• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 3:28 PM
JAMVI: Uhatari wa ‘suti’ kwa Ruto, Raila

JAMVI: Uhatari wa ‘suti’ kwa Ruto, Raila

Na CHARLES WASONGA

HATUA ya Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga kushikilia kuwa wawaniaji wanaounga azma zao za urais sharti wawanie kwa tiketi za vyama vyao huenda ikawakosesha kura mwaka ujao.

Hii, kulingana na wadadisi, ni kwa sababu vyama vingine vidogo hukumbatiwa na wawaniaji ambao hutendewa hiana katika mchujo wa vyama hivi vikubwa. Isitoshe, baadhi ya wawaniaji kama hao, pamoja na wagombeaji wa kujitegemea, huwa na wafuasi sugu wanaowaamini.

Bw Javas Bigambo anasema hali ilithibitishwa katika uchaguzi mkuu uliopita ambapo wabunge wengi walifaulu kuchaguliwa kwa tiketi ya vyama vidogo huku wengine wakishinda kama wagombeaji huru.“Kwa mfano, katika uchaguzi mkuu wa 2017 Rais Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto walifaidi pakubwa kutokana na uungwaji mkono kutoka kwa wagombeaji kama vile Maendeleo Chap Chap cha Gavana Mutua na Frontier Economic Party.

Kwa hivyo, wakati kama huu ni hatari kwa Ruto na Raila kupigia debe mfumo huo maarufu kama ‘six piece’ anaeleza.

VITI VYOTE

Dkt Ruto amekariri kuwa wanasiasa wote ambao wanaunga mkono azma yake ya urais, sharti wawanie viti vyote katika uchaguzi kwa tiketi ya chama United Democratic Alliance (UDA).Isitoshe, amewashauri viongozi wa vyama vidogo na wanaounga mkono azma yake kuvivunja vyama hivyo na kujiunga na chama cha UDA;

pendekezo ambalo wanasiasa hao wamepinga.Naibu Rais amevitaja vyama kama vya kikabila huku akiipa UDA hadhi ya chama cha kitaifa chenye uungwaji mkono kote nchini.Kwa upande wake Bw Odinga amewashauri wafuasi wake kuwapigia kura wagombeaji wa ODM pekee chaguzi za viti vyote vitakavyowaniwa katika uchaguzi mkuu.

Viti hivyo ni; ugavana, useneta, ubunge, mwakilishi wa kike na udiwani.Bw Odinga ameonya kuwa wawaniaji wa vyama vingine pamoja na wagombeaji huru watakosesha ODM fedha ambazo hutolewa na serikali kufadhili shughuli za vyama vya kisiasa.

“Kando na kukosesha chama cha ODM fedha, wawaniaji wa kujitegemea na watatuwekea vikwazo bungeni tukitwaa mamlaka mwaka ujao,” Bw Odinga alisema katika makao makuu ya ODM alipopokea wanasiasa 200 kutoka Kisii waliojiunga na chama hicho.Vile vile, waziri huyo mkuu wa zamani aliwataka wanasiasa wenye nia ya kuhama chama hicho baada ya kupoteza katika mchujo kufanya hivyo mapema.

“Mchujo wetu utaendeshwa kwa njia huru na haki. Kwa hivyo, wale ambao wanashindwa katika shughuli kama hiyo wasalie katika chama kwani watateuliwa katika nyadhifa zingine serikali. Huu mtindo wa kuenda ‘independent’ au kuhamia chama kingine ilhali unadaiwa kuwa unaunga mkono azma yangu ya urais, haitatusaidia kama chama,” Bw Odinga akaeleza.

VUGUVUGU LA AZIMIO

Lakini huenda mwanasiasa huyo akalegeza msimamo huo sasa ambapo amezindua vuguvugu jipya kwa jina, Azimio la Umoja. Alitangaza uzinduzi huo Ijumaa katika uwanja wa kimataifa wa michezo wa Kasarani, Nairobi alipotangaza rasmi azma yake ya kuwania urais 2022.

Duru ziliambia meza ya “Jamvi la Siasa” kwamba vuguvugu hilo litageuzwa kuwa muungano wa vyama kadhaa vya kisiasa ambao kwayo mwanasiasa anaweza kuwania kiti chochote katika uchaguzi mkuu.Kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Amos Kimunya amedhamini mswada wa marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa ili kuruhusu wanasiasa kugombea nyadhifa kwa tiketi ya miungano ya kisiasa.

Mswada utajadiliwa katika kikao maalum cha Bunge la Kitaifa ambacho kimeratibiwa kufanyika mnamo mnamo tarehe 21 mwezi huu.Lakini kwa upande wake, Dkt Ruto anawataka wafuasi wa chama cha UDA kuwapigia kura wagombeaji wa chama hicho pekee katika nafasi zote sita katika uchaguzi mkuu ujao.

“Nawaomba wafuasi wa UDA wasiwapigie kura wagombeaji wa hivi vyama vidogo vidogo kwa sababu vitatukanganya. Tunataka kuwa na wabunge wengi, maseneta wengi na magavana wengi ili sera yetu ya kuinua uchumi ya watu wadogo iweze kutekelezwa katika ngazi zote za serikali,” Dkt Ruto akasema juzi alipoongoza kampeni katika kaunti ya Kwale.

“Nia yetu ni kustawisha UDA ili kiwa chama kikubwa cha kitaifa ndiposa kiweze kuendeleza ajenda yake ya kuinua maisha ya mahasla kupitia mfumo wa kukuza uchumi kuanzia chini. Kwa hivyo, nataka ieleweke kwamba UDA haitashiriki muungano na hivyo vya vidogo vya kikabila,” Naibu Rais akakariri.

Alikuwa akirejelea vyama kama vile; The Service Party (TSP) kinachoongozwa na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, Chama cha Kazi (CCK) chake Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria na Chama cha Mashinani (CCM) kinachoongozwa na aliyekuwa Gavana wa Bomet Isaac Rutto.

Licha ya Mbw Kiunjuri, Kuria na Rutto kutangaza wazi kwamba wanaunga mkono azma ya Dkt Ruto ya kuingia Ikulu 2022, wameshikilia kuwa katu hawatavunja vyama vyao ili kuungana na UDA.

You can share this post!

JAMVI: Waasi kuhama Ford-K ni dafrau kwa Wetangula

Mudavadi, Weta wajianika kwa kususia hafla ya Raila

T L