• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 7:22 PM
JUNGU KUU: Ruto atakavyopanga ‘wazee’ Uhuru, Raila

JUNGU KUU: Ruto atakavyopanga ‘wazee’ Uhuru, Raila

NA BENSON MATHEKA

RAIS William Ruto anapanga kuhakikisha kuwa mtangulizi wake Uhuru Kenyatta na mshirika wake katika Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga wanatekeleza majukumu yao katika upinzani bila makali ya kutoa jasho serikali yake.

Tangu hotuba yake ya kwanza katika bunge la taifa akiwa rais, Dkt Ruto amerudia mara tatu katika hafla tofauti kwamba hana nia ya kuwahangaisha viongozi “wazee” waliotekeleza jukumu muhimu katika nchi hii akisisitiza kuwa atawapanga kwa njia ya heshima.

Kwenye hotuba hiyo alimkejeli Uhuru akisema ni rais aliyegeuka kuwa kiongozi wa upinzani, huku naibu wake( Ruto) akishinda urais.

Aidha, alimtaja Bw Odinga kama kiongozi wa upinzani aliyebadilika kuwa mgombea urais wa serikali katika uchaguzi mkuu wa Agosti akirejelea ukuruba wake na Uhuru.

Jumapili iliyopita akiwa Homa Bay, Rais Ruto alisema kwamba jukumu lake kubwa ni kuhudumia raia wote na akasisitiza kwamba atawapanga viongozi waliomtangulia kwa njia ya heshima.

“Nawaomba tushirikiane kujenga nchi yetu. Hawa wazee wetu waliotekeleza jukumu lao kwa nchi, aliyekuwa waziri mkuu na Rais mstaafu wetu, niachieni hao nitawapanga, na nitawapanga kwa njia ya heshima,” Rais aliambia wakazi wa Homa Bay.

Rais Ruto aliashiria kwamba ana nia ya kumsukuma Bw Odinga kustaafu siasa japo alisema anafikiri anaweza kusaida nchi katika mipango tofauti ya kimataifa.

“Anaweza kufanya kazi nasi kama mzee wa heshima, hatuwezi kumchagulia anachotaka kufanya,” Rais Ruto alisema.

Mnamo Jumanne akiwa Nyeri kuhudhuria mazishi ya kaka ya naibu wake Rigathi Gachagua, Rais Ruto alikariri kwamba hana nia ya kumkosea heshima Bw Uhuru.

Kulingana na wadadisi wa siasa, mpango wa Rais Ruto kwa Bw Odinga na Bw Uhuru ni kuhakikisha hawana makali ya kutoa jasho serikali yake huku akitambua kwamba wawili hao ni washirika katika muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja One Kenya.

Bw Odinga ni kiongozi wa muungano huo naye Uhuru ni Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Azimio japo hajakuwa akihudhuria mikutano ya mikakati tangu alipomkabidhi Ruto hatamu za uongozi.

“Rais Ruto anataka kuwapanga kwa kutumia mbinu mbili; moja ni kuhakikisha ametoa pumzi upinzani na amefaulu kufanya hivyo kwa kuhakikisha ana idadi kubwa ya wabunge na maseneta. Ameafikia hili kwa kunyakua vyama tangu vya Azimio na amefaulu. Hii itamfanya Bw Odinga kutokuwa na wanajeshi wa kumwezesha kutoja jasho serikali kwa maamnuzi yake,” asema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.

Anasema kwamba pia huenda Dkt Ruto alimaanisha kwamba hatavumilia visa vyovyote atakavyohisi vinahujumu serikali yake kutoka kwa viongozi hao.

“Anajua uwezo na ushawishi wao na kwamba wako na wafuasi wasiopungua milioni saba waliopigia Azimio kura na wanaweza kupatia utawala wake wakati mgumu,” aliongeza Bw Kamwanah.

Wachanganuzi wanasema kwamba mbinu nyingine ya kuwapanga ni kuwatenganisha viongozi hao jambo ambalo alianza kufanya hata kabla ya kuapishwa kwa kumpa Uhuru kazi ya kuwa balozi wa amani katika nchi jirani.

Katika hotuba yake ya kwanza baada ya kuapishwa kuwa rais, Dkt Ruto alisema kwamba Uhuru alikuwa amekubali kuwa mpatanishi katika nchi zinazokumbwa na misukosuko eneo la Afrika Mashariki.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: CBC: Machogu avae viatu vya Magoha

MIKIMBIO YA SIASA: Faida na zigo la KK kama wengi bungeni

T L