• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
KIPWANI: “Naskia fiti, naskia poa…”

KIPWANI: “Naskia fiti, naskia poa…”

NA SINDA MATIKO

“SIJUI mbona naskia fiti, naskia poa, mbona naskia fiti naskia poa mi naskia…”

Utakuwa unajua ni mshororo wa hiti gani kama wewe ni mfuatiliaji mzuri wa sanaa yake Mohammed Ali Said ukipenda Masauti.

Sio siri kuwa kwa sasa yeye ni miongoni mwa wasanii wachache kutoka Mombasa wanaozidi kuuweka muziki wa Pwani kwenye ramani. Juzikati alipiga mastori na kufunguka safari yake ya muziki.

Sababu za kujiita Masauti ni zipi?

Jina lilitokea kiutani, kuna produsa kwa jina Ian Michapo kule Mombasa ndio alinibandikiza. Ian alikuwa anamiliki studio ikawa nakwenda kule kila siku kufanya mazoezi sababu sikuwa najua kuimba kabisa.

Hukuwa unajua kuimba?

Eeeh! Ian alikuwa akinipa voko za wasanii tofauti tofauti ili nifanye mazoezi nazo kwa ajili ya kuboresha voko zangu. Kwa hiyo mara nyingi alikuwa akija ananikuta nilishafungua studio nafanya mazoezi. Siku moja alikuja na akiwa nje akasema “Nakusikia mzee masauti hayo yanaanza kukuakua” basi jina likashika.

Baadaye ulihamia Nairobi mazima, unaona ukirudi Mombasa?

Toka nije Nairobi 2014 kujitafuta kimaisha na kimuziki, sijawahi kurejesha makaazi yangu Mombasa mpaka leo.

Ulikuwa ni uamuzi uliofanya au ulijikutaje Nairobi?

Nilichukuliwa na J Blessing (mwelekezi video) nikaishi naye mara kidogo ikatokea mushkili bado sikurudi nyumbani nikawa nahamiahamia kwa masela kama vile produsa Motif hadi nilipojikuta nipo kwangu.

Halafu siku hizi umeanza kama kuimba kwa kizungu pia hatujakuzoea hivyo?

Maisha yangu yote naimba Kiswahili si afadhali nijaribu kuimba Kiingereza kidogo nione kama na watu wanaozungumza Kiingereza watanisikiza.

Shule ulienda ipi?

Aah, shule nilienda kadhaa Gideon Ngala, Ananda Marga na Imara Daima.

Kwa nini ulibadilisha shule sana, au matokeo?

Duh! Shule ilikuwa noma. Sikupepeta masomo. Kusema ule ukweli