NA CHARLES WASONGA
KUPITISHWA kwa Mswada wa Marekebisho ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), 2022 katika Seneti Alhamisi sasa kunaashiria kuwa Kenya Kwanza itakuwa na usemi zaidi katika uteuzi wa mwenyekiti na makamishna wapya wa tume hiyo.
Hii ni kwa sababu mswada huo unaopendekeza kubadilishwa kwa muunda wa jopo litakaloendesha mchakato wa uteuzi wa makamishna hao utashirikisha mwakilishi wa Tume ya Utumishi wa Umma (PSC), inayodhibitiwa na serikali.
Aidha, mswada huo, unaosubiri kutiwa saini na Rais William Ruto, unapendekeza kushirikishwa kwa mwakilishi wa Kamati ya Shirikishi ya Vyama vya Kisiasa (PPLC).
Sheria ya zamani kuhusu uteuzi wa jopo la kuteua makamishna ya IEBC haikutoa nafasi kwa PSC na PPLC kuteua wawakilishi miongoni mwa wanachama wake saba.
Asasi zilizoteua wanachama katika jopo hilo zilikuwa Tume ya Huduma za Bunge (wawakilishi wanne), Baraza la Madhehebu ya Kenya (IRCK) na Chama cha Mawakili Nchini (LSK).
Mswada huo umetenga nafasi mbili kwa PSC na PPLC, na kuipokonya Tume ya Huduma za Bunge nafasi mbili.
Hii ina maana kuwa tume hiyo, inayoshughulikia masilahi ya wabunge na wafanyakazi wa asasi hiyo, sasa imesalia na nafasi mbili pekee katika jopo litakaloundwa.
Nafasi moja itaendea mrengo wa KKA huku mwingine ukipewa Azimio.
Mswada huo ambao ulidhaminiwa na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wa mnamo Oktoba, 2022, ndio wa kwanza kudhaminiwa na mrengo wa Rais Ruto tangu alipoingia mamlakani Septemba 13, 2022.
Mswada huo ulipitishwa katika Bunge la Kitaifa Desemba 18, baada ya wabunge wa KKA kuwalemea wenzao wa Azimio kiidadi.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema haja kubwa ya muungano wa Kenya Kwanza (KKA), unaongozwa na Rais Ruto, ni kushawishi uteuzi wa mwenyekiti na makamishna wapya wa IEBC kwa manufaa yao katika uchaguzi mkuu wa 2027.
“Dkt Ruto na wandani sasa wamefaulu kuhakikisha kuwa wanachama wengi katika jopo litakaloundwa kuendesha shughuli ya uteuzi wa wanachama wapya wa IEBC ni watu ambao wataimba ‘wimbo’ wao. Hii hatimaye itafanikisha azma yao ya kuhakikisha kuwa mwenyekiti na makamishna watakaoteuliwa ni wale watakaowapendelea katika uchaguzi mkuu wa 2027,” anasema Martin Andati.
“Ukweli ni kwamba baada ya kutangazwa mshindi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022, Dkt Ruto alianza kuandaa mipango ya kushinda katika uchaguzi utakaofuata. Hatua ya kwanza katika mipango hiyo ilikuwa ni kudhibiti Bunge la Kitaifa na Seneti ili kuwezesha miswada, hoja na maamuzi yanayoendeleza masilahi yake kufaulu, na amefaulu,” anaongeza.
Hii ndio maana wakati wa mjadala kuhusu mswada huo, mnamo Alhamisi, maseneta wa muungano tawala, KKA, waliuunga mkono kwa dhati, huku wenzao wa Azimio wakaupinga vikali.
Wakiongozwa na kiongozi wa wengi seneta Aaron Cheruiyot na mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Masuala ya Sheria Hillary Sigei, maseneta wa KKA walisisitiza kuwa mswada huo upitishwe jinsi ulivyotoka Bunge la Kitaifa, bila kufanyiwa marekebisho.
Waliangusha marekebisho yote yaliyopendekezwa na mrengo wa Azimio wakati wa kikao hicho maalum kilichoitisha na Spika Amason Kingi.
Kwa mfano, Seneta Mteule wa ODM Catherine Mumma alipendekeza kuwa mswada huo ufanyiwe marekebisho ili kuondoa sehemu inayoipa tume ya utumishi wa umma nafasi ya kuteua mtu mmoja kuwa mwanachama wa jopo la kuteua makamishna wa IEBC.
Kulingana na pendekezo hilo, lililoungwa mkono na kiongozi wa wachache Seneta Stewart Madzayo na Seneta wa Siaya Oburu Oginga, vyama vyama vya kisiasa ndivyo vinapasa kuwa na usemi katika uteuzi huo.
“Tunafaa kufuata mfano wa uteuzi wanachama wa tume hii uliofanywa 1997 ambapo vyama vya kisiasa ndivyo vilihusishwa pakubwa. Matokeo ya mbinu hiyo yalionekana katika uchaguzi mkuu wa 2002 ambayo ni ya kipekee nchini iliyoendeshwa kwa njia huru na haki, na matokeo ya urais kukubalika na wote,” akasema Bi Mumma, ambaye pia ndiye mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi katika ODM.
Maseneta wengine wa Azimio Edwin Sifuna (Nairobi) na Godffrey Osotsi (Vihiga) walisisitiza kuwa tume ya PSC ni asasi ya Serikali Kuu na hivyo Rais Ruto ndiye ataamua yule atakayeteuliwa kuwakilisha asasi hilo katika jopo hilo la uteuzi.
“PSC ni chombo ambacho Rais hutumia kuteua watu katika utumishi wa umma. Sasa iweje kwamba tunampa Rais, ambaye atashiriki katika uchaguzi mkuu ujao, nafasi ya kuteua mtu katika jopo la kuteua makamishna wapya wa IEBC?” akauliza Bw Osotsi.
Jopo litakaloteuliwa sasa litaongoza mchakato wa uteuzi wa makamishna watano wa IEBC pamoja na mwenyekiti.
Hii ni baada ya muhula wa mwenyekiti wa zamani Wafula Chebukati na waliokuwa makamishna Profesa Abdi Guliye na Boya Molu kutamatika Januari 17, 2023.
Wengine kama; Juliana Cherera, Justus Nyang’aya na Francis Wanderi walijiuzulu Desemba mwaka jana baada ya kukabiliwa na kutuhuma za kukiuka sheria kwa kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais yaliyotangazwa na Bw Chebukati mnamo Agosti 15, 2022 katika Bomas of Kenya.
Naye Kamishna Irene Masit amesimamishwa kazi na amekuwa akichunguzwa na jopokazi liliteuliwa na Rais, kwa makosa yayo hayo yanayowakabili Cherera na wenzake.
Jopokazi hili, linaloongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa Aggrey Muchelule, halijawasilisha ripoti yake rasmi kwa Rais Ruto.
Subscribe our newsletter to stay updated