• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
KIGODA CHA PWANI: Joho anavyomkweza Mboko kwa kususia hafla za Azimio Pwani

KIGODA CHA PWANI: Joho anavyomkweza Mboko kwa kususia hafla za Azimio Pwani

NA PHILIP MUYANGA

JE kutokuwepo kwa aliyekuwa gavana wa Mombasa Hassan Ali Joho katika mikutano ya siasa ya muungano wa Azimio ya hivi sasa katika ukanda wa Pwani hususan wiki jana katika uwanja wa Caltex Likoni kuliimarisha ushawishi wa kisiasa mbunge wa eneo hilo Bi Mishi Mboko?

Hili ndilo swali wakazi wengi wa Mombasa pamoja na wachanganuzi wa sisasa wanajiuliza kwa kuwa Bi Mboko alionekana kuwa mstari wa mbele zaidi ya viongozi wengine hususan wale wa Mombasa katika mkutano huo.

Ingawa alikuwa mbuge mwenyeji wakati wa mkutano huo,ujasiri aliokuwa nao ulidhihirisha ya kuwa ushawishi wake ulikuwa unaimarika katika siasa za Mombasa.

Mbunge huyo wa Likoni aliyekuwa amevalia sare ya kijani kibichi cha mwituni (jungle green) alionekana mara kwa mara akishauriana na kiongozi wa muungano wa Azimio Bw Raila Odinga wakati wa mkutano huo katika uwanja wa Caltex.

Bi Mboko ambaye pia alikuwa anaongoza ratiba za sherehe hizo zilizongoozwa na Bw Odinga,Bw Kalonzo Musyoka na Bi Martha Karua hakusita kuwachangamsha wananchi kwa hotuba na misemo yake iliyowasisimua waliokuwa wamehudhuria.

Hata hivyo, licha ya kuonekana kuwa na ushawishi mkuu,Bi Mboko alitambua uwepo wa gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir katika hotuba yake na pia alimtaja mara mbili tatu katika mkutano huo.

“Hapa Mombasa tukiwa chini ya gavana Abdulswamad Shariff Nassir tujipange na mabasi twende Nairobi (kwa maandamano),” alisema Bi Mboko.

Wa kwanza kuunga

Bi Mboko alikuwa mmoja wa viongozi wa kwanza wa chama cha ODM mjini Mombasa kuunga mkono Bw Nassir katika harakati zake za uwaniaji wa kiti cha ugavana.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, kutokuwepo kwa Bw Joho katika mikutano ya siasa ya hivi majuzi kumeonekana kutoa nafasi nzuri kwa Bi Mboko kujinoa makali katika uongozi wa siasa za chama cha Orange Democratic Movement (ODM) na Azimio katika kaunti ya Mombasa na ukanda wa Pwani.

Wachanganuzi hao wanasema kuwa kando na Bw Joho,Bi Mboko mbinu za kisiasa za kuwachangamsha wananchi katika mikutano na kwamba anaweza kuwa na ushawishi mkubwa kwa chama hicho kama kiongozi wa kutoka ukanda wa Pwani.

Si wakati wa mkutano huo pekee wa kisiasa Bi mboko ameonyesha ujasiri wake,takriban wiki tatu zilizopita,katika hafla ya rais William Ruto ya kuzindua ujenzi wa kiwanda cha gesi katika eneo la Dongo Kundu, alionyesha ujasiri wake wa kisiasa na kuomba nafasi za kazi kupewa wakaazi wa Likoni kwanza.

Bi Mboko alisema kuwa wakazi wa Likoni walikuwa na heshima na kwamba ilikuwa vyema wapate kufaidika na miradi ya serikali hususan katika eneo spesheli la uchumi maarufu kama special economic zone,lililoko eneo la Dongo Kundu.

Si mwoga

Mchanganuzi wa masuala ya siasa pamoja na ya jamii Prof Hassan Mwakimako anasema kuwa Bi Mboko si mwoga na ana mbinu ya kusisimua wananchi jambo ambalo halijafanyika Mombasa kwa muda mrefu kuona mwanamke mwanasiasa kusimama jukwaani na kuchapa siasa.

“Anaoneysha aina tofauti ya siasa ya mwanamke wa kipwani,siasa hiyo haijaonekana hapo awali,” alisema Prof Mwakimako.

Aliongeza kusema kuwa Bi Mboko anaziba pengo la Bw Joho kutokuwa katika mikutano ya siasa kwa mbinu yake ya kuwashawishi watu kisiasa na kusisimua umati wa watu ikitiliwa maani kuwa baadhi ya viongozi wengine wa Pwani wamekuwa wamenyamaza na anajaza pengo hilo.

Prof Mwakimako alisema kuwa siasa za gavana wa Mombasa Bw Abdulswamad Nassir ni za kiupole na hawezani na aina ya mazingira usisimuaji watu ikilinganishwa na Bi Mboko.

Hata hivyo, mchanganuzi wa siasa na masuala ya jamii Bw Ayub Mwangi alisema kuwa bado siasa za Mombasa zinatawaliwa na wanaume.

Bw Mwangi alisema kuwa ana uhakika ya kuwa kutakuwa na mwanasiasa mwanaume ambaye atajitokeza na kuwa na ushawishi mkuu kumliko Bi Mboko.

“Bi Mboko ni mwanamke jasiri kisiasa lakini kati ya wanawake, kwa wanaume wanasiasa sidhani,” alisema Bw Mwangi.

Aliongeza kusema kuwa Bw Nassir kwa upande wake hapendi siasa za malumbano na kwamba yuko na ustaarabu mwingi wa kisiasa kuwa kiongozi mwenye ushawishi mkubwa Mombasa.

“Bw Nassir atakuwa sawa akiendeleza ajenda ya maendeleo kwa kuwa atataka kuchaguliwa tena kama gavana mwaka wa 2027,” alisema Bw Mwangi.

Mwanasiasa mmoja wa zamani aliyetaka jina lake libanwe alisema kuwa Bi Mboko yuko na ubora unaohitajika kisiasa ambao unaweza kumpeleka mbali.

“Bi Mboko amejionyesha kuwa mwanasiasa ambaye ni jasiri hususan huku Mombasa,na pia tangu ajiunge na siasa kwa sasa amepata uzoefu wa kutosha kuhusiana na siasa za Mombasa na Pwani kwa ujumla,” alisema mwanasiasa huyo.

Mwanasiasa huyo mkongwe alisema kuwa kustaafu kwa Bw Joho kama gavana kunaweza kumpatia Bi Mboko nafasi ya kuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa kwani ana mbinu za kusisimua wananchi katika mikutano ya siasa ambayo wanasiasa wengi wa Mombasa hawana.

  • Tags

You can share this post!

JUNGU KUU: Mikakati ya Ruto kumfifisha Raila

PENZI LA KIJANJA: Ikiwa mnapendana, msisahau busu kwani...

T L