• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 6:07 PM
JUNGU KUU: Vita vya Uhuru na Ruto kufaidi Raila

JUNGU KUU: Vita vya Uhuru na Ruto kufaidi Raila

NA CHARLES WASONGA

VITA vipya vilivyochipuza kati ya Rais William Ruto na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta huenda vikamfaidi kiongozi wa upinzani Raila Odinga katika vita vyake dhidi ya utawala wa Kenya Kwanza.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa sasa wanasema nipe nikupe hiyo kati ya Rais Ruto na Bw Kenyatta itampa Bw Odinga nguvu zaidi ya kuiponda serikali, kuiyumbisha na hata kuikosesha nafasi ya kutekeleza ahadi nyingi ilizotoa kwa Wakenya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

“Ikiwa joto hili la uhasama ambalo limechipuza tena kati ya Rais Ruto na Rais mstaafu halitapoeshwa kwa njia ya upatanisho, Raila ambaye ameanzisha msururu wa mikutano ya hadhara kote nchini ya kuipaka tope serikali hii changa atampa motisha mpya,” mchanganuzi wa msuala ya kisiasa Javas Bigambo amenukuliwa akisema.

Anaongeza: “Raila atatumia nafasi hii kueneza ujumbe kwa wananchi kwamba serikali hii haina ajenda zozote za maendeleo zenye manufaa kwao ila inaongozwa na nia ya kulipiza kisasi dhidi ya wale aliowasawiri kama mahasidi wake, haswa, Rais Kenyattaa ambaye alimpokeza mamlaka kwa amani.”

Akiongea mjini Mombasa Jumatatu alipofungua mkutano wa wabunge Rais Ruto alionekana kumshambulia Bw Kenyatta akidai ndiye amekuwa akifadhili mikutano ya Raila ya kupinga serikali ilia apate nafasi ya kukwepa kulipa ushuru.

“Hata kama wanadhamini maandamano, ningetaka kuhakikishia kuwa sharti walipe ushuru. Sharti tuwe na nchi ambapo kila mtu analipa ushuru,” akasema, akiongeza: “Sirejelei ushuru mpya bali zile ambazo ni halali na zimeidhinishwa na Bunge.

Rais alifananisha mienendo ya watu mashuhuri nchini, ambao hakuwataja, wa kukwepa ushuru na hali inayosawiriwa katika riwaya ya “Shamba la Wanyama” ambapo wanyama baadhi ya wanyama ni bora kuliko wengine.

“Hatuko katika Shamba la Wanyama ambapo watu wengine ni bora kuliko wenzao. Sharti sote tulipe ushuru. Haijalishi idara ya mikutano ambayo utadhamini kuyumbisha ajenda yetu. Sharti ulipe ushuru,” akaongeza Dkt Ruto aliyeonekana mwenye ghadhabu.

Rais alionekana kurejelea Bw Kenyatta, japo hakumtaja jina moja kwa moja. Lakini Rais huru mstaafu amejibu madai hayo akayataja kama “kilele za watu ambao wameshindwa kufanya kazi waliyopewa.”

Rais Ruto alitoa kauli yake baada ya mwanablogu na mwanaharakati wa Kenya Kwanza Denis Itumbe kudai kuwa mikutano ya hadhara ya Bw Odinga inadhamini na “mtu fulani ambaye ambaye hataki watu walipe ushuru baada ya yeye na familia yake kukinga na sheria fulani kongwe kulipa ushuru kwa mali wanayomiliki.”

Bw Itumbe aliweka mitandaoni sehemu ya Sheria ya zamani kuhusu Ardhi, “Estate Duty Act, Cap 483” iliyokinga familia za Rais wa kwanza Jomo Kenyatta na Rais wa Pili Daniel Arap Moi dhidi ya kulipa ushuru kwa ardhi kubwa zinazomiliki.

Lakini baada ya Rais Ruto kutoa cheche kuhusu suala hilo la ushuru, maseneta watatu waliochaguliwa kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA), John Methu (Nyandarua), James Murango (Kirinyaga na mwenzao wa Nyeri Wahome Wamatinga walimshambulia, moja kwa moja, Bw Kenyatta wakidai anatumia pesa alizokwepa kulipa kama ushuru kuhujumu serikali ya Kenya Kwanza.

“Sisi kama viongozi tunaowawakilisha raia, hatuwezi kunyama huku mtu kama Rais mstaafu Uhuru Kenyatta akwepa ushuru na kutumia pesa hizo kufadhili maandamano na mikutano inayolenga kuvuruga amani nchini. Hivi karibuni tutadhamini mswada wa kubatilisha sheria hii inayokinga familia za Kenyatta na Moi dhidi ya kulipa ushuru,” akasema Bw Methu.

Bila kutoa ithibati yoyote, maseneta hao waliochaguliwa kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoogozwa na Rais Ruto mwenyewe walidai kuwa wafadhili wa Azimio walifanya mikutano katika maeneo ya Maasai Mara, Mlima Kenya na Mombasa “kupanga njama zao za kuyumbisha serikali ya Kenya Kwanza.”

Kwa upande mwingine, Seneta wa Nandi Samson Cherargei ameanzisha kampeni ya kumshinikiza Rais Ruto kumvua Bw Kenyatta wadhifa wa kuwa mpatanishi mkuu katika mchakato wa kuleta amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

“Rais Ruto anafaa kumpiga kalamu Bw Kenyatta kama balozi wa amani wa Kenya nchini DRC. Hawawezi kuendelea kutekeleza wajibu wa kuleta amani katika nchi hiyo ihali anafadhili fujo humo nchini,” Bw Cherargei akasema kupitia Twitter.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kenyatta Profesa Eric Masinde Aseka anasema kuwa kama Rais mstaafu, Bw Kenyatta anafaa kupewa heshima na mrithi wake.

“Hizi vita ambavyo Uhuru anapigwa wakati huu bila shaka huenda ukaendeleza moto wa kisiasa ambao umeanzishwa na Bw Odinga kupitia mikutano yake ya kuipaka tope serikali ya Kenya Kwanza. Bilas haka Rais Ruto hataongoza kwa amani ikiwa ataonekana kama kiongozi anayeongozwa na nia na lengo la kulipiza kisiasa,” akaongeza mchanganuzi huyo wa masuala ya kisiasa.

  • Tags

You can share this post!

Ruto anavyomfufua Uhuru kisiasa

HUKU USWAHILINI: Kuna jibaba huku limeshindwa kumdekeza mke...

T L