• Nairobi
  • Last Updated April 15th, 2024 2:58 PM
JUNGU KUU: Rigathi, Mudavadi wazozania wizara

JUNGU KUU: Rigathi, Mudavadi wazozania wizara

NA WANDERI KAMAU

HUENDA tofauti za kisiasa zilizoibuka kati ya Rais William Ruto na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i zikachipuka upya katika utawala wake, baada ya taharuki kuanza kushuhudiwa baina ya vigogo kadhaa.

Tofauti hizo zinahofiwa kuibuka kati ya Naibu Rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa ANC, Bw Musalia Mudavadi.

Hata kabla ya kulitangaza baraza lake la mawaziri, imeibuka kuwa Bw Mudavadi amepangiwa kutumia afisi ya Harambee Annex kuendesha shughuli zake, kama Msimamizi Mkuu wa Mawaziri.

Afisi hiyo ilikuwa ikitumiwa na Dkt Ruto alipokuwa akihudumu kama Naibu Rais.

Kulingana na mkataba uliotiwa saini baina ya vyama vya UDA na ANC katika mrengo wa Kenya Kwanza, Rais Ruto aliahidi kumteua Bw Mudavadi kama Kinara Mkuu wa Mawaziri, ikiwa mrengo huo ungeibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 9.

Ni nafasi inayolingana na ile aliyokuwa akishikilia Dkt Matiang’i, baada ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kutofautiana kisiasa na baadaye kukosana na Rais Ruto.

Kando na hayo, imeibuka kuwa Bw Gachagua anashinikiza kutengewa wizara muhimu kama Fedha na Usalama wa Ndani, “kutokana na idadi kubwa ya kura ukanda wa Mlima Kenya ulimpa Dkt Ruto.”

Hata hivyo, duru zimeeleza kuwa Bw Mudavadi pia anashinikiza kutengewa moja ya wizara hizo.

Kutokana na mwelekeo huo, wadadisi wanasema kuwa huenda tofauti zilizoibuka kati ya Dkt Ruto na Dkt Matiang’i zikachipuka upya, hali ambayo huenda ikazua msukosuko wa kisiasa hata kabla ya serikali yake kuanza kutekeleza ahadi ilizotoa kwa Wakenya.

“Huu huenda ukawa mwanzo mbaya sana kwa Dkt Ruto, ikiwa atashindwa kudhibiti tofauti baina ya vigogo hao wawili, kwani hali iyo hiyo ndiyo ilizua tofauti za kisiasa kati yake na Bw Kenyatta,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kwenye uchaguzi huo, Dkt Ruto alizoa jumla ya kura 3.5 milioni katika kaunti zote kumi katika ukanda wa Mlima Kenya.

Kaunti hizo zinajumuisha Nyeri, Nakuru, Meru, Embu, Tharaka Nithi, Nyandarua, Laikipia, Murang’a, Kiambu na Kirinyaga.

Duru zimeleza kuwa Bw Gachagua pia anashinikiza kutengewa Wizara ya Kilimo, ili kumwezesha “kutimiza ahadi” alizotoa kwa wenyeji wa Mlima Kenya.

Wadadisi wanasema kuwa ikiwa Rais Ruto hatachukua hatua za haraka kudhibiti tofauti ambazo zimeanza kujitokeza baina ya vigogo hao wawili, huenda akakumbwa na mawimbi makali ya kisiasa hata kuliko Bw Kenyatta.

Baada ya Bw Kenyatta kubuni handisheki na kiongozi wa Azimio-One Kenya, Bw Raila Odinga mnamo 2018, uhasama kati yake na Rais Ruto uliongezeka vikali, baada ya kumkweza Dkt Matiang’i kuwa kama Kinara wa mawaziri wengine.

Wadadisi hata hivyo wanasema kuwa kwa kuonekana kuwakweza vigogo kama Mudavadi na Moses Wetang’ula kuwa Kinara wa Mawaziri na Spika wa Bunge la Kitaifa mtawalia, lengo la Dkt Ruto ni kuongeza uungwaji mkono wake kisiasa katika eneo la Magharibi.

“Rais Ruto ashaanza kubuni mikakati ya ‘kampeni’ za mwaka 2027. Kwa sasa anayalenga maeneo ambayo hakupata uungwaji mkono mwaka huu ili kuyajumuisha kwenye serikali yake. Ni mkakati unaoweza kuzua ukosoaji mkubwa kwa maeneo na vigogo ambao watahisi ‘kutorejeshewa mkono’ vizuri,” asema Bw Korir Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Hata hivyo, washirika wa karibu wa Dkt Ruto wanataja hayo kama “vumi na propaganda zinazoenezwa na washindani wake.”

“Kuna watu wengi ambao hawamtakii mafanikio kwenye serikali yake. Hata hivyo, watashtuka kutokana na mikakati atakayoweka kutimiza ahadi alizotoa,” asema mbunge Ndindi Nyoro (Kiharu).

  • Tags

You can share this post!

Raia kupoteza Azimio isipong’ata bungeni

Kenya Kwanza ni piga ua kwa Azimio

T L