NA WANDERI KAMAU
JE, Rais William Ruto aliwahadaa Wakenya kuhusu ahadi alizotoa kwao wakati wa mahojiano ya pamoja aliyofanyiwa Alhamisi na vyombo vya habari?
Kumekuwa na hisia tofauti.
Kwa viongozi katika muungano tawala wa Kenya Kwanza, Rais Ruto aliwaeleza Wakenya ukweli kuhusu mafanikio na hatua alizofikia katika siku 100 za kwanza za utawala wake.
Kwa mrengo wa Azimio, Rais Ruto ni mdanganyifu; kiongozi anayeendelea kujitetea hata baada ya kuwasaliti na kuwahadaa Wakenya. Ni kauli mbili kinzani.
Ni misimamo mikali iliyodhihirishwa na wabunge Nelson Koech (Belgut) na Seneta Godfrey Osotsi (Vihiga).
Kwa Bw Osotsi, mahojiano ya Dkt Ruto huwa njia ya kutetea ‘uongo’ wake, kauli inayopingwa vikali na Bw Koech.
Godfrey Osotsi-Seneta, Vihiga
“Mahojiano ya Rais Ruto huwa yanafanywa kurejelea hatua na mafanikio aliyopata kama Rais. Hata hivyo, mahojiano aliyofanyiwa Alhamisi yalimsawiri kama kiongozi ambaye bado yuko kwenye kampeni. Ikiwa mahojiano hayo yalifanywa kumpa nafasi ya kuwaelezea Wakenya mafanikio aliyopata baada ya siku 100, basi alianguka kwa asilimia 100. Alikuwa ametoa msururu wa ahadi ambazo hajatimiza hata kidogo.”
Nelson Koech-Mbunge, Belgut
“Rais Ruto amedhihirisha wazi ni kiongozi mkweli na anayetimiza ahadi zake. Kwa muda wa siku 100 za kwanza za uongozi wake, Wakenya wameanza kuhisi mabadiliko, ijapokuwa bado anahitaji muda zaidi. Tuna imani atatimiza yale yote aliyoahidi kabla ya muhula wa kwanza kukamilika.”