NA MARGARET MAINA
Kujisema vibaya
UAMUZI wa kujikosoa mara kwa mara na kujizungumzia vibaya ni mojawapo ya ishara kwamba hujipendi.
Kujiweka chini na kuzingatia madhaifu au makosa yako kunadhoofisha hali ya kujiamini.
Kutafuta uthibitisho wa mara kwa mara
Kutegemea sana uthibitisho wa nje na kutafuta idhini ya mara kwa mara kutoka kwa wengine kunaonyesha ukosefu wa kujiamini na kujithamini.
Hofu ya kushindwa
Hofu ya kushindwa kufanikiwa inaweza kusababisha mtu kuepuka changamoto au fursa mpya. Hofu hii inatokana na kutokuwa na imani katika uwezo wako binafsi na mwoga wa kuhukumiwa au kukosolewa.
Kuona ugumu wa kusema ‘la’ na ‘hapana’
Mtu asiyejiamini anaweza kutanguliza mahitaji ya wengine kuliko yake mwenyewe hata pale ambapo ni wazi anaumia.
Kukataa pongezi
Ugumu wa kukubali pongezi au kuzitia doa kwa maneno ya kujidharau ni ishara ya kutojiamini. Hii inatokana na imani kwamba mtu hastahili kusifiwa au kutunukwa sifa.
Kujiona ‘mkamilifu kabisa’
Kujiona kwamba wewe ni mkamilifu na mtu anayestahili kila kitu kizuri kunaweza kuonyesha una mapungufu. Hitaji la kudumu la kutokuwa na dosari linatokana na woga wa kuhukumiwa au kutofikia viwango visivyowezekana.
Kupendeza watu
Kutaka kuwafurahisha wengine na kutanguliza mahitaji yao huku ukipuuza yako ya kibinafsi kunaweza kuwa ishara ya kutojiamini. Hofu ya kukataliwa au kuachwa husukuma baadhi ya watu kuwa na tabia hii.
Kujilinganisha na wengine
Kujilinganisha mara kwa mara na wengine na kuhisi kana kwamba umesalia nyuma kimaendeleo na tabia ya kuwa na wivu ni ishara tosha ya kutojistahi. Tabia hii inatokana na imani kwamba wengine ni bora kukuliko au wanastahili zaidi.
Kuepuka changamoto au hatari
Kutojiamini kunaweza kusababisha mtu aepuke changamoto au akwepe jambo kwa kukosa ujasiri. Kuepuka huku kunatokana na hofu ya kushindwa na imani kwamba mtu hana uwezo wa kuhimili vikwazo.
Kujihujumu
Kujihusisha na tabia za kujiharibu au kudhoofisha mafanikio ya mtu mwenyewe kunaweza kuwa dhihirisho la kutojithamini.
Kuomba msamaha kupita kiasi
Kuomba msamaha mara kwa mara kwa mambo madogomadogo au kuchukua jukumu kupita kiasi ili kusudi ujipendekeze kwa wengine kunaweza kuwa ishara ya kutojistahi. Tabia hii inatokana na hofu ya kutokea kwa migogoro au kutowapendeza wengine.
Kokosa ari ya uthubutu
Ugumu wa kujieleza kwa kutaja mahitaji, matamanio, au maoni yako ni ishara ya kutojiamini. Tabia hii inatokana na hofu ya kukataliwa, mgongano, au kutochukuliwa kwa uzito.
Kujitenga
Kujitenga na hali za kijamii au kuepuka maingiliano ya kijamii kunaweza kuwa ishara ya kutojiamini. Kujitenga huku kunaweza kutokana na woga wa hukumu au imani kwamba mtu havutii au kupendwa.
Kujipuuza
Kupuuza kujitunza, kama vile kupuuza afya ya kimwili, matunzo mengine ya binafsi, au ustawi wa kihisia, kunaweza kuonyesha kutojistahi. Tabia hii inatokana na kutojithamini na kutojiona mtu mwenye umuhimu.