• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 8:00 AM
Kioja ndume wa kupigana wakifurusha waombolezaji Kakamega   

Kioja ndume wa kupigana wakifurusha waombolezaji Kakamega  

 

NA TITUS OMINDE

MAZISHI ya askofu mmoja katika kijiji cha Burimbuli, Shihuli, Kaunti ya Kakamega mnamo Jumamosi, Mei 27, 2023 yalitamatika kwa fujo pale ndume wa kupigana walipofurusha waombolezaji waliokuwa wamebaki katika boma la mchungaji huyo.

Waombolezaji walitimuliwa kila mmoja akichukua gari nambari mguu niponye, vurumai zilizoashiria kilele cha maziko hayo.

Sarakasi ilianza baada ya askofu Ken Kwasira wa kanisa la Word of Christ Prophetic kuzikwa, ambaye pia alikuwa mmoja wa wamiliki wa ndume wa kupigana katika jamii ya Waluhya Kaunti Ndogo ya Shinyalu.

Kulingana na mila ya jamii hiyo, ni kwamba kila anakozikwa mmiliki wa ndume wa kupigana ni lazima sherehe itamatishwe kwa miereka ya fahali.

Punde baada ya mwendazake kuzikwa wamiliki wa ndume hao walianza kuingia kwa boma la mwendazake huku wakishangilia ndume wao tayari kwa mapigano ya kuashiria kuzikwa kwa shujaa mmiliki wa ndume.

Baadhi ya ndume walioshiriki miereka baada ya mazishi ya askofu Ken Kwasira mmiliki wa ndume wa kupigana Kakamega mnamo Mei 26, 2023. Picha / Titus Ominde

Ili kuwapa mori ndume husika, wenyeji waliwashangilia huku wakichimbua mchanga kwenye kaburi la mwendazake kama njia moja ya kuomboleza marehemu kabla ya miereka.

Punde si punde, boma la marehemu lilibadilika na kuwa uwanja wa miereka kati ya ndume ambao walikuwa wametawala uwanja wa boma hilo.

Ndume hao walianza kupigana huku wakifurusha waombolezaji haswa wale ambao hawakufahamu mila za jamii hiyo.

Ghafla bin vuu, boma lilisalia mahame huku familia ya karibu ya marehermu ikijifungia ndani ya nyumba kukwepa kuvamiwa na ndume hao.

Mmmoja wa wazee ambao waliongoza mapigano hayo, Bw Joseph Kwarula alisema ni lazima sherehe ya kupiganisha fahali ifanywe punde tu baada ya kuzikwa kwa mmiliki wa ndume wa aina hiyo.

Kwarula alisema iwapo ndume hawatashiriki vita huenda kukatokea mkosi katika jamii.

“Hii si fujo ni kawaida mmoja wetu anapokufa ni sharti kushuhudiwe miereka ya ndume ili kufurahisha wazee wa jadi, mbali na kufurahisha mwendazake. Sherehe kama hii vile vile hutumika kuondoa laana katika jamii,” alisema Bw Kwarula.

Aidha, Kwarula aliwataka wageni ambao hawaelewi tamaduni hiyo kutokaribia katika ulingo wa masumbwi kwa kuonya kuwa wakati mwingine fahali hao wenye mori na hasira huvamia watu waliokaribu na wakati mwingine hutokea maafa.

“Wakati wa mapigano haya hutokea ajali na hata wakati mwingine fahali hawa wanaweza kuvamia watu na hata kuwaua,” alisema Bw Kwarula.

Hata hivyo, utulivu ulirejea bomani humo baada ya mapigano hayo kutulizwa.

  • Tags

You can share this post!

Seneta Onyonka: Rais Ruto yafanye magazeti kuwa rafiki...

Harusi ya kukata na shoka ya wanandoa wenye ulemavu kuskia...

T L