• Nairobi
  • Last Updated December 3rd, 2023 8:00 PM
KIKOLEZO: Blanda za R. Kelly

KIKOLEZO: Blanda za R. Kelly

Na THOMAS MATIKO

SIKU ya kufa nyani, miti yote huteleza.

Akiwa na umri wa miaka 54, staa wa RnB Robert Kelly al-maarufu R. Kelly, anapitia kipindi kigumu cha maisha yake.

Pale alipo kwa sasa, anachukia na kujutia umaarufu alioupata. Umaarufu huo uliompa ushawishi mkubwa, sasa unatishia kumwangamiza kabisa. Wiki iliyopita, alipatikana na kesi ya kujibu akishtakiwa na makosa 16 ya kingono na unyanyasaji wa kimapenzi. Kwa makosa hayo, huenda akahukumiwa kifungo cha maisha, mahakama itakapotoa uamuzi wake mwaka kesho.

NGORI ILIKOANZIA

Kwa zaidi ya miongo miwili sasa, R. Kelly amekuwa akikabiliwa na tuhuma za unyanyasaji wa kimapenzi dhidi ya wanawake kadhaa.Madai haya yalianza kuchipuka katika miaka ya 1990s, alipodaiwa kuwa na tabia ya kuwawinda wasichana matineja kisha kuwanyanyasa kimapenzi.

Huenda uovu huu ulichangiwa na alichopitia utotoni. Kwenye kitabu cha wasifu wake, alifichua kwamba aliwahi kulawitiwa kimapenzi na mwanamke mmoja wa familia yake, alipokuwa na miaka minane tu.

Lakini je, sakata yake ilianzia wapi?

1994: AMWOA TINEJA AALIYAH

Akiwa na umri wa miaka 27, alifunga ndoa ya kisiri na nyota marehemu Aaliyah aliyekuwa na umri wa miaka 15 kipindi hicho.

Jarida la Vibes Magazine baadaye lilibaini kuwa Aaliyah aliongopea kuhusu umri wake kwenye cheti chao cha ndoa.

Kesi ilipofikishiwa mahakamani, mfanyikazi wake wa zamani alitoa ushahidi dhidi yake kwa kudai kuwa alihongana ili Aaliyah apate kitambulisho bandia kuonyesha kwamba ametimiza umri wa miaka 18.

Kwa upande wa Aaliyah, aliishi kukana kuwa kwenye mahusiano naye.

R. Kelly ndiye aliandika na kuproduzi albamu ya kwanza na ya pekee ya Aaliyah iliyoitwa Age Aint Nothing But A Number.

Baada ya kifo chake 2001, aliamua kusalia kimya kuhusu uhusiano wao na kila alipoulizwa, aligoma kujibu akisema kafanya hivyo kwa heshima za mwendazake.

1996: ASHTAKIWA NA EX TIFFANY

Tiffany Hawkins alifungua mashtaka dhidi yake akimshtumu kwa kumsababishia majeraha mwilini na msongo wa mawazo kipindi walipodeti kwa miaka mitatu.Alidai kuwa alianza kushiriki ngono na R. Kelly akiwa na miaka 15 tu na jamaa akiwa na 24 kipindi hicho. Uhusiano wao ulifika mwisho alipotimiza miaka 18. Tifanny alitaka kulipwa fidia ya dola 10 milioni (Sh100 milioni) lakini aliishia kukubali Sh2.5 milioni baada ya kushawishiwa na R. Kelly na kesi kumalizika.

2001: ASHTAKIWA NA MWANAFUNZI

Tracy Sampson alifungua mashtaka dhidi yake akimshtumu kwa kumshurutisha kushiriki naye mapenzi.Kipindi hicho Tracy alikuwa na miaka 17 na alikuwa akijifunza kazi katika lebo ya Kelly Epic Records. Anasema jamaa alikuwa akimkazia maisha kwa kumpangia sehemu anazopaswa kwenda na watu anaopaswa kutangamana nao. Kesi hiyo ilimalizika nje ya korti baada ya R. Kelly kuamua kumfidia na kiasi cha fedha ambacho hakikuwekwa wazi.

