• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
KFCB yatumia wasanii kupigana na wizi wa mifugo

KFCB yatumia wasanii kupigana na wizi wa mifugo

NA TITUS OMINDE

BODI ya Uainishaji wa Filamu Nchini (KFCB) imegeukia muziki na sanaa kusaidia kukabiliana na kero la wizi wa mifugo North Rift.   

KFCB aidha imeanza kushirikiana na wanamuziki chipukizi na wasanii wa kizazi kipya kutumia talanta zao na burudani katika vita dhidi ya wizi wa mifugo na ujangili, changamoto ambazo zimeonekana kulemea vyombo vya usalama.

Tayari bodi hiyo imepiga hatua kushirikisha wasanii mbalimbali kutoka katika maeneo tajika kwa wizi wa mifugo na itikadi kali, ikilenga kuteka mchango wao kuangazia maovu.

Meneja wa Kanda ya North Rift, Bonventure Kioko alisema shirika lake linashirikiana na wizara ya mambo ya ndani na vyombo vingine vya serikali kuhusisha vijana kutoka maeneo yaliyoathirika na ujambazi na wizi wa ng’ombe kwa kuwawezesha kupitia vipaji vyao kuwa mabalozi katika mapambano dhidi ya uhalifu lengwa.
“Kwa sasa serikali inafanya kila iwezalo kutokomeza wizi wa ng’ombe na ujambazi wa aina hiyo North-Rift. Kama KFCB tunashirikiana na serikali kwa kuwawezesha wasanii wachanga kutoka kanda hii ili kutumia vipaji vyao kupambana na ujambazi kwa kuongezea juhudi za serikali,” alisema afisa huyo.
Akizungumza mjini Eldoret siku mnamo Jumapili, Mei 21, 2023 wakati wa mafunzo kwa wasanii kutoka West Pokot, Baringo, Nandi Uasin-Gishu, Bungoma na Trans Nzoia, Bw Kioko aliwataka vijana walio na talanta kutoka eneo hilo kutafuta usaidizi kutoka kwa KFCB ili kuwajengea uwezo katika kukuza talanta zao ili kupambana na maovu katika jamii.
Bw Kioko alikariri uwezo wa talanta katika vita dhidi ya ujambazi na itikadi kali.
“Kama bodi tunashirikiana na vijana kuchunguza mbinu za kutumia ujuzi wao wa kisanii katika vita dhidi ya visa vya uhalifu nchini,” alisema Bw Kioko.

Alitoa changamoto kwa vijana kuepuka misimamo mikali, akiwahimiza kutafuta uwezeshaji wa kifedha kupitia talanta zao kwa kusaka usaidizi kutoka kwa KFCB.

Aidha, alisema kuwa vipaji vina uwezo mkubwa kuwezesha vijana kiuchumi badala ya kung’ang’ania tamaduni zinazorudisha maendeleo nyuma hasa wizi wa ng’ombe miongoni mwa shughuli nyingine zilizopitwa na wakati.

“Tunawaomba vijana wajitokeze kutafuta usaidizi kutoka kwa KFCB ili kusaidia talanta zao. Vipaji vinaleta pesa nyingi ikilinganishwa na tamaduni zilizoharamishwa na serikali,” alisema Bw Kioko.

  • Tags

You can share this post!

Gaspo Women kususia mechi dhidi ya Vihiga Queens

Akiri kuua mwanawe kutokana na msongo wa mawazo

T L