• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
KIGODA CHA PWANI: Maendeleo Pwani yanahitaji umoja wa viongozi wa huko

KIGODA CHA PWANI: Maendeleo Pwani yanahitaji umoja wa viongozi wa huko

NA PHILIP MUYANGA

WAKATI wa kuchaguliwa kwa spika wa bunge la seneti, baadhi ya wabunge wa Pwani wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya walimpigia kura aliyekuwa gavana wa Kilifi Amason Kingi kutwaa kiti hicho licha ya kuwa muungano huo ulisusia zoezi hilo.

Suala hilo liliashiria mwelekeo wa umoja wa maseneta wa Pwani katika bunge hilo kumchagua ‘mmoja’ wao bila ya kuzingatia tofauti zao za kisiasa au vyama vyao.

Kwa wakazi wengi wa Pwani, matumaini yao ni kuwa jambo hilo ndio mwanzo wa safari ya umoja wa wabunge wa Pwani katika bunge la seneti na lile la kitaifa.

Wakazi hao walilifurahia kwa dhati jambo hilo wakisema kuwa umoja huo wa maseneta ndio unaohitajika kuendeleza ukanda wa Pwani katika shughuli za kitaifa katika mabunge yote mawili bila kujali vyama vyao.

Wanasema kuwa umoja wa wabunge wa Pwani umekuwa vigumu kupatikana kwa muda mrefu huku wengi wao wakiegemea vyama vyao kila wakati bila kujali mahitaji ya wapwani kwa jumla.

Wanaongeza kusema kuwa kwa sasa ni sharti wabunge wa bunge la kitaifa na lile la seneti kuungana na kuhakikisha wamewasilisha miswaada ambayo itawafaidi wananchi wa ukanda wa Pwani na pia kuhakikisha kuwa inaungwa mkono na wabunge wengine wa sehemu zingine nchini.

UCHUMI WA PWANI

Kulingana na wakazi wa ukanda wa Pwani, wanataka miswada ihusianayo na mahitaji yao kama vile utalii,uchumi wa samawati maarufu kama blue economy na uchimbaji wa madini imewasilishwa na wabunge hao katika mabunge yao.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kuwa suala la umoja wa wabunge wa Pwani ni muhimu sana hususan katika kusukuma ajenda ya maendeleo hususan yale ya uchumi wa Pwani kupitia miswaada watakayoiwasilisha.

Wanaongeza kusema kuwa ukanda wa Pwani utazidi kuendelea iwapo miswaada ihusikanayo na maendeleo ya kaunti zote sita itawasilishwa na wabunge hao na kuhakikisha imepita na kuwa sheria.

Mwanasiasa wa zamani ambaye pia ni mchanganuzi wa siasa Bw Abdulrahman Abdalla anasema kuwa wabunge wa ukanda wa Pwani wanafaa kuacha tofauti zao za kisiasa na kuwasilisha bungeni miswaada ambayo itasidia mkaazi wa Pwani.

“Inafaa kabisa wabunge wa ukanda huu wa Pwani wawache siasa za vyama, washachaguliwa tayari na kwa sasa kazi iliyobaki ni kuwafanyia kazi wakaazi,” alisema Bw Abdalla.

Bw Abdalla anasema kuwa ukanda wa Pwani uko na changamoto za kimaendeleo na umoja wa viongozi wao hususan wale walioko bunge la kitaifa na lile la seneti utasukuma serikali kuu kuweza kuharakisha maendeleo kama vile yale ya miundo misingi.

Aliongeza kusema kuwa wabunge wa Pwani wako na majukumu makubwa katika kuhakikisha kuwa hata miswaada ya kitaifa yenye manufaa ya wakaazi wa maeneo ya mwambao wa Pwani inapita na wanaipigia debe.

Bw Abdalla aliongeza kusema kuwa wabunge wa seneti wa chama cha muungano wa Azimio kutoka ukanda wa Pwani walifanya jambo nzuri sana kuunga mkono kuchaguliwa kwa Bw Kingi.

“Kwa hivyo wabunge wote wa bunge la kitaifa na lile la seneti kutoka ukanda wa Pwani wanafaa waungane na kuhakikisha sheria zitungazwo zinazowaathiri wakaazi wa Pwani kwa njia moja au nyingine wameziangalia vizuri kwa umoja licha ya tofauti zao za kisiasa,” alisema Bw Abdalla.

Bi Maimuna Mwidau ambaye pia ni mchanganuzi wa masuala ya siasa alisema kuwa wabunge wa Pwani wanaweza kuungana kwa suala ambalo liko na umuhimu mkubwa kwa maeneo watokayo.

“Mfano ni kura ya spika wa seneti,wabunge wa azimio waliweza kuonyesha ujasiri na kumpigia mwenzao kura kuwa spika wa bunge hilo,ujasiri huo unadhihirisha kwamba ikiwa kutakuwa na jambo la muhimu basi wabunge wa pwani wataweza kuungano licha ya kuwa mirengo tofauti,” alisema Bi Mwidau.

Hata hivyo Bi Mwidau alisema kuwa kama wabunge wengine nchni,ni wawakilishi wa maeneo yao kupitia vyama vyao na kila chama huwa na ajenda yake katika bunge.

“Kwa hivyo kuna wakati chama kinaamua kupiga kura kwa njia moja au nyingine kwa hivyo wabunge wa Pwani hawatakuwa na budi kufuata msimamo wa chama kwanza,bila hivyo wanaweza kuchukuliwa hatua ndani ya chama kwa kukosa kuunga chama mkono,” alisema Bi Mwidau.

Kwa upande wake,mshauri wa masuala ya siasa Bw Bozo Jenje alisema kuwa kuhusiana na masuala ya Pwani yenye utaifa, ni muhimu sana kwa wabunge hao kuungana na kuweza kuyatetea ili kusaidia katika kuimarisha hali ya kimaisha ya wakaazi wa Pwani.

MBINU MBADALA

Bw Jenje alisema kuwa suala la ardhi kutokuwa na hati miliki,mabwenyenye wenye ardhi na hawapo,ubunifu wa mbinu za ukulima wa kisasa,afya jamii na mbinu mbadala za kisosholojia na uchumui ni mojawapo ya masuala wabunge wa Pwani wanafaa kuangazia sana katika bunge la kitaifa na lile la seneti.

“Pia jambo lingine muhimu ambalo wanafaa kuzingatia ni waweke uongozi wao kwa manufaa ya wapwani na sio tu kwa ubinafsi wao na kuridhisha viongozi wa vyama vyao,” alisema Bw Jenje.

Mkazi mmoja wa kaunti ya Taita Taveta aliyejitambulisha kama Bw Mwakio alisema kuwa umoja wa wabunge wa Pwani katika bunge la kitaifa na lile la seneti utahakikisha masuala yanayowaathiri wakaazi wa ukanda wa Pwani yametatuliwa.

“Kwa mfano hapa Taita Taveta suala la wanyama kuvamia makaazi ya watu ni mojawapo ya mambo ambayo wabunge wote wa Pwani wanafaa kuliangazia bungeni,hii ndiyo njia pekee wapwani wanaweza kuhakikisha kilio chao kimesikizwa na serikali kuu,” alisema Bw Mwakio.

  • Tags

You can share this post!

MIKIMBIO YA SIASA: Faida na zigo la KK kama wengi bungeni

Muhoozi: Ruto katika njia panda

T L