Na FARIDA OKACHI
Mwigizaji Catherine Kamau almaarufu Kate Actress anataka kampuni ya habari ya TUKO EXTRA kumuomba msamaha kwa kupeperusha habari anazosema zimemharibia sifa.
Mwigizaji huyo ambaye siku chache zilizopita alishtua mashabiki wake kwa kutangaza kutengana na mume wake, Phil Karanja, anasema Tuko ilipeperusha habari ambazo zilimharibia sifa na kuonekana kuwa na utovu wa maadili.
Kupitia kwa mawakili wake, Ano Advocates, Kate anadai kwamba TUKO EXTRA ilipeperusha kipindi kinachofahamika “Chat with Lily” Septemba 23, 2023 kupitia mtandao wa YouTube ambapo anamshutumu Hussein Yusuf, mfanyakazi wao, kwa kutumia maneno ambayo yalimwacha Bi Kamau kuonekana kama msanii ambaye hana maadili huku akiwahusisha Lily Aisha na Victor Otengo na kuzidi kumdhalilisha.
Kwenye kipindi hicho ambacho anasema kimetazamwa na zaidi ya watu 48,000, mwigizaji huyu analalamika kwamba maneno yaliyotumika yalikuwa ya uongo na ya kuchukiza ambayo yalimtatiza kisaikolojia.
Wakili wake, Waithera Ngugi anasema mteja wake aliathirka kutokana na chapisho hilo analosema lilimharibia jina na biashara na kumpekelea kupata hasara.
Wakili huyo sasa anataka TUKO kusitisha kupeperusha na kuepuka lugha ya kuudhi mteja wake kwa mitandao yote ya kijamii. Anataka pia waombe msamaha kwa umma, kutoa taarifa rasmi ya msamaha na kuhakikisha unamfikia Hussein Yusuf pamoja na kufuta video hiyo kwenye mitandao yao ya kijamii.
Iwapo masharti hayo hayatatekelezwa katika kipindi cha siku 14 kuanzia siku ya ilani hii, kampuni hiyo ya mawakili itachukua hatua ya kuelekea mahakamani na kushtaki TUKO.