MEI 2002: KESI ZAIDI DHIDI YAKE

Kati ya Aprili na Mei mwaka huo, kesi zaidi ziliwasilishwa dhidi yake. Patrice Jones alimshtaki kwa kumpachika mimba akiwa tineja wa chini ya miaka 18. Anasema alilazimika kutoa ujauzito huo.Mwanamke mwingine mchanga Montina Woods, naye akamshtaki kwa madai ya kumrekodi akiwa anashiriki naye ngono bila ya kumwarifu.Kesi zote hizo R. Kelly alizimaliza kwa kuwalipa watuhumu wake kiasi cha fedha kisichojulikana huku nao wakitakiwa kutozungumzia sakata hizo.

JUNI 2002: KESI DHIDI YA WATOTO WACHANGA

Alifunguliwa mashtaka 21 ya kumdhulumu binti mchanga kwa kutengeneza video za dhuluma za kingono. Anadaiwa kumchanganya binti huyo na kumpelekea kushiriki ngono naye kisha akarekodi. Ilichukua miaka sita kwa kesi hiyo kuanza kusikilizwa toka ilipowasilishwa. Mahakama ilimwachilia huru baada ya ushahidi kushindwa kuthibitisha kuwa mrembo huyo alikuwa kweli mchanga matukio hayo yalipotokea.

2004: AKAMATWA NA MKANDA WA NGONO

R. Kelly alikamatwa na polisi na kushtakiwa na makosa 12 ya kuwadhulumu watoto kingono. Staa huyo alikamatwa akiwa kwenye likizo na kukutwa na kamera waliyotumia polisi kumfungulia mashtaka.

Kwenye kamera hiyo, polisi walipata video aliyokuwa amerekodi akishiriki ngono na binti wa chini ya miaka 18.Kesi hiyo ilitupiliwa mbali baada ya jaji kukata kauli kuwa polisi hawakuwa na ushahidi wa kutosha kuhusu tuhuma dhidi yake, walipokwenda kumkamata.

2017: ‘Awateka’ MADEMU SITA

Jarida la Buzzfeed lilichapisha makala na kufichua kuwa R. Kelly, alikuwa ‘kawateka’ mademu sita aliowatumia kufanya naye ngono. Buzzfeed ilidai kuwa aliwanasa wasichana hao mmoja baada ya mwingine.

Hii ilikuwa ni pale kila mmoja wao alipomtokea kuomba usaidizi wake wa kutoka kimuziki. Ikawa kwamba ili akusaidie, ni lazima ukubaliane na matakwa yake.

Kwa kukubaliana na matakwa yake, R. Kelly ndiye alikuwa akiamua watakachokula, watakavyovaa, muda gani wanapaswa kuoga, kulala na pia kushiriki ngono naye huku akirekodi. Pia aliwapokonya simu zao ili wasiweze kuwasiliana na mtu yeyote.

Taarifa hizi zilifichuliwa na wafanyakazi wake wa zamani.

2018: WATUHUMU WAJITOKEZA

Baada ya ripoti ya Buzzfeed kutoka, watuhumu kadhaa dhidi yake walipata nguvu na kujitokeza kuelezea masaibu yao.Jerhonda Pace aliyelipwa fidia kusalia kimya alikiuka mkataba huo na kufichua kwamba alianza kushiriki ngono na jamaa akiwa chini ya umri wa miaka 18.

Mwanamke mwingine Kitti Jones naye alidai kulazimishwa kushiriki ngono na wanawake wengine na R. Kelly na wakati mwingine alipokiuka amri, jamaa alimshushia kipigo.

Kitti aidha alikuwa miongoni mwa waliokuwa na ukaribu naye waliofichua ufidhuli na dhuluma walizopitia mikononi mwa jamaa, walipohojiwa na BBC Three Documentary, Machi 2018.

