• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 10:25 PM
KIGODA CHA PWANI: Uteuzi wa Omar, Shahbal katika EALA utawafufua?

KIGODA CHA PWANI: Uteuzi wa Omar, Shahbal katika EALA utawafufua?

NA MWANDISHI WETU

JE, kupendekezwa kwa aliyekuwa muwaniaji wa kiti cha ugavana wa Mombasa, Hassan Omar na mfanyabiashara Suleiman Shahbal kuwa wajumbe wa bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutawapa mwamko mpya wa kisiasa hususan katika Kaunti ya Mombasa?

Hili ni swali wengi ambalo wengi wanajiuliza baada ya wawili hao, ambao wanatoka mirengo tofauti ya kisiasa, kupendekezwa na vyama vyao kuwania nafasi tisa zilizotengewa taifa la Kenya katika bunge hilo la EALA.

Bw Omar ambaye aliwania ugavana wa Mombasa katika uchaguzi wa Agosti 9 na kushindwa na Bw Abdulswamad Sheriff Nassir, ni wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) kilichoko katika muungano wa Kenya Kwanza.

Kwa upande wake, Bw Shahbal alijiondoa katika kinyang’anyiro cha kiti hicho na kumuunga mkono Bw Nassir baada ya maafikiano na wakuu wa chama cha ODM ambacho kiko katika muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.

Kabla ya kujiondoa katika kinyang’anyiro cha ugavana, Bw Shahbal alikuwa mmoja wa mahasimu wakuu wa kisiasa wa Bw Omar.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, iwapo wawili hao watachaguliwa kwenda bunge la EALA, basi watakuwa wamepata mwamko mpya wa kisiasa.

Wachanganuzi hao pia wanahoji kuwa iwapo mmoja wao atapata nafasi ya kuwa katika bunge hilo la jumuiya ya Afrika Mashariki na mwingine kukosa, basi aliyepata kiti hicho atakuwa katika nafasi ya juu ya kisiasa kumzidi mwenzake.

Hata hivyo, baadhi ya wachanganuzi wa siasa wanasema kuwa kupendekezwa kwa wawili hao hakutakuwa na tofauti yoyote kubwa kwa manufaa yao ya kisiasa na siasa za Mombasa.

Hili, wanasema kuwa ni kwa sababu walikuwa wanataka kiti cha ugavana na wakakikosa na kwamba siasa za uchaguzi mkuu ujao huenda zikawa na masuala tofauti ya kuangazia ndiposa kupendekezwa kwao hakutakuwa na mwamko mkubwa wa kisiasa kwao.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa, Dkt Daniel Mwaringa, kupendekezwa kwa wanasiasa hao na vyama vyao ni mojawapo ya njia ya kutambua umuhimu wao katika siasa hasa iwapo watachaguliwa na bunge la kitaifa nchini kwenda EALA.

Aliongeza kuwa pia iwapo watapata nafasi hiyo, basi watakuwa na umuhimu wa kisiasa huku wakilenga uchaguzi mkuu ujao.

Dkt Mwaringa anasema kuwa iwapo Bw Omar na Bw Shahbal watakuwa katika bunge hilo, basi wakati wa siasa za 2027 utakapofika na iwapo watawania tena ugavana, wataeleza wananchi mambo waliyoweza kuyatekeleza walipopewa nafasi hiyo.

“Nafasi hiyo itakuwa imewapa jukwaa zuri la kisiasa, na pia itazua mkondo mpya wa jinsi watakavyofanya siasa zao katika uchaguzi ujao,” akasema Dkt Mwaringa.

Dkt Mwaringa ambaye ni mhadhiri wa Mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Kifundi cha Mombasa (TUM) aliongeza kuwa iwapo mmoja wao hatachaguliwa kwenda EALA, basi atakayepata kiti hicho atakuwa katika nafasi nzuri ya kujipigia debe wakati siasa za Mombasa zitakaporejea.

Mchanganuzi mwingine wa siasa, Bi Maimuna Mwidau anasema kuwa kupendekezwa kwa Bw Omar na Bw Shahbal kwa bunge hilo ni njia moja ya vyama vyao kuwatunuku kama shukrani kwa kazi walioifanya wakati wa kampeni za uchaguzi wa Agosti.

“Watakapofanikiwa kuchaguliwa EALA, basi nafasi hiyo itawapa fursa ya kupata mwamko mpya katika siasa sio nchni peke yake bali katika jumuia ya Afrika Mashariki kwa jumla,” akasema Bi Mwidau.

Anaongeza kuwa iwapo watachaguliwa katika bunge hilo, Bw Shahbal anaweza kuimarisha biashara zake ikitiliwa maanani kuwa Bw Shahbal ni mfanyabiashara tajika huku Bw Omar akiwa mtetezi wa haki za kibinadamu atakayeweza kupata ukumbi ili kuendeleza utetezi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na hoja zake.

“Kulingana na tajriba zao na uzoefu wa siasa nchni, itabidi wawe na uwezo wa kutambulika hapa nchni huku wakiendeleza kazi huko Arusha (iwapo watachaguliwa),” asema Bi Mwidau.

Bi Mwidau anaongeza kuwa iwapo wawili hao watakaa kimya kwa muda mrefu, sifa zao zitasahaulika na wakati wa siasa zijazo basi watakosa umaarufu nchini na katika siasa za Mombasa.

Hata hivyo, Bi Mwidau anasema kuwa kwa wengine kupelekwa katika bunge la Eala ni kama kutupwa msituni.

Kwa upande wake, mshauri wa masuala ya siasa, Bw Bozo Jenje anasema kuwa nyadhifa za ubunge wa EALA kwa muda mwingi huwa hazina uzito wa siasa.

Anasema kuwa wawili hao hawakuwa wa kwanza kutoka ukanda wa Pwani kupata kiti hicho na wale waliokuwa hapo awali michango yao ilikuwa sio rahisi kutambulikana mashinani kwani malengo ya EALA ni utaifa wala sio maeneo ya bunge ya humu nchini.

“Iwapo watachaguliwa kwenda kwa bunge hilo la EALA na watasimama kidete na kupigania mwinuko wa sheria za biashara kutekelezwa na vikwazo vingi vya sheria kuondolewa, basi watakuwa na manufaa katika ukanda wa Pwani na Kenya kwa jumla,” akasema Bw Jenje.

  • Tags

You can share this post!

MIKIMBIO YA SIASA: Kenya Kwanza yatishia kuzima Winnie...

WALIOBOBEA: Poghisio alivyoleta mageuzi katika sekta ya ICT...

T L