• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
KIGODA CHA PWANI: Wapigakura watarajia makuu kwa wawakilishi wao wa kike

KIGODA CHA PWANI: Wapigakura watarajia makuu kwa wawakilishi wao wa kike

NA MWANDISHI WETU

JE, wabunge wa kaunti wanaowakilisha kina mama katika ukanda wa Pwani wana mipangilio gani kwa wananchi waliowachagua miezi miwili iliyopita mbali na shughuli za bunge la kitaifa?

Hili ni swali linaloulizwa na baadhi ya wakazi wa kaunti sita za ukanda wa Pwani wanaotaka kujua wawakilishi hao sita watatimiza vipi ahadi zao walizotoa katika kampeni.

Ingawa kiti hicho wanachokikalia ni cha wanawake, faida ya maendeleo yanayotokana na uongozi wake inafaidi jamii nzima ndiposa ni muhimu kwa wabunge hao kuweka mikakati mwafaka ya kutimiza ahadi zao za maendeleo kwa wananchi.

Kwa wakazi wa ukanda wa Pwani, wabunge hao wanafaa kujitokeza na kuweka wazi mipango yao ya maendeleo kwani wakati wa kampeni uliisha na sasa ni wakati wa kuwafanyia kazi raia.

Kulingana na baadhi ya wachanganuzi wa siasa, baadhi ya wananchi hawajui umuhimu wa kiti hicho na manufaa yake kwa jamii ndiposa wabunge hao wanatakikana kujitokeza wazi na kueleza mipango ya miradi yao kwa miaka mitano ijayo.

Wanadai kuwa kutokuwa na mshawasha katika kiti hicho ni kuwa kinachukuliwa kama ‘kiti spesheli’ kilichoachiwa wanawake pekee.

Wachanganuzi hao wakisiasa wanasema kuwa si makosa ya baadhi ya wananchi kutojua umuhimu wa kiti hicho kwani hakujawa na maelezo ya kijamii kukihusu licha ya nafasi hiyo ya ubunge kuwapo tangu mwaka wa 2013.

Katika kampeni zao, baadhi yao walisema kuwa lengo lao kuu ni kuboresha hali ya kina-mama katika kaunti licha ya kiti hicho kuwa na mgao mchache sana wa kifedha kutoka kwa hazina kuu ya serikali kupitia hazina ya National Government Affirmative Action Fund (Ngaaf).

Pia walitaka mgao wa pesa kutoka hazina kuu ya kitaifa uweze kuongezwa kwa kiti hicho ili wanaowakilisha wanawake waweze kusaidia jamii ipasavyo.

Baada ya kuchaguliwa kama mwakilishi wa kinamama katika Kaunti ya Mombasa, Bi Zamzam Mohamed alisema kuwa amewapangia vijana mambo mazuri kuhusiana na masuala ya ajira na biashara.

“Kina mama pia nimewapangia biashara kemkemu, maisha yenu yalikuwa chini kwani mlikuwa mmesahaulika,” akasema Bi Mohamed punde tu baada ya kutangazwa mshindi wa kiti hicho.

Alisema pia atashughulikia suala la mtoto wa kike na kuhakikisha kuwa wasichana waliopata mimba za mapema wanapata nafasi ya kurudi shuleni na kuendelea na masomo yao.

Katika Kaunti ya Lamu, Bi Monica Muthoni Marubu aliahidi kutekeleza miradi mbalimbali iinayohusisha wanawake, vijana na walemavu ili kuinua hali yao ya kimaisha.

Anaongeza kuwa baadhi ya wanawake na wasichana wamepata tabu kwa kukosa sodo mbali na changamoto nyingine.

“Nitaanzisha miradi ambayo itashughulikia changamoto hizo,” akasema Bi Marubu alipotangazwa mshindi wa kiti hicho.
Bi Amina Dika ambaye ni mwakilishi wa Kaunti ya Tana River alisema kuwa yuko na uwezo wa kuleta maarifa mapya na kwamba kinamama wanahitaji usawa.

Wawakilishi wengine katika ukanda wa Pwani ni, Bi Lydia Haika (Taita Taveta), Bi Fatuma Masito (Kwale) na Bi Getrude Mbeyu (Kilifi).

Mashauri wa masuala ya kisiasa, Bw Bozo Jenje anasema kuwa ingawa inaweza kuwa mapema kutarajia viongozi hao kueleza mipangalio yao,ni vyema waanze kwani hata magavana wanaendelea kuweka mikakati ya kuimarisha kaunti zao.

“Mbunge wa kaunti anahudumia kaunti nzima kama gavana,hivyo basi anafaa kuanza mapema kuhakikisha amefika maeneo-bunge yote na kueleza ajenda yake kwa wananchi,” asema Bw Jenje.

Bw Jenje anasema utendakazi wa wabunge hao wa kaunti unafaa kuonekana kupitia miradi ya maendeleo kwa jamii kama vile vikundi vya kina mama na vijana.

Hoja hiyo inaungwa mkono na mchanganuzi wa siasa za Pwani, Bw Abdulrahman Abdalla anayesema kuwa wabunge hao wa kaunti wanafaa wajitokeze na kuwaelezea wananchi ni miradi gani wanayonuia kuitekeleza katika kipindi chao.

Bw Abdalla anasema kuwa wakati wa kampeni, wabunge hao wa kaunti, sawia na viongozi wengine, walitoa ahadi chungu nzima ndiposa inafaa waanze kuzitekeleza mapema na kuonyesha ari ya kuwafanyia kazi wananchi.

“Hata kama ni mradi mmoja kwa mwaka, ni vizuri wabunge hao wawaambie wananchi,” akasema Bw Abdalla ambaye pia alikuwa mwasiasa kupitia chama cha Kanu miaka iliyopita.

Kulingana na Bw Abdalla, kiti cha uwakilishi wa wanawake kinafaa kuangaziwa kwani wananchi wengi hawajui majukumu ya kiti hicho licha ya kuwa afisi ya kisiasa kama zile nyingine.

Mama mmoja kutoka eneo la Shanzu, Kaunti ya Mombasa aliyetaka jina lake libanwe, anasema bado hawajaona faida ya kiti hicho cha ubunge wa kaunti kwani licha ya kuwa katika vikundi kadhaa vya akina mama, hawajasaidika.

“Tunasikia kuna pesa huwa zinatolewa (Ngaaf) lakini hatujui huwa zatumika vipi au watu huzipataje kwani pia sisi tunazihitaji katika vikundi vyetu,” akasema mama huyo.

You can share this post!

JUKWAA WAZI: Junet, Ichung’wa wakabana koo kuhusu...

Real Madrid wakomoa Sevilla na kufungua pengo la alama sita...

T L