• Nairobi
  • Last Updated October 1st, 2023 9:40 PM
JAMVI LA SIASA: Ruto angemtumia Kalonzo kuatika mbegu ya udikteta

JAMVI LA SIASA: Ruto angemtumia Kalonzo kuatika mbegu ya udikteta

NA CHARLES WASONGA

JUHUDI za Rais William Ruto za kutaka kumvutia kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka katika serikali yake ya Kenya Kwanza imetajwa kama njama ya kurejesha nchi hii katika utawala udikteta wa chama kimoja.

Aidha, wadadisi wa masuala ya kisiasa waliozungumza na safu hii wanasema pendekezo lake kwamba vyama tanzu katika muungano wa Kenya Kwanza (KKA) vivunjwe ili kuunda chama kimoja cha United Democratic Alliance (UDA) ni sehemu ya mpango wa kufikia lengo hilo.

Mwenyekiti wa UDA Johnstone Muthama na Katibu Mkuu Veronica Maina wamekubali kwamba wazo hilo limetoka kwa “safu ya juu ya uongozi wa Kenya Kwanza”.

“Wazo hilo linaungwa na uongozi wa Kenya Kwanza, kwa misingi kuwa ni bora kwa sisi sote kuwa wanachama wa chama kimoja. Tayari Chama Cha Kazi kimekubali kujiunga na UDA,” Bw Muthama akanukuliwa akisema Septemba.

Kwa hivyo ufichukuzi wa Rais Ruto wiki jana, kwamba amekuwa akizungumza na Bw Musyoka kwa nia ya kumshirikisha katika serikali yake unasawiriwa kama sehemu ya mpango wa kufikia lengo hilo.

Lengo lake lilikuwa ni kuupa mrengo wake nguvu zaidi kisiasa ili kujipa ushawishi mkubwa, kiasi cha kuweza kufanikisha mageuzi ya Katiba kuendeleza masilahi ya kumfaidi kisiasa.

Akiongea katika ibada ya maombi ya kutoa shukrani katika Kanisa la AIC, Kitui mjini wiki jana, Rais Ruto alisema amezungumza na Bw Musyoka kwa lengo la kumshawishi ajiunge na serikali lakini amehiari kusalia upinzani.

“Stephen ni kakangu mkubwa na atakapokuwa tayari nitafanya kazi naye,” Rais Ruto akasema.

Shirikisha

“Niliwaambia nilipokuwa hapa kwamba Mungu akinijaalia kuwa Rais, nitamshirikisha Stephen katika serikali yangu. Ningetaka mjue kwamba nilimtafuta na tukaketi na kuzungumza. Nilimwomba tufanye kazi naye lakini akasema anataka kuendelea kuwa upinzani,” akaongeza.

Lakini itakumbukwa kwamba mnamo Septemba 16, Rais Ruto alisisitiza kuwa hangeshirikisha kiongozi yeyote wa upinzani katika serikali yake.

Akiongea katika mkutano wa kundi la wabunge wa muungano wa KKA mjini Naivasha, Dkt Ruto alisema baadhi ya mrengo wake kudhibiti bunge la kitaifa na seneti, sasa watalenga kuwahudumia Wakenya.

Hilo, alisema, litatimizwa vizuri kwa kuweka mipaka kati ya serikali na upinzani, ambao utajitwika wajibu wa kuhakikisha utendakazi wa serikali ili kuimarisha uwajibikaji.

“Hii ndio maana tumekubaliana kwamba hatutateua mwanasiasa yeyote wa upinzani serikalini kwa sababu tunatana upinzani wenye nguvu. Tunataka upinzani ambao utahakiki utendakazi wa serikali kwa sababu hatarajii kuficha chochote; tunataka kuendesha serikali itakayowajibika wa raia waliotuchagua,” Rais Ruto akaeleza.

Bw Herman Manyora sasa anasema Dkt Ruto anaonekana kubadili msimamo huo na anataka kudhoofisha kabisa upinzani ili kutumia mamlaka ya urais kuendeleza utawala mbaya.

“Ni marais wanaotaka kuendeleza utawala wa kidikteta ambao husambaratisha na hatimaye kudhoofisha nguvu za vyama vya upinzani, anavyofanya Rais Ruto. Kwa kumwalika Kalonzo ndani ya serikali yake, Rais anapania kuendeleza uongozi usiowajibika kwa yoyote,” anasema mchanganuzi huyo wa masuala ya kisiasa.

Kulingana na Bw Manyora, endapo Rais Ruto atafaulu kumnasa kiongozi huyo wa Wiper, bila shaka idadi ya wabunge wanaoegemea mrengo wa Azimio la Umoja-One Kenya utapuungua na hivyo kupunguza zaidi usemi wa mrengo huo katika upitishaji miswada na hoja.

“Kalonzo akiondoa Azimio bila shaka wabunge na maseneta wa chama cha Wiper wanabadili uamunifu wao kutoka mrengo huo hadi ule wa Kenya Kwanza. Hii ina maana kwamba wabunge wa ODM ndio watasalia Azimio kutekeleza wajibu wa upinzani,” anaongeza.

  • Tags

You can share this post!

MALEZI KIDIJITALI: Chagulia mtoto wako teknolojia inayomfaa

JUNGU KUU: Hofu ya Ruto ‘kutekwa’ na mawaziri...

T L