• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 6:55 PM
JAMVI: Chama cha Kingi hatarini kufungiwa nje kura ijayo

JAMVI: Chama cha Kingi hatarini kufungiwa nje kura ijayo

Na LEONARD ONYANGO

CHAMA cha Pamoja African Alliance (PAA) chake Gavana wa Kilifi Amason Kingi kiko katika hatari kubwa ya kuzuiliwa kusimamisha wawaniaji katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.

PAA ni miongoni mwa vyama 19 ambavyo havijaidhinishwa kuwa vyama kamili na Msajili wa Vyama vya Kisiasa (RPP).

Vyama hivyo 19 sasa vinatumia cheti cha muda na vimezuiliwa kujihusisha na shughuli za kisiasa hadi vitakaposajiliwa kuwa vyama kamili.

Vyama vilivyo na cheti cha muda havikuruhusiwa kuwasilisha sheria za uteuzi wa wawaniaji kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Makataa ya kuwasilisha sheria za uteuzi wa wawaniaji kwa IEBC yalikuwa Jumatatu, Oktoba 18, 2021.

Kulingana na Msajili wa Vyama vya Kisiasa Bi Ann Nderitu, hatima ya chama cha PAA na vingine 18 vilivyo na cheti cha muda, iko mikononi mwa IEBC.

“Iwapo IEBC haitaongeza muda wa kuwasilisha sheria za uteuzi, hiyo ina maana kwamba vyama ambavyo havikuwasilisha sheria za uteuzi wa wawaniaji havitashiriki katika Uchaguzi Mkuu ujao,” Bi Nderitu akaambia Taifa Jumapili.

Vyama vingine vilivyo na tiketi ya muda ambavyo viko katika hatari ya kuzuiliwa kushiriki uchaguzi ujao ni Mkenya Daima Party, Kenya Democracy for Change kinachotumia miwani kama nembo yake, Daraja Redevelopment Party, Msingi wa Utaifa na African Democratic Congress kati ya vinginevyo.

Chama kinapopewa cheti cha muda kinahitajika kutimiza matakwa fulani na kisha kutuma maombi ya kutaka kusajiliwa kuwa chama kamili.

Miongoni mwa matakwa hayo ni kusajili wanachama kutoka maeneo yote ya nchi na kufungua afisi za chama katika angalau kaunti 24 kati ya mengineyo.

Chama kinachoshindwa kutimiza matakwa hayo baada ya siku 180 tangu kupewa cheti cha muda, kinafutiliwa mbali.

Chama cha PAA kilipewa cheti cha muda Julai 21, 2021.

Vyama 83 kati ya 91 ambavyo vimesajiliwa kikamilifu, viliwasilisha sheria za uteuzi wa wagombea kwa IEBC baada kuthibitishwa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa kuwa vimetimiza matakwa ya Katiba na Sheria ya Uchaguzi.

Hiyo inamaanisha kuwa vyama vinane ambavyo havikuwasilisha sheria zake za uchaguzi, havitashiriki Uchaguzi Mkuu ujao.

IEBC inaendelea na shughuli ya kukagua sheria za uteuzi za vyama 83.

Vyama ambavyo kanuni zake za uteuzi zitabainika kukinzana na sheria zitatakiwa kufanya marekebisho ndani ya siku 14.

Kufikia Novemba 15, 2021, IEBC itatoa vyeti kwa vyama ambavyo sheria zake za uteuzi zimeidhinishwa.

“Sheria za uteuzi za vyama vya kisiasa ni sharti zifuate Katiba ya 2010 na Sheria ya Uchaguzi ya 2011. Kanuni za uteuzi zinazokiuka Katiba na Sheria zitakataliwa,” anasema mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati.

Chama cha PAA ambacho kinaungwa mkono baadhi ya madiwani wa Kaunti ya Kilifi, kilionekana kuwa tishio kwa umaarufu wa ODM chake Bw Raila Odinga na United Democratic Alliance (UDA) cha Naibu wa Rais William Ruto.

Mbunge wa Magarini, Bw Michael Kingi pia ametangaza wazi kukiunga mkono kufikia sasa.Gavana Kingi ni miongoni mwa wanasiasa ambao wamekuwa wakisisitiza kubuniwa kwa chama kimoja ambacho kitapigania masilahi ya kanda ya Pwani.

Kufikia sasa, Pwani bado imebaki nyuma wakati ambapo vigogo wa kisiasa wa maeneo mengine wanaendeleza mashauriano ya kuunda miungano.Chama cha PAA, hata hivyo, kimekuwa kikumbwa na pingamizi kubwa kutoka kwa wanasiasa wanaoegemea kambi ya Dkt Ruto.

Miongoni mwao ni mbunge wa Kilifi Kaskazini, Owen Baya, ambaye anashikilia kuwa chama cha PAA hakina maono yoyote mapya kwa Wapwani na kitaifa.

Mbunge huyo aliyechaguliwa kupitia kwa ODM amekuwa akikashifu uundaji wa chama hicho akidai kuwa kinalenga kutumia vibaya hisia za Wapwani kwa manufaa ya viongozi ambao hawataki kutokomea baada ya 2022.

Kulingana naye, wanasiasa wanafaa wawe wanatilia maanani hitaji la kuunganisha Wapwani na jamii nyingine zote kitaifa badala ya kuunda vyama ambavyo vinaonekana kuwa vya kieneo.

Iwapo chama cha PAA kitazuiliwa kushiriki Uchaguzi Mkuu ujao, litakuwa pigo kwa Gavana Kingi ambaye anahudumu muhula wa mwisho.

Gavana Kingi alinuia kutumia chama chake cha PAA kuendelea kuwa na usemi kisiasa katika eneo la Pwani kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.

Bw Kingi katika miezi ya hivi karibuni amekuwa akikwepa Dkt Ruto na Bw Odinga wanapozuru eneo la Pwani.

Chama cha Kadu Asili ambacho kimekuwa kikihusishwa na ukanda wa Pwani, wiki iliyopita kilitangaza kuingia kwenye muungano wa One Kenya Alliance (OKA) na kusambaratisha ndoto ya eneo hilo kutaka kuwa na chama kimoja.

Muungano wa OKA unajumuisha Seneta wa Baringo Gideon Moi (Kanu), Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula.

Mwenyekiti wa Kadu Asili, Joshua Kombora, alisema chama hicho kitakutana na washirika wake katika eneo la Pwani ili kuwaelezea kwa nini waliamua kujiunga na OKA.

You can share this post!

JAMVI: Limuru III: Changamoto tele Mlima ukijaribu kuja...

Mwanamume apatikana amefariki ndani ya chumba kwenye orofa...

T L