• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
JUNGU KUU: Hofu Ruto anadhibiti bunge na mahakama

JUNGU KUU: Hofu Ruto anadhibiti bunge na mahakama

NA CHARLES WASONGA

HUKU Rais William Ruto akimaliza mwezi mmoja tangu kuapishwa kwake kuwa rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya, maswali yameibuliwa kuhusu nia yake katika kudhibiti Bunge na Idara ya Mahakama.

Kulingana na Katiba nguzo hizi mbili zinafaa kuhakiki utendakazi wa Serikali Kuu zikizuia uwezekano wa kuchipuza kwa utawala mbaya na ufisadi. Asasi ya Bunge na Idara ya Mahakama zinapasa kufanya kazi kwa njia huru bila kuonekana kushawishiwa au kuingiliwa na mtu au asasi yote, ikiwemo Afisi yake Rais.

Lakini tangu kuapishwa kwake mnamo Septemba 13, Rais Ruto ameonekana kama kiongozi wa taifa ambaye anataka kuwa na usemi katika yale yote yanayofanyika katika bunge na mahakamani.

Hii imeibua maswali kuhusu kwa kufanya hivyo kwa manufaa ya wananchi au kwa ajili ya kulinda na kuendelea masilahi yake na wandani wake wa kisiasa.Kwa mfano, hata kabla ya kuapishwa, Dkt Ruto alianzisha kampeni ya kudhoofisha mrengo wa upinzani, Azimio la Umoja-One Kenya, bungeni, kwa kushawishi jumla ya wabunge 14 wa mrengo huo kuhamia Kenya Kwanza.

Wabunge hao ni wale waliochaguliwa kwa tiketi cha vyama vya United Democratic Movement (UDM), Pamoja African Alliance (PAA), Maendeleo Chap Chap (MCC)) na Movement for Development and Growth (MDG), ambavyo, kisheria, vingali ndani ya Azimio.

Pili, kuporomoka kwa kesi za ufisadi dhidi ya wandani wa Rais Ruto, baadhi yao wakiwa ni wale ambao amewapendekeza kushikilia nyadhifa za uwaziri na makatibu wa wizara.

Wao ni aliyekuwa Seneta wa Meru Mithika Linturi, aliyekuwa mbunge wa Malindi Aisha Jumwa, aliyekuwa Gavana wa Moses Lenolkul, aliyekuwa Afisa Mkuu wa kampuni ya kusambaza umeme nchini (KPLC) Kenneth Tarus, miongoni mwa wengine.

Hali hii imeibua maswali kutoka kwa wadau, kama vile Chama cha Mawakili Nchini (LSK) ambacho kimeanza kuhoji uhuru wa idara ya mahakama na Afisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (ODDP) Noordin Haji.

“Tumeingiwa na hofu kwamba huenda kesi hizo zinaporomoka kwa sababu mahakama au afisi ya Bw Haji zimeingiliwa. Kuna uwezekano mkubwa kwamba serikali kuu inashawishi kuondolewa kwa kesi hizi, ikizingatiwa kuwa wale ambao kesi zao zimetupiliwa wamependekezwa kushikilia nyadhifa kuu uwaziri na makatibu wa wizara,” anadai Rais wa LSK Eric Theuri.

Naye mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Tom Mboya anasema kuwa hatua Rais Ruto kudhibiti bungeni na asasi za kufanikisha utekelezaji wa haki kama vile ODPP na Idara ya Mahakama ni hatari kwani itachangia kunawiri wa ufisadi, hulka ya kudharua sheria na utawala mbaya.

“Kimsingi, Bunge na Idara ya Mahakama zinapasa kufanyakazi kwa njia huru ili ziweze kuhakiki utendakazi wa serikali kuu. Ikiwa bunge litageuzwa kama jukwa la kusifia na kupitisha chochote kutoka kwa serikali na mahakama zinatupilia mbali kesi kiholela, Kenya itakuwa ikielekea katika mkondo wa utawala wa kidikteta,” anaeleza msomi huyo.

Dkt Mboya anaeleza kuwa ishara ya kwanza kwamba Ikulu imefaulu kuteka bunge ilionekana wakati wa uchaguzi waa Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula mnamo Septemba 8.

Seneta huyo wa zamani wa Bungoma alizoa jumla ya kura 214 na kumshinda aliyekuwa Spika wa Bunge hilo Kenneth Otiato Marende aliyepata kura 118.

Hii ni licha ya kwamba kisheria, mrengo wa Azimio uliomdhamini Marende ulishinda jumla ya viti 171 vya ubunge katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 huku muungano wa Kenya Kwanza (KKA) ikiwa na wabunge 165.

Hii ina maana kuwa kando na wabunge 14 ambao Rais Ruto alifaulu kuwashawishi kuhamia mrengo wa Kenya Kwanza, kuna wabunge kadha wa Azimio waliompigia Bw Wetang’ula kura.

Kimsingi, Rais Ruto “alinyakua” wabunge wa Azimio kwa lengo la kuhakikisha kuwa anadhibiti Bunge la Kitaifa, lenye ushawishi mkubwa katika uhakiki wa utendakazi wa serikali.Bunge hilo pia ndilo lenye usemi katika utayarishaji wa bajeti ya kitaifa na upigaji msasa wa watu ambao Rais Ruto amependekeza kushikilia nyadhifa za Waziri, Makatibu wa Wizara na mabalozi wa Kenya katika mataifa ya kigeni.

Kesho, Jumatatu, Oktoba 17, kamati ya bunge la kitaifa kuhusu uteuzi, chini ya uongozi wa Bw Wetang’ula inaanza kupiga msasa watu 22 waliopendekezwa na Rais Ruto kuhudumu katika baraza lake la mawaziri.

Licha ya upinzani kutoka kwa wabunge wa Azimio wanaodai kuwa baadhi ya watu waliopendekezwa kushikilia nyadhifa hizo hawajaafiki hitaji maadili na uongozi bora, kuna uwezekano mkubwa kwa wote hao watapitishwa kwa vyeo hivyo.

Lakini Naibu Rais Rigathi Gachagua ameshikilia kuwa kesi dhidi ya Bw Linturi, Bi Jumwa ziliporomoka kwa sababu ‘zilichochewa kisiasa’.

“Mahakama haiwezi kuendelea na kesi ambazo hazina ushahidi, kesi zilizoletwa kufanikisha malengo fulani ya kisiasa,” akasema.

Bw Gachagua pia ameitetea serikali dhidi ya madai kuwa imeteka bunge na Idara ya mahakama akisema nia yake ni kufanya kazi na nguzo hizi ‘kwa manufaa ya Wakenya’.

“Kwa mfano, tunataka kushirikiana na bunge kupitisha miswada itakayotuwezesha kama serikali kutimiza ahadi tulizowapa Wakenya, haswa kupunguza gharama ya maisha. Hatuna nia ya kuhujumu uhuru wa bunge,” akaongeza.

  • Tags

You can share this post!

Teuzi: Mwanachama wa PAA ashtaki IEBC

Ruto ateua mpelelezi mwenye tajriba kurithi Kinoti DCI

T L