• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 8:55 PM
KIGODA CHA PWANI: Ziara ya Raila Mombasa kulinda ngome yake dhidi ya wimbi la KK

KIGODA CHA PWANI: Ziara ya Raila Mombasa kulinda ngome yake dhidi ya wimbi la KK

JE ziara ya kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Bw Raila Odinga jijini Mombasa wiki jana ilikuwa ni ya kulinda ngome yake ya ukanda wa Pwani kutoka kwa muungano tawala wa Kenya Kwanza?

Hili ni swali watu wengi wanajiuliza kwa kuwa ziara hiyo ilifanyika siku chache tu baada ya Rais William Ruto kumaliza ziara yake fupi ya sherehe za kufungua mwaka mjini Mombasa alipokaa kwa takriban siku nne.

Katika ziara yake, Bw Odinga alikutana na viongozi waliochaguliwa kupitia chama cha ODM kuanzia wabunge hadi wawakilishi wa wadi pamoja na wajumbe wa chama hicho katika kaunti ya Mombasa.

Kulingana na baadhi ya wachanganuzi wa siasa, ziara ya Bw Odinga ilikuwa ni ya kukata makali ile ya Rais Ruto ambapo viongozi wengi wa chama cha ODM walionekana kuhudhuria hafla zake.

Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir na mwenzake wa Kilifi Gideon Mung’aro ni mojawapo ya viongozi waliohudhuria baadhi ya vikao na mikutano ya Rais Ruto akiwa maeneo ya Mombasa na Kilifi.

Hata hivyo baadhi ya wanasiasa waliohudhuria vikao hivyo walisema kuwa kujiunga katika mikutano ya Rais ilikuwa ni kwa sababu ya maendeleo ya ukanda wa Pwani.

Baadhi ya wananachi wamesema kuwa kuhudhuria kwa wanasiasa wa upinzani katika mikutano ya Rais ni baadhi ya majukumu ya nyadhifa zao ingawa ilikuwa nadra sana miaka iliyopita kupata kiongozi wa upinzani akiwa amehudhuria shughuli za rais wa chama tawala.

Hata hivyo, baadhi ya wachanganuzi wa siasa wanaamini kuwa viongozi wengi waliochaguliwa kupitia vyama vya upinzani hususan kile cha ODM wanatarajiwa kujiweka karibu na upande wa Rais Ruto.

Katika ziara yake, Bw Odinga alipuzilia mbali madai ya kuwa ukanda wa Pwani umemponyoka kama ngome yake na ile ya chama cha ODM na kutwaliwa na Kenya Kwanza.

Akizungumza na wanahabari, Bw Odinga pia alikanusha madai ya kuwa Bw Hassan Joho ambaye ni mmoja wa naibu viongozi wa ODM alikuwa hashughuliki na chama kwa kutoonekana katika mikutano yake (Bw Raila).

Bw Odinga alisema kuwa Bw Joho alikuwa nje ya nchi na akirudi ataendelea na mchango wake wa kuimarisha chama cha ODM.

Aliongeza kusema kuwa Bw Nassir ambaye alikuwa katika ikulu ya rais mjini Mombasa wakati wa sherehe za kuvuka mwaka alikuwa ni mwanachama wa ODM.

Hata hivyo, Bw Odinga alisema kuwa chama tawala kilikuwa kinajaribu kunasa viongozi waliochaguliwa chini ya mwavuli wa Azimio kupitia vishawishi.

“Uhusiano baina ya serikali za kaunti na ile ya kitaifa uko katika katiba ndiposa magavana wanafaa kufanya kazi na serikali ya kitaifa,” alisema Bw Odinga.

Viongozi wa Mombasa wa ODM wakiongozwa na Bw Nassir walisema watabakia katika chama hicho na hawatahama.
Wabunge Badi Twalib (Jomvu), Rashid Bedzimba (Kisauni), Masoud Machele (Mvita), Omar Mwinyi (Changamwe) na seneta Mohamed Faki waliohudhuria mkutano huo uliohutubiwa na Bw Odinga waliapa kubakia kwa chama cha ODM.

“Tubaki kwa chama chetu,hii ni ngome yako, wawakilishi wadi wengi ni wa chama cha ODM,” alisema Bw Twalib.

Mchanganuzi wa masuala ya siasa Prof Halimu Shauri alipuuza dhana ya kuwa ziara ya Bw Odinga ilikuwa ni kwa sababu ya kulinda ngome yake ya chama cha ODM kutoka kwa muungano wa Kenya Kwanza.

Prof Shauri ambaye pia ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Pwani kilichoko Kilifi alisema kuwa baadhi ya watu wameitafsiri vibaya ziara ya Bw Odinga Mombasa.

Aliongeza kusema kuwa, Bw Odinga alikuwa hashtuliwi na ziara ya Rais Ruto jijini Mombasa.

Prof Shauri alisema kuwa kiongozi mwenye hadhi ya Bw Odinga hawezi kutoa ujumbe wake kwa taifa katika vijiji au miji midogo ndiposa labda alichagua kuongea kuhusu Bw Wafula Chebukati, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) katika ziara yake ya Mombasa.

“Ujumbe huo una uzito iwapo utatolewa katika mji unaojulikana,” alisema Prof Shauri akiongeza kusema kuwa Bw Odinga kuzuru Mombasa hakumaanishi alikuwa na wasiwasi kuhusu ngome yake na ziara ya Rais Ruto.

Wakili Yusuf Aboubakar ambaye pia ni mchanganuzi wa siasa alisema kuwa ziara ya Bw Odinga ilikuwa ni ya kuonyesha kuwa bado yuko na ushwawishi mkubwa katika ukanda wa Pwani.

Kulingana na Bw Aboubakar ziara ya Bw Odinga ilikuwa ni dhihirisho ya kuwa Mombasa ni ngome yake na hafai kupuziliwa mbali.

“Ziara hiyo ilikuwa ni ujumbe wa kisiasa kuonyesha kuwa anashikilia ngome ya pwani pamoja na chama chake cha ODM,” alisema Bw Aboubakar.

Kulingana na Dkt Daniel Mwaringa ambaye ni mhadhiri katika chuo kikuu cha ufundi cha Mombasa (TUM) kuna hali ya wasiwasi ambayo imetanda katika chama cha muungano wa Azimio na kwamba baadhi ya watu wanakihama.

“Katika Azimio Bw Raila anataka kujipatia umuhimu ambao amepoteza,amepoteza umuhimu huo katika ukanda wa Pwani,” alisema Dkt Mwaringa.

Dkt Mwaringa aliongeza kusema kuwa katika ukanda wa Pwani,baadhi ya watu wanahama Azimio na kuelekea muungano wa Kenya Kwanza.

  • Tags

You can share this post!

JUNGU KUU: IEBC gae Chebukati, wenzake wakistaafu

Mkenya Ondoro ashinda Houston Marathon kwa mara ya pili,...

T L