• Nairobi
  • Last Updated April 15th, 2024 2:58 PM
JUNGU KUU: Kibarua cha Raila na Uhuru kuokoa Azimio

JUNGU KUU: Kibarua cha Raila na Uhuru kuokoa Azimio

NA BENSON MATHEKA

VIONGOZI wa Azimio la Umoja One Kenya, Uhuru Kenyatta na Raila Odinga, wanakabiliwa na kibarua kigumu kuudumisha muungano huo baada ya kubwagwa kwenye uchaguzi mkuu uliopita huku vyama tanzu vikihamia mrengo wa Kenya Kwanza wa Rais mteule Dkt William Ruto.

Tayari, vyama tanzu kadhaa vya muungano huo vimeuhama na kujiunga na Kenya Kwanza hatua ambayo wadadisi wa siasa wanasema ni dalili zake kusambaratika.

Chama cha United Democratic Movement (UDM) kinachoongozwa na Seneta wa Mandera Ali Roba kiliutema muungano huo punde tu baada ya Dkt Ruto kutangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa Agosti 9 hatua ambayo imenyima Kenya Kwanza wabunge saba.

Chama cha UDM pia kiliashiria kuwa kitabanduka kutoka Azimio na wachanganuzi wa siasa wanasema kwamba huo unaweza kuwa mwanzo wa vyama tanzu kuhama muungano huo. Wabunge wa vyama tanzu pia wanahamia Kenya Kwanza alivyofanya William Kamket wa Kanu.

“Kibarua ambacho kinakabili Uhuru Kenyatta na Raila Odinga ni kudumisha muungano wa Azimio la Umoja One Kenya baada ya kushindwa katika kura ya urais. Kuna maswali mengi kuhusu jinsi muungano huo uliundwa na kuna ushawishi wa Dkt Ruto ambaye anawinda vyama tanzu vya Azimio ili mrengo wake uwe na idadi kubwa ya wabunge katika mabunge yote mawili,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Geff Kamwanah.

Mchanganuzi huyu anahisi kwamba huenda Uhuru Kenyatta ambaye ni mwenyekiti wa Baraza Kuu la Muungano huo akakosa ushawishi baada ya kuondoka mamlakani Jumanne ijayo.

“Baada ya kuondoka mamlakani, Uhuru Kenyatta hatakuwa na ushawishi mkubwa katika kuunganisha vyama tanzu katika muungano huo ikizingatiwa chama chake cha Jubilee kina wabunge 27 pekee. Chama cha ODM kinaweza kulalamika kuwa kikiwa na wabunge 90 kinafaa kuamua mambo katika muungano huo na kuufanya uvunjike,” asema.

Katika mkutano wa kwanza na wabunge wa muungano huo Jumatano wiki hii, Bw Kenyatta alihimiza wabunge kutonunuliwa na upande wa Kenya Kwanza ili Azimio iwe na nguvu za kukosoa serikali.

“Msikubali kuwekwa mfukoni. Ukinunuliwa utajuta. Ni wakati wa kuonyesha iwapo utanunuliwa Kwa Sh5, au utasimama kutetea maslahi ya Wakenya 50 milioni,” Kenyatta aliambia wabunge hao.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa George Kimani, kuna hofu kwamba muungano huo hautadumu kwa muda mrefu.

Hali halisi ya Azimio itabainika baada ya miezi sita ijayo muda wa kuuhama utapokuwa umeiva kulingana na mkataba wake uliowasilishwa kwa msajili wa vyama.

“Ukweli ni kwamba ni muungano dhaifu na kushindwa kwake uchaguzini kumefanya vyama tanzu hasa vile vidogo kuwazia kujipanga upya,” akasema Kimani.

Anasema kuna uwezekano wa kila chama tanzu cha muungano huo kuwa kivyake kabla ya mwisho wa mwaka huu.

“Azimio ilikuwa chombo cha kutumia kwenye uchaguzi mkuu uliopita na ungedumu kwa muda kama ungeshinda. Kumbuka katika historia ya Kenya hakuna muungano unaodumu baada ya uchaguzi ukikosa kushinda. Hata ukishinda, huwa ni kwa muhula mmoja tu kisha unasambaratika,” asema Kimani na kutoa mfano wa muungano wa Narc uliosambaratika baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa 2002, Cord, NASA na Jubilee iliyosambaratika baada ya chaguzi za 2013 na 2017 mtawalia.

  • Tags

You can share this post!

Ruto pagumu kuwatosheleza ‘wageni wapya’

UJAUZITO NA UZAZI: Tatizo la mtoto kuvuja mkojo

T L