• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
KIKOLEZO: Wazito waliojipanga

KIKOLEZO: Wazito waliojipanga

NA SINDA MATIKO

JANGA la Covid-19 lilipozuka, jambo moja lililojitokeza na kuwashangaza wengi ni jinsi wasanii walivyogeuka na kuwa ombaomba.

Kutokana na ukosefu wa kazi ikizingatiwa kuwa wengi wao hutegemea sanaa kuingiza kipato, wengi waliumia. Hii ikaibua mjadala mmoja ambao kila mdau alikuwa akihoji, je wasanii huwa hawawekezi?

Majibu ni mawili, wapo wale ambao hawajali na pia wapo ambao wanachakarika hapa nje. Leo tunawaangazia wasanii ambao hawategemei kipato cha muziki kujiingizia riziki.

BUTITA

Mchekeshaji huyu anamiliki kampuni ya SPM Buzz inayojihusisha na masuala ya habari za burudani. Lakini pia kampuni hii, inajihusisha na utengenezaji wa sinema na pia matangazo ya kibiashara ya wateja mbalimbali.

KHALIGRAPH JONES

(Biashara ya magari) Rapa Jones ni mmoja wa wasanii ambao kila leo huwasisitizia wasanii wenzake umuhimu wa uwekezaji. Muziki wake umekuwa ukimlipa vizuri kwani ni kati ya wasanii wachache mno wasiokosa shoo.

Lakini moja ya vitu vikubwa ambavyo mashabiki wengi na wale wanaomfuatilia wamegundua kutoka kwake ni hamu yake kubwa ya magari. Mara kwa mara rapa Jones huposti magari aina aina ya kifahari kwenye mitandao yake ya kijamii. Juzi kati aliulizwa ana magari mangapi na kwa nini anapenda kuringisha sana mashine zake mitandaoni.

“Ungeniuliza miaka minne au mitano iliyopita nina magari mangapi, ningekuambia nane au kumi lakini siko huku tena. Gari nyingi ambazo watu wamekuwa wakiona naposti na kujijazia, wasichojua zingine sio za kwangu. Ni magari ya kibiashara sababu nipo kwenye biashara ya magari.”

Kuna kila sababu za kuamini kakake mkubwa rapa Lamaz Span ambaye amekuwa kwenye biashara hiyo kwa miaka na mikaka ndiye aliyemvuta huko.

NADIA MUKAMI

(Saluni, Wakfu wa Lola, Kampuni ya Sevens Creative Hub) Nadia anaingiza pesa za kutosha kupitia mauzo ya muziki wake iwe ni kupitia tovuti za kupakia na kupakua muziki kama vile Boomplay, YouTube, Spotify, Apple Music na kadhalika.

Vilevile, Mukami anaingiza pesa kupitia shoo anazopiga na kando na hiyo anaingiza hela anapotumika kwenye dili za biashara matangazo. Lakini nje ya vipato hivi vinavyoingizwa kwa njia ya muziki, pembeni anafanya mambo mengine.

Kupitia kampuni yake ya Sevens Creative Hub, Nadia anajihusisha na biashara ya kutoa huduma za Experiential. Hii ni biashara ambayo kwamba mteja anapokuwa ana tukio lake , basi Sevens inajukumika kuhakikisha wateja wote wanafurahia huduma. Aidha, Sevens inayo studio ambayo hurekodi muziki kwa ada lakini pia hujihusisha na uandaaji wa biashara matangazo. Kando na hilo, Nadia kaanzisha wakfu wake wa Lola ambapo lengo ni kuwapeleka chuo zaidi ya mabinti 100. Hili analifanya kwa kuwasaka wadhamini ambao hupampu fedha kwenye wakfu huo. Juzi kati Nadia alifungua saluni ya kifahari katikati mwa jiji na biashara hiyo anasema inampeleka vizuri.

KING KAKA

(Kaka Empire, Kaka Clothing, King Kaka Foundation) Rapa King Kaka amekuwa kwenye gemu kwa miaka na mikaka.

Alianza bila chochote wala lolote ila kwa sasa ana jambo lake. Ni miongoni mwa wasanii wachache ambao wameweza kuishi maisha yao vizuri bila ya kutegemea kipato cha muziki kila kukicha.

Msanii Kennedy Ombima almaarufu King Kaka. PICHA | MAKTABA

Baadhi ya biashara zake ni lebo yake ya Kaka Empire ambayo ni lebo ya usimamizi na utayarishaji muziki. Baadhi ya wasanii ambao wamewahi kusimamiwa na Kaka Empire ni pamoja na Avril, Rich Mavoko, Timmy TDat, Owago Onyiri na Femi One ambaye ameendelea kuwa chini ya lebo hiyo licha ya wasanii wengine wote kujitoa. Vile vile, King Kaka anamiliki laini yake ya mavazi ambayo humwingizia kipato kwa kuwauzia mashabiki dizaini ya mavazi yake ambao hupendezwa na swagg yake. Pia ana wakfu wake ambao umejikita mno kwenye usambazaji wa sodo kwa wasichana wanaotokea familia za kimaskini na maeneo ya ukame ambapo wasichana wanapata tabu kupata bidhaa hii muhimu.

NAMELESS & WAHU

Mke na mume wamekuwa kwenye muziki kwa miaka na mikaka. Wanatajwa kuwa wanamuziki wenye utajiri mkubwa, utajiri ambao wameutengeneza kupitia muziki. Wawili hao wanamiliki maghorofa kadhaa jijini Nairobi ambako wao hukusanya kodi kila mwezi kutoka kwa wapangaji. Kando na hayo, Wahu anamiliki saluni kubwa katika mitaa ya kifahari ya Westlands.

SAMIDOH

Kwa sasa hakuna msanii wa muziki wa Mugithi anayefanya vizuri kama Samidoh. Skendo zake za kimapenzi pia zimechangia kumuuza sana. Lakini kando na muziki wake, Samidoh kajitengenezea himaya yake ya kipato. Mjini Nakuru anakotokea, msela anamiliki mgawaha wa burudani na msosi uitwao Unique Tavern. Vile vile, 2021 alianza mradi wa ujenzi wa ghorofa ya upangaji jijini Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tutumie vizuri Kumi hili la Mwisho la...

Dini potovu lasababisha maafa ya wanne

T L