti ya Nakuru Jumapili, Mei 28, 2023 walifunga pingu za maisha katika hafla iliyovutia umati mkubwa uliofika kushuhudia wawili hao wakilishwa kiapo kuwa mke na mume.
Akiwa amevalia gauni jeupe, Bi Jenifer Wanja Maina, 24, huku amesindikizwa na wazazi wake, alitembea kwa madaha hadi kwenye madhabahu ambapo mumewe Bethwel Kinyua ,41, alikuwa akimsubiri kwa hamu na tabasamu.
Katika hafla hiyo ya kipekee, Bi Wanja na Bw Kinyua walibadilishana nadhiri katika kanisa la Katoliki la St Francis Kiti, eneobunge la Nakuru Mashariki.
Katika misa iliyoongozwa na Padre Vincent Makhoha, akisaidiwa na mtafsiri, bibi na bwana harusi, waumini na jumuiya ya viziwi walifuatilia matukio ya hafla hiyo.
Watafsiri wa ishara walikuwepo kila kona ili kusaidia jumuiya ya viziwi waliofika kushuhudia harusi hiyo.
Wanja na Kinyua walivaa tabasamu nyusoni mwao huku wakishikana mikono mara kwa mara, ishara tosha ya mapenzi kunoga.
Padre Makhoha alieleza kwamba mtafsiri wa ishara angetafsiri maneno yake katika lugha ya ishara ili wale wenye matatizo ya kuskia waweze kufuatilia Ibada.
Wawili hao hatimaye walibadilishana viapo vyao vya ndoa, huku shangwe, vifijo na nderemo zikitawala.
Baada ya kuashiria muungano wao kwa kuvishana pete, wapenzi hao walitia saini cheti chao cha ndoa ili kukamilisha itifaki za kidini na za kisheria.
Kulingana na bwana harusi, wawili hao walikutana katika hafla ya kanisa eneo la Mukurweini, Kaunti ya Nyeri 2022.
Baada ya kujuana, wakawa marafiki na baadaye ukazaa uhusiano wa kimapenzi.
Alisema walianza kuchumbiana, huku Bw Kinyua akikutana na wazazi wa Bi Wanja kabla ya kupanga harusi ya kitamaduni ya Wakikuyu.
“Punde tuu macho yangu yalikutana na yake nilijua tuu atakuwa mke wangu, nilianza kumfuatilia na baadaye alinikubalia na leo (Mei 28, 2023) tupo hapa kanisani tunakula kiapo cha ndoa, tunashukuru waumini kwa kutushika mikono siku hii maalum,” bwana harusi aliambia kanisa.
Kwa upande wake, Bi Maina anayetoka eneo la Machine Mjini Nakuru, alisema kuwa safari yao haijakuwa rahisi.
Alisema kuwa walifanya mapenzi yao kustawi kupitia ujumbe mfupi wa simu ambao ni sehemu kubwa ya mawasiliano kati yao, na kuongeza kuwa hawajali kile ambacho watu wanafikiria juu ya uhusiano wao.
“Sisi ni kama wanandoa wengine, nina furaha leo kwani hatimaye nimefunga ndoa na rafiki yangu wa karibu. Ni mtu mzuri, anayenipenda na kunijali,” alisimulia.
Wazazi wao hawakuficha furaha yao, mamake bi harusi Mercy Wambui akikumbuka jinsi bintiye alivyopasua mbarika kwamba alikuwa amepata mchumba aliyetaka kumuoa.
Alisema kuwa Bi Wanja, ambaye ni bintiye wa pekee, alimwambia kwamba punde watakapomaliza harusi yao ya kitamaduni watafunga ndoa kanisani.
“Tumekuwa tukingoja siku hii. Nina furaha kwamba mwanangu sasa ameolewa. Ninawatakia kila la heri na baraka za Mungu katika maisha yao mapya,” babake bwana harusi Bw Titus Kinyua alisema.