• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 6:55 PM
KAULI YA WALLAH: Ni busara kufikiri badala ya kupapia kusema au kujibu

KAULI YA WALLAH: Ni busara kufikiri badala ya kupapia kusema au kujibu

NA WALLAH BIN WALLAH

KUFIKIRI ni kazi. Ubongo wako hauwezi kukupa majibu sahihi ya maswali unayoulizwa bila ya ubongo kufanya kazi ya kufikiri vizuri! Kuelewa swali vyema ndiko kupata jibu au majibu sahihi.

Kusema au kujibu kwa papara tu kunasababisha kutoa majibu batili yasiyoeleweka ama yasiyowiana na swali lililoulizwa au maswali yaliyoulizwa!

Wanafunzi wengi shuleni hula mwande, hubunda au hufeli siyo kwa kuwa ni wajinga! La hasha! Kushindwa kwao hutokana na kujibu haraka haraka kabla ya kuchambua na kutambua kiini cha swali.

Ili kuelewa kiini cha swali lazima mtu afanye kazi ya kufikiria dhamira ya swali kabla hajalijibu. Majibu sahihi ni kuelewa maswali kwa usahihi! Hakuna mwanafunzi wa kushindwa kuyajibu vizuri maswali anayoyaelewa barabara!

Chunguza uone!!Usijibu haraka haraka kabla ya kufikiria na kuelewa unachotaka kujibu na unavyotaka kujibu! Katika maswali kuna kufikiri na katika kufikiri kuna kutaka kujua madhumuni ya muulizaji maswali ndipo utoe jibu au majibu! Maswali hufikirisha!

Fikiri kabla hujatamka au kujibu!Maswali yanapoingia kichwani mwa binadamu, yanaupa ubongo msukumo wa kufanya udadisi na kutafiti zaidi ili afikie kina kamili cha kupata majibu yanayofaa! Kadri mtu anavyokumbana na maswali mazito ya kujiuliza au anayoulizwa ndivyo anavyojifunza mambo ambayo hakuwa ameyaelewa!

Maswali hujulisha, huerevusha na kutanabahisha!Ninashangaa watu wengine wanapotoa majibu haraka haraka tu punde wanapoulizwa maswali! Hawajui kwamba majibu ya papara ni hatari? Tena yanapotosha?

Watu wenye hasira, ukali na majivuno rohoni huwa wepesi wa kutoa majibu mengi upesi upesi kuonesha ubabe wao waulizwapo maswali! Mbona?Leo tufahamishane kwamba mtu anapokuwa na majibu mengi ya haraka haraka kichwani, anadhani na kujiona kuwa anajua kila kitu!

Kumbe ajuaye kila kitu ni Mola tu! Kujibu haraka haraka bila kukuna kichwa ni kutangaza udhaifu na kudhihirisha tu kwamba mtu hajui anavyojibu kwa mujibu wa majibu mujarabu yaliyotarajiwa kuyatosheleza maswali yaliyoulizwa!

Huku kujibu kwa papara tumeshuhudia sana mara nyingi katika matukio mbalimbali ya mahojiano na mihadhara hapa na pale! Ni hatari! Tufikiri kabla ya kujibu!

Ndugu wapenzi, mtu akiulizwa swali au maswali yoyote, ni bora zaidi kufikiri na kulielewa swali ndipo ajue atakavyojibu! Kujibu swali kwa kulielewa, kwa heshima na adabu ni utu! Majibu mazuri huonesha busara aliyo nayo mtu!

Chonde chonde! Fikiri kabla hujasema na ufikiri zaidi kabla hujajibu haraka haraka! Kufikiri ni kazi!!!

You can share this post!

HADITHI: Pengo asononekea hadhi ya chini wanayopewa walimu...

Natembeya kuwania ugavana Trans Nzoia