• Nairobi
  • Last Updated April 15th, 2024 2:58 PM
KIGODA CHA PWANI: Ni nani atakuwa macho na masikio ya Rais Ruto Pwani?

KIGODA CHA PWANI: Ni nani atakuwa macho na masikio ya Rais Ruto Pwani?

NA PHILIP MUYANGA

HUKU rais mteule Dkt William Ruto akisubiri kutwaa mamlaka rasmi siku ya Jumanne atakapoapishwa,inasubiriwa kuonekana ni kiongozi yupi atakuwa macho na maskio yake katika ukanda wa Pwani.

Kulingana na baadhi ya wachanganuzi wa kisiasa, kiongozi huyo itabidi akubalike kwanza na wananchi na pia kuonyesha mchango wake katika ushindi wa muungano wa Kenya Kwanza wa kiti cha urais.

Majina ya Bw Salim Mvurya na Bw Amason Kingi waliokuwa magavana wa Kwale na Kilifi mtawalia yametajwa sana katika siasa za Pwani iwapo wanaweza kuchukuwa nafasi hiyo na kuwa ‘msemaji’ wa Pwani katika serikali ya Dkt Ruto.

Siku ya Alhamisi Bw Kingi alichaguliwa kama spika wa bunge la Seneti na inasubiriwa kuonekana iwapo kuchaguliwa kwake kutainua ushawishi wake wa siasa hususan zile za ukanda wa Pwani.

Bw Mvurya na Bw Kingi walikuwa mstari wa mbele kumpigia debe Dkt Ruto katika kampeni za kusaka kiti cha urais eneo la Pwani na haijabainika wazi ni nani baina yao yuko na ushawishi mkubwa wa kisiasa katika ukanda wa Pwani.

Usemi wa Joho

Baada ya rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Bw Raila Odinga kuamua kushirikiana kupitia mchakato wa ‘handisheki’, gavana wa Mombasa anayeondoka Bw Hassan Joho alionekana kuwa na usemi mkuu wa kisiasa katika eneo la Pwani.

Hata hivyo, baada ya mahakama ya upeo kuthibitisha uchaguzi wa Dkt Ruto, ndoto ya Bw Joho ya kuwa kiongozi au ‘msemaji’ wa ukanda wa Pwani huenda ikiwa imefikia kikomo.

Licha ya chama cha ODM kuwa na idadi kubwa ya wabunge na wawakilishi wadi katika mabunge ya kaunti,huenda ikawa vigumu sana kwa Bw Joho kusukuma maswala ya siasa za Pwani kwa kuwa chama chake hakipo kwa serikali.

Kulingana na Prof Halimu Shauri, Bw Mvurya na Bw Kingi hawajaonyesha kuwa mawakala wakuu wa siasa ambao wanaweza kuongoza Pwani.

Prof Shauri alisema kuwa majadiliano ya uongozi wa Pwani kwa wawili hao basi ni kwa faida yao ya kibinafsi na sio kwa manufaa ya ukanda mzima wa Pwani.

Aliongeza kusema kuwa kutoshinda kwa Bw Hassan Omar katika kura ya ugavana kaunti ya Mombasa pia kulitia doa uwezo wa wawili hao kuhamasisha wapiga kura na kuwa mawakala wa kisiasa wenye uwezo.

Prof Shauri ambaye ni mhadhiri katika chuo kikuu cha Pwani kilichoko Kilifi alisema kuwa isipokuwa Dkt Ruto awapatie nyadhifa kuu za kisiasa (Bw Kingi ni Spika wa Seneti sasa) basi hawatakuwa na ushawishi mkuu wa kisiasa eneo la Pwani.

Mhadhiri huyo aliongeza kusema kuwa Bw Kingi hakuweza kuhakikisha chama chake kimepata kiti cha ugavana kaunti ya Kilifi kilichochukuliwa na Bw Gideon Munga’ro wa chama cha ODM.

Prof Shauri pia alisema kuwa Bw Kingi alishindwa kumuunga mkono mgombea wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) wa kiti hicho cha ugavana Bi Aisha Jumwa na badala yake akamuunga mkono mwaniaji wa chama chake cha Pamoja African Alliance (PAA), George Kithi.

Aliongeza kusema kuwa ingawa Bw Joho amepoteza ushawishi wake wa siasa za kitaifa, bado yuko na ushawishi mkuu katika kaunti ya Mombasa.

Mhadhiri huyo wa chuo kikuu alisema kuwa Bw Joho anaweza kutembea kwa kujiamini katika kaunti ya Mombasa huku akijua kuwa ameweza kusaidia chama chake cha ODM kupata ugavana kaunti hiyo.

“Bw Joho anaweza sema kuwa aliweza kumsaidia Bw Abdulswamad Nassir kupata ugavana wa Mombasa,hii inaonyesha ya kuwa yuko na ushawishi katika kaunti ya Mombasa na anaweza kutembea katika mitaa, uliona alivyokuwa anatembea na rais hivi majuzi,”alisema Prof Shauri.

Mchanganuzi mwingine wa siasa Bi Maimuna Mwidau alisema kuwa Bw Mvurya aliweza kuhakikisha chama cha UDA kimetwaa ushindi wa kiti cha ugavana kupitia kwa Bi Fatma Achani.

Bi Mwidau alisema kuwa ushindi wa Bi Achana uliongeza idadi ya magavana wa chama hicho kwa baraza la magavana ndiposa Bw Mvurya atakuwa na ushawishi wa kisiasa.

“Bw Mvurya atakuwa na ushawishi mkubwa lakini katika kiwango cha kaunti ya Kwale peke yake,kwa upande wake Bw Kingi ni mshirika wa Kenya Kwanza lakini hakusaidia muungano huo kupata kura zaidi ya Bw Mvurya,” alisema Bi Mwidau.

Aliongeza kusema kuwa ukanda wa Pwani hauna kinara wa kisiasa ambaye anaweza kushawishi siasa za Pwani katika meza ya kitaifa.

Ngome zao

Bi Mwidau alisema kuwa ushawishi wa Bw Joho uko katika chama cha ODM ambacho hakitakuwa katika serikali ijayo.

Mchanganuzi mwingine wa siasa Bw Mndwamrombo Mwakera alisema kuwa kwa Bw Kingi na Mvurya kuwa wakala washawishi wa kisiasa katika ukanda wa Pwani au kitaifa,ni lazima waweze kuungwa mkono katika ngome zao za nyumbani ambazo wawili hao hawana kwa sasa.

Bw Mwakera alisema kuwa wawili hao wako na kibarua kikubwa kuvunja ngome ya ODM katika kaunti zao na eneo la Pwani kwa jumla.

Aliongeza kusema kuwa kulingana na nyadhifa watakazo kuwa nazo za kitaifa katika serikali kuu ndipo viongozi hao wataweza kujiweka kama mawakala wa kisiasa wa ukanda wa Pwani.

Mshauri wa maswala ya kisiasa Bw Bozo Jenje alisema kuwa Bw Kingi na Bw Muvrya wamekuwa na ushawishi wa kisiasa na kulingana na mabadiliko ya kisiasa watakuwa na ushawishi mkubwa na kuweza kuomba mgao wa keki ya kitaifa kwa niaba ya wakaazi bila wasiwasi wowote.

  • Tags

You can share this post!

Jaji Mkuu atangaza kanuni mpya kuhusu kusikilizwa kesi za...

Asukumwa jela miaka 4 kwa kuiba pombe kali

T L