• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 8:55 PM
JUNGU KUU: Ubabe wa Machogu na Matiang’i u wazi Gusii

JUNGU KUU: Ubabe wa Machogu na Matiang’i u wazi Gusii

NA WANDERI KAMAU

IMEBAINIKA kuwa moja ya kiini cha ‘masaibu’ ya kisiasa yanayomwandama aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, ni ubabe wa kisiasa unaoendelea baina yake na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu katika eneo la Kisii.

Duru zinaeleza kuwa Dkt Matiang’i anaonekana kughadhabishwa na umaarufu na ushawishi mpya wa kisiasa ambao Bw Machogu ameanza kupata katika eneo hilo, ikizingatiwa kuwa tangu alipoteuliwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kuwa waziri mnamo 2013, ndiye amekuwa kigogo na msemaji mkuu wa kisiasa wa jamii ya Abagusii.

Katika utawala wa Bw Kenyatta, Dkt Matiang’i alikuwa miongoni mwa mawaziri wenye ushawishi mkubwa, kiasi kuwa alionekana kama ‘Kaimu Naibu Rais’ baada ya Rais William Ruto (wakati huo akiwa Naibu Rais) kukosana na Bw Kenyatta.

Ni hatua iliyomfanya kukosana vikali na Rais Ruto na washirika wake, kwani walimlaumu kwa “kunyakua” majukumu ya Dkt Ruto.

Kulingana na wadadisi, moja ya hatua kuu Rais Ruto kumteua Bw Machogu kama Waziri wa Elimu ni kumkuza kama kigogo na msemaji wa kisiasa wa jamii ya Abagusii, “kuchukua nafasi ya Dkt Matiang’i”.

“Ni wazi kuwa Dkt Matiang’i ndiye amekuwa msemaji rasmi wa kisiasa wa jamii ya Abagusii, hasa kutokana na ushawishi wake mkubwa aliokuwa nao katika serikali ya Bw Kenyatta. Hili pia linatokana na kutawazwa kwake kuchukua nafasi hiyo na Baraza la Wazee wa Abagusii, wakiongozwa na Mzee James Matundura mnamo 2021,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kulingana na diwani mmoja kutoka eneo hilo ambaye hakutaka kutajwa, “sarakasi” hizo zilianza baada ya Dkt Matiang’i kuhisi kuwa ushawishi wa Bw Machogu ulikuwa ukiongezeka katika eneo hilo, hivyo kutishia nafasi yake.

Kwenye mahojiano na ‘Jamvi la Siasa’, diwani huyo alisema kuwa Dkt Matiang’i, ambaye pia ni miongoni mwa viongozi wa chama cha United Progressive Party (UPA), alihisi kuwa kuongezeka kwa umaarufu wa kisiasa wa Bw Machogu kulikuwa kukififisha usemi na nyota yake ya kisiasa katika kauti ya Nyamira na eneo la Kisii kwa ujumla.

“Hilo ndilo mwanzo wa matukio yote tunayoshuhudia kwa sasa,” akasema diwani huyo.

Hata hivyo, washirika wa karibu wa Dkt Matiang’i wanataja madai hayo kama uongo, wakisisitiza kuwa umaarufu wa waziri huyo wa zamani haujafifia hata kidogo miongoni mwa jamii ya Abagusii “kutokana na utendakazi wake wa hali ya juu alipohudumu kama waziri”.

Kwenye mahojiano, Seneta wa Kisii Richard Onyonka anasisitiza kuwa serikali ya Rais William Ruto “inaonekana kutiwa hofu na umaarufu ambao Dkt Matiang’i ameendelea kudumisha licha ya kuondoka serikalini”.

“Unapoona serikali ikifanya kila juhudi kumwelekeza Dkt Matiang’i licha ya kutokuwa serikalini, hilo linaonyesha jinsi inavyohofishwa na umaarufu wake. Ni wakati ianze juhudi mpya za kisiasa kujijenga miongoni mwa raia badala ya kuanza kuwatishia viongozi,” akasema Bw Onyonka akimtetea vikali Dkt Matiang’i.

Wadadisi wanasema kuwa kibarua sasa kitakuwa jinsi Bw Machogu, ambaye ni mshirika wa kisiasa wa muda mrefu wa Rais Ruto, ataendesha mikakati yake mipya kumzima kabisa Dkt Matiang’i katika eneo hilo.

Wanaeleza kuwa Rais Ruto amemteua Bw Machogu kama “mtu wake wa mkono” katika eneo hilo kwani kando na kuhudumu kama afisa wa utawala nchini kwa muda mrefu, ana uzoefu wa kisiasa kwani amehudumu kama mbunge wa eneo la Nyaribari Masaba na baadaye akawania ugavana katika Kauti ya Kisii mwaka 2022 ijapokuwa hakufaulu.

  • Tags

You can share this post!

MALEZI KIDIJITALI: Hili hapa tishio jipya kwa watoto...

JAMVI LA SIASA: Hii ndiyo hatari ya Rais Ruto kuandama Uhuru

T L