• Nairobi
  • Last Updated September 26th, 2023 10:25 PM
KIGODA CHA PWANI: Kaunti za Pwani zaweza kujikimu bila kutegemea kodi ya bandarini?

KIGODA CHA PWANI: Kaunti za Pwani zaweza kujikimu bila kutegemea kodi ya bandarini?

KUSIMAMISHWA kwa juhudi za gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir za kutaka kuongeza mapato ya kifedha ya kaunti kupitia kodi ya mizigo itokayo bandarini kumezua mjadala mkubwa iwapo serikali za kaunti sita za Pwani zina uwezo wa kujikimu bila kutegemea serikali ya kitaifa.

Baadhi ya serikali za kaunti za ukanda wa Pwani zinakabiliwa na madeni takriban Sh11 bilioni kwa pamoja ambayo yaliachwa na serikali za awali kabla ya uchaguzi wa Agosti mwaka jana ndiposa juhudi za kaunti ya Mombasa kufaidika na bandari zilikuwa zinasubiriwa na wengi.

Kila mwaka serikali ya kitaifa hujipatia takriban Sh15 bilioni zitokanazo na kodi inayotozwa mizigo na huduma zingine katika bandari ya Mombasa na inatarajiwa ya kuwa kipato hicho kitaongezeka na uwepo wa bandari ya Lamu iliyoanza kazi hivi majuzi.

Barua ya Mwanasheria Mkuu Justin Muturi ya kuzuia serikali ya kaunti ya Mombasa kutoza kodi mizigo itokayo bandarini imekashifiwa na baadhi ya viongozi wa Pwani huku wachanganuzi wa siasa wakisema kuwa uamuzi huo wa Bw Muturi ulikuwa wa haraka.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kuwa Bw Muturi alifaa kujadiliana na viongozi wa Pwani na kupata suluhu kwani bandari ni raslimali ya ukanda wa Pwani ambayo inafaa kuwafaidisha wananchi.

Hata hivyo, wachanganuzi wengine wa siasa wanasema kuwa ni sharti kaunti za ukanda wa Pwani kutafuta njia m’badala za kujipatia pesa na pia kuzima njia zote za ufisadi unaohusisha baadhi ya wafanyikazi.

Ukiukaji katiba

Kulingana na barua ya Bw Muturi kwa gavana wa Mombasa, hatua ya kaunti ya kutaka kutoza kodi ni ukiukaji wa Katiba na kwamba serikali ya kaunti haina uwezo kisheria kutoza kodi kwa mizigo yoyote inayoingia nchini.

Suala la kutoza mizigo kodi kutoka bandari ya Mombasa lilikuwa tayari limepitishwa na wawakilishi wadi katika bunge la kaunti ya Mombasa kupitia Mswaada wa Fedha za Kaunti wa 2022/2023 na kwa sasa itabidi wakune vichwa kutafuta njia m’badala kaunti hiyo itakavyoweza kujipatia pesa.

Seneta wa kaunti ya Mombasa Bw Mohamed Faki alisema kuwa kaunti za Mombasa na Lamu zina haki na pia zinastahili kupata pesa zinazopatikana kutoka bandari zilizoko katika kaunti hizo.

Alitoa mfano wa kaunti ya Narok inayofaidi kwa mbuga ya wanyama ya Maasai Mara kwani kipato kitokacho huko kinaenda moja kwa moja kwa serikali hiyo.

“Serikali ya kitaifa haiwezi kuwa inaweka sheria tofauti tofauti kuhusiana na kaunti ya Mombasa kujipatia kipato kutoka bandari ya Mombasa, ni lazima tupate mapato,” alisema Bw Faki.

Rasilimali

Seneta maalum Bi Shakila Abdalla ambaye pia ni mkaazi wa Lamu alisema kuwa bandari ndio raslimali ya wakazi wa Pwani na ni sharti kiwango fulani cha fedha zitokazo huko zibakie kwa kaunti.

“Tunafaaa tumiliki bandari zetu,pia tunataka bandari ya Lamu iwe na bodi ya usimazi wa Lamu,” alisema Bi Abdalla.

Wakili Stephen Odiagga anasema kuwa matarajio ya wakaazi wa kaunti ya Mombasa na Pwani kwa jumla ni kuwa watanufaika na kitega uchumi chao ambacho ni bandari na pia kampuni zingine zilizoko humo.

Bw Odiagga ambaye pia ni mchanganuzi wa masuala ya jamii alisema kuwa wakaazi wa kaunti ya Mombasa hawawezi kukosolewa kwa kutaka kupata kipato kutoka kwa bandari kwani kaunti hiyo imebeba takriban wakaazi wa kaunti zote sita za Pwani.

“Maoni yangu ni kwamba Mwanasheria Mkuu amekatisha mjadala huu kwa haraka sana,haya ni mambo ambayo yanafaa majadiliano na watu wote,” alisema Bw Odiagga.

Bw Odiagga alisema kuwa hata kama majadiliano ya kaunti ya Mombasa ya kutoza kodi mizigo inayoingia nchni hayafai, mjadala wa suala hilo ni muhimu kwani utozaji wa kodi ni suala la kisiasa.

“Mwanasheria Mkuu anaweza kuwa alikuwa na nia nzuri, lakini vile alitoa maoni na kukatiza mjadala huo mara moja haikuwa vizuri kwa wakaazi wa Mombasa na wananchi wa Pwani,” alisema Bw Odiagga.

Wakili huyo alisema kuwa kaunti za Pwani zinafaa kuangalia njia zingine za kutafuta kipato kwa kutumia nafasi zinazoletwa na wawekezaji kwa mfano katika eneo la biashara la Dongo Kundu ambalo linatarajiwa kuanza kufanya kazi miezi kadhaa ijayo.

Mbuga za wanyama

Aliongeza kuwa wakati umefika kwa wakazi wa Taita Taveta kuanza kujadili vile watanufaika na mbuga ya wanayama pori ya Tsavo.

“Na hatusemi kuwa tuna tamaa ya kuchukua kila kitu kutoka kwa mbuga hiyo,wakati ndovu zinaharibu mimea sisi ndio tunapata tabu,je hakuna kitu kidogo wakaazi wanafaa kupata?”aliuliza Bw Odiagga.

Wakili huyo alisema kuwa suala hilo la Tsavo linafaa kujadiliwa kama vile lile la utozaji mzigo kodi kutoka bandari na kaunti ya Mombasa.

Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir akihutubia wakazi wakati wa uzinduzi wa mradi wa “Kazi kwa Vijana” majuzi. Yaonekana kusimamishwa kwake kutoza kodi ya mizigo itakayo bandari ya Mombasa kutaumiza kaunti za pwani. PICHA|MAKTABA

Baadhi ya wachanganuzi wa siasa wanasema kuwa serikali za kaunti za ukanda wa Pwani ni lazima zitafute njia m’badala za kupata pesa na kuweza kuwavutia waekezaji.

Wanadai kuwa iwapo watategemea pesa kutoka serikali ya kitaifa au raslimali zinazotegemewa na taifa nzima basi hazitaweza kujikimu mahitaji yao na zitabakia na madeni chungu nzima kila mwaka.

Wanaongeza kuwa kaunti za ukanda wa Pwani ni sharti ziweke mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuwavutia wawekezaji ambao biashara zao zitafaidi kaunti hizo kwa kodi watakazotoa.

  • Tags

You can share this post!

MIKIMBIO YA SIASA: Juhudi za Raila kukomboa Jubilee...

UJAUZITO NA UZAZI: Tatizo la ‘colic’ kwa mtoto...

T L