• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Jumuiya ya kaunti za Pwani: Raia wanataka kuona vitendo, huduma

Jumuiya ya kaunti za Pwani: Raia wanataka kuona vitendo, huduma

NA PHILIP MUYANGA

MATAMSHI ya magavana wa kaunti sita za ukanda wa Pwani ya kuweka kando tofauti zao za kisiasa ili kuangazia maendeleo hususan kupitia muungano wa Jumuiya ya Kaunti za Pwani yamepokelewa kwa hisia tofauti tofauti na wakazi wa ukanda huo.

Hii ni kwa kuwa tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Kaunti za Pwani kumekuwa na kutoelewana baina ya magavana wa kaunti sita za ukanda wa Pwani kwa sababu za kisiasa ambazo kwa muda mrefu zilisababishwa na uwepo wao katika vyama tofauti vya kisiasa.

Licha ya kusema kuwa watafanya kazi pamoja na kuhakikisha uchumi wa Pwani utasonga mbele swali wengi wanajiuliza ni iwapo uamuzi wa magavana hao wa kuacha tofauti zao za kisiasa utadumu ikizingatiwa wako katika mirengo tofauti ya kisiasa. Magavana Abdulswamad Shariff Nassir, Gideon Mung’aro na Dhadho Godhana wa Mombasa, Kilifi na Tana River walichaguliwa kupitia chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kilichoko katika muungano wa Azimio.

Kwa upande mwingine, Bi Fatuma Achani (Kwale) alichaguliwa kupitia tikiti ya United Democratic Alliance (UDA), Bw Issah Timamy (Lamu) katika tikiti ya chama cha Amani National Congress (ANC) na Bw Andrew Mwadime (Taita Taveta) alichaguliwa kama mgombea huru.

Maendeleo

Baadhi ya wachanganuzi wa siasa wanasema kuwa muungano wa Jumuiya ya Kaunti za Pwani ni chombo mwafaka cha kuimarisha maendeleo katika ukanda wa Pwani lakini iwapo kutakuwa na uungwaji mkono wa kisiasa au umoja wa magavana wote.

Wachanganuzi hao wanasema kuwa kufaulu kwa Jumuiya ya Pwani kunategemea magavana hao sita kuwacha tofauti zao za kisiasa na misukumo ya vyama vyao katika utenda kazi wa kaunti na kuamua kuendeleza ukanda wa Pwani.

Kwa mfano, Disemba 2021 katika mkutano mmoja wa kujadili masuala ya kuinua uchumi kupitia ufadhili wa muungano wa bara Uropa gavana Dhadho Godhana ndiye aliyekuwa katika kikao hicho kati ya magavana sita wa ukanda wa Pwani.

Kutokuwepo kwa viongozi hao kulikashifiwa vikali na baadhi ya waliohudhuria kikao hicho kilochowajumuisha baadhi ya wataalamu wa sekta mbali mbali za masuala yahusikanayo na uchumi.

Wachanganuzi wa siasa pia wanasema kuwa ni vizuri kwa viongozi wa Jumuiya ya Kaunti za Pwani kuhakikisha pia wameelezea wakazi wa Pwani masuala yahusikanayo na jumuiya kwani baadhi yao hawayajui. Hili wanasema ni muhimu kwani mipango yote ya miradi ya maendeleo isipokubaliwa na wananchi basi huwa haiwezi kuendelea.

Akinukuliwa na Taifa Leo siku ya Alhamisi wiki hii katika kongomano lililowaleta viongozi wa kaunti zote sita mjini Mombasa, Bw Godhana alisema kuwa kulikuwa na tofauti kadhaa ambazo alizitaja kuwa za kawaida na kwamba Jumuiya ya Kaunti za Pwani haikuwa imevunjika.

“Viongozi waliotutangulia walipata changamoto katika Jumiya ya Kaunti za Pwani lakini viongozi na wataalamu wamekuwa wakitafuta njia za kukwepa mambo yanayoleta mgawanyiko huo,” alisema Bw Godhana.

Naye gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro alisema kuwa viongozi wa sasa wako tayari kurejesha uhusiano mzuri kwa manufaa ya ukanda wa Pwani.

Bw Mung’aro aliongeza kusema kuwa wataendesha vyema Jumuiya ya Kaunti za Pwani ili kuweza kufikia malengo ya wakaazi wa ukanda mzima wa Pwani.

Kwa upande wake gavana wa Taita Taveta Bw Andrew Mwadime alisisitiza kuwepo kwa umoja wa viongozi wa Pwani ili kuendeleza uchumi.

Licha ya magavana hao kusisitiza kuwa wataungana na kufanya kazi pamoja ili kuimarisha Jumuiya ya Kaunti za Pwani, wachanganuzi wa siasa wanasema kuwa ni lazima watekeleze masuala ya maendeleo katika kaunti zao kwanza.

Prof Halimu Shauri ambaye ni mchanganuzi wa siasa alisema kuwa iwapo kaunti hizo zimeshindwa kujiendeleza basi itakuwa vigumu kuendeleza jumuiya nzima.

Aliongeza kusema kuwa magavana hao wanafaa waonyeshe wananchi wataweza kuendeleza kivipi kaunti zao ndiposa waweze kuangazia majukumu ya Jumuiya ya Kaunti za Pwani.

“Kuwepo kwa pamoja kwa Jumuiya ya Kaunti za Pwani si jambo mbaya, ni suala zuri sana lakini hekima huanzia nyumbani,” alisema Prof Shauri ambaye pia ni mhadhiri katika chuo kikuu cha Pwani kilichoko kaunti ya Kilifi.

Kuwekeza katika miradi

Prof Shauri alisema kuwa ni vyema iwapo kwa pamoja wataweza kuungana na kuwekeza miradi ya pamoja kwa mfano kuanzisha hospitali maalum ya kutibu aina moja ya maradhi kama vile saratani itakayohudumia kaunti zote sita.

Mshauri wa masuala ya siasa Bw Bozo Jenje alisema kuwa kuungana kwa magavana hao ni jambo nzuri kwa kuwa umoja wao ni nguvu kwa ukanda wa Pwani.

“Kwa wakati huu, magavana hao wakija pamoja na kuungana wanaweza kuvutia mashirika mengine ya misaada kwa uzito wa masuala yao,” alisema Bw Jenje.

Aliongeza kusema kuwa magavana hao wakijitenga na kila mmoja kuwa kivyake, basi watakosa nguvu za kukabiliana na masuala yanayokumba ukanda mzima wa Pwani.

Mchanganuzi wa siasa za ukanda wa Pwani Bw Abdulrahman Abdalla alisema kuwa kwa muungano wa Jumuiya ya Kaunti ya Pwani kuimarika ni lazima wananchi wenyewe wahusishwe.

Bw Abdalla alisema kuwa ingawa ni vizuri kufanya mikutano ya jumuiya katika mikahawa ya kifahari,ni vizuri viongozi hao na usimamizi wa muungano huo kufika mashinani mara kwa mara kuwaelezea wananchi yanayojiri.

“Kwa kusema ukweli,Jumuiya ya Kaunti za Pwani ni suala nzuri,lakini lazima waelekee mashinani wakutane na wananchi.Ni watu wangapi kule mshinani kama kaunti za Taita Taveta,Tana River na Lamu wanafahamu kuhusu jumuiya?” aliuza Bw Abdalla ambaye alikuwa mwanasiasa miaka ya zamani.

You can share this post!

MIKIMBIO YA SIASA: Kwa mkakati huu, Sakaja yuko vizuri!

WALIOBOBEA: ‘Sirkal’ alipokataa wadhifa serikalini

T L