Lovel Jones rafiki wa zamani wa R. Kelly, alifichua kuwa jamaa aliwahi kumtuma kumsakia mabinti wachanga hasa kwenye masherehe. Alidai kwamba lilikuwa jambo la wazi kuwa jamaa alipendelea ngono na mabinti wachanga.

2018: Kampeni ya ‘Mute KELLY’

Kampeni ya ‘Mute Kelly’ (Mnyamazisheni Kelly) ilianzishwa ikilenga kuhakikisha kuwa ngoma za staa huyo hazichezwi kwenye vyombo vya habari.

Pia mapromota wa shoo zake nao walilengwa huku nazo tovuti za kupakia na kupakua muziki kama vile Spotify, Apple Music na Pandora zote zikiafikia uamuzi wa kuondoa nyimbo zake kwenye mitandao yao. Ni uamuzi ambao baadaye ziliupiga chini.

Kipindi hicho tu, alishtakiwa na mpenzi wake mwingine wa zamani, aliyedai kuwa jamaa alimwambukiza ugonjwa wa zinaa makusudi.

2019: Filamu MPYA YAMFUNGA

Lifetime documentary Surviving R. Kelly ndiyo filamu iliyochora picha kamili ya maovu na sakata ya staa huyo. Wiki mbili baada ya kupeperushwa, lebo yake ilimchuja huku shoo zake zilizokuwa zimepangiwa kufanyika Marekani na New Zealand zikifutiliwa mbali. Februari mwaka huu, wakili wa maceleb Michael Avenatti, alimfungulia mashtaka baada ya kusema amepokea video ya ngono inayomwonyesha staa huyo akishiriki ngono na binti mwenye umri wa miaka 14.

Kesi hiyo ilipowasilishwa, uongozi wa mashtaka nao uliishia kuongeza mashtaka mengine 11 yaliyomshtumu kwa kuwashurutisha mabinti wenye umri wa kati ya miaka 13 hadi 16 kushiriki naye ngono.

Aidha alishtakiwa kwa njama ya kuwatishia maisha mashahidi na pia kuwa na mipango wa kuwasafirisha mabinti wachanga kutoka Illinois hadi Brookyln kwa lengo la kuwatumia kingono.

Agosti mwaka huo, alinyimwa dhamana na mahakama kwa kuhofia anaweza kutoroka nchi au pia kuvuruga ushahidi.

JUNI 2021: MAWAKILI WAMTOROKA

Miezi miwili kabla ya kesi yake kuanza kusikilizwa rasmi, aliwaajiri mawakili wapya ili kukitia nguvu kikosi chake cha wanasheria.

Hatua hiyo ilipelekea mawakili wake wa awali Steve Greenberg na Michael Leornard kujiondoa kwa madai kuwa hawangeweza kufanya kazi na mawakili wapya walioajiriwa.

AGOSTI 2021: APATIKANA NA KESI YA KUJIBU

Kesi ya mashtaka yote dhidi yake ilianza kusikilizwa Agosti 18.

Baada ya zaidi ya wiki nne ya kusikilizwa kwa kesi hiyo ambapo zaidi ya mashahidi 30 walipanda kizimbani, majaji walimpata na hatia kwenye mashtaka yote yaliyowasilishwa dhidi yake.

Hukumu ya kesi hiyo itafanywa Mei 4, 2022 na kuna uwezekano mkubwa akafungwa maisha.

Baada ya maamuzi hayo kutolewa, wakili wa baadhi ya watuhumu Gloria Allred, alikuwa na haya ya kusema; “Kwa miaka 47 niliyojihusisha na sheria, nimewafuatilia wahalifu wengi wa ngono dhidi ya wanawake na watoto. Kwa wote hao, naona R. Kelly ndiye mbovu zaidi”.

You can share this post!

Hofu ya Pwani kususia kura za 2022 yatanda

Umiliki wa Newcastle United watwaliwa na mabwanyenye wa...