NA SINDA MATIKO
KUNA sanaa fulani ya uchekeshaji ambayo Wakenya bado wanahangaika kuielewa, iitwayo ventriloquism (uchekeshaji kwa kutumia kikaragosi kwa Kiswahili).
Hii ni sanaa ya uchekeshaji kwa kutumia kikaragosi. Kitokeacho hapa ni msanii mchekeshaji kuigiza kama vile anafanya maongezi ya majibizano kati yake na kikaragosi.
Idadi kubwa ya watu hasa Afrika ambapo sanaa hii sio maarufu, wameishia kuamini mambo mengi sana.
“Wapo watu ambao wamedai huwa nina rekoda ya sauti niliyotia kwenye kikaragosi na ndio huwa ninajibizana nayo, ikaonekana ni kana kwamba ninazungumza na kikaragosi chenyewe,” anasema Nelson Wachira Gitonga, almaarufu Jonte.
Gitonga ndiye msanii mchekeshaji wa pekee anayeifanya sanaa hii ya uchekeshaji kwa kutumia kikaragosi hapa nchini.
“Nilipokuwa kijijini Desemba kuna baadhi ya watu walidai natumia uchawi kufanya kikaragosi kuzungumza wakati sio kiumbe hai,” Jonte anazidi kutiririka.
Ventriloquisim ni nini?
Kutokana na mkanganyiko huu, Wachira na kikaragosi chake alichokipa jina la Jonte, ameamua kujitwika mzigo wa kujaribu kuwaelewesha Wakenya kuhusu sanaa hii.
“Sio kwamba kikaragosi huwa kinazungumza au kwamba ina rimoti, hapana. Ni mbinu ya usanii ambayo kama msanii unajifunza kuzungumza pasi na kufungua mdomo kwa hiyo sauti inakuwa ikitokea kooni,” anafafanua.
Lakini sio hiyo tu, ili kuaminisha watu kwamba ni kile kikaragosi ndicho kinachozungumza, msanii hutakiwa kubadilisha sauti iwe tofauti na yake.
“Sanaa hii humpa msanii hulka mbili za watu tofauti. Kwa mfano, ninapouliza swali huwa nazungumza kwa ukawaida wangu, ila inapotakiwa Jonte ajibu, lazima nibadilishe sauti iwe ni kama ni yeye ndiye anajibu lakini pia nimchezeshe kama vile ni binadamu. Hii ina maana nimtingize kichwa, au nichezeshe mikono yake kujenga taswira ya kwamba ni kiumbe hai wakati siyo.”
Kutokana na majukumu haya, hii sio mbinu rahisi kwa sababu mwanzo ni lazima ufanye mazoezi ya siku nyingi kuelewa namna ya kuzungumza kutokea kooni pasi na kuonekana unazungumza kwa mdomo wako.
“Zipo herufi ngumu kama zile voweli ambazo huwa ngumu sana kutamkika pasi na kufungua mdomo hivi lazima ufanye mazoezi ya kutosha.”
“Kujigawanya kuwa mtu wa hulka mbili sio jambo rahisi sababu natakiwa kuwa Wachira na vile vile Jonte. Unahitaji uelewa na maarifa makubwa. Waliobobea kwenye sanaa hii wana uwezo wa kuwa na hulka hadi ya watu watano, sio rahisi.”
Je inalipa?
Licha ya kuwa ni sanaa mpya, Jonte anashukuru kwamba Wakenya wameanza kuikubali na hii ni kwa sababu ya ule ucheshi na uhusika.
Siku za hivi karibuni, amejikuta akitengeneza fedha kiasi cha haja kwa kupiga shoo kadhaa kwenye kumbi na hafla mbalimbali.
“Huwa nachaji Sh3,000 kwa shoo ya dakika tano na kiasi hicho hupanda kwa kutegemea na hafla na muda ninaotakiwa kupiga shoo.”
Kazi hii sasa imeanza kumwingizia kipato zaidi ya kazi ambayo amekuwa akifanya kwa zaidi ya miaka saba.
“Sikufanikiwa kusoma baada ya babangu kufariki maisha yakawa magumu sababu tulikuwa watoto wengi nyumbani kwa hiyo baada ya kidato mama anakutimua nyumbani ukajipange.”
Alijaribu kuwa makanga, fundi wa mjengo na kila aina ya kibarua alichopatana nacho kabla ya kupata kazi yake ya sasa ya kuangamiza wadudu wasumbufu maafisini na manyumbani kwa unyunyuziaji dawa almaarufu fumigation.
Ila kwa sasa mambo yanabadilika.
“Jonte ananiingizia kipato zaidi ya kazi yangu hii na nashukuru. Ila matamanio yangu ni kwa Wakenya kuweza kuielewa sanaa hii. Hilo likitokea nina uhakika kutengeneza pesa za maana haitakuwa tatizo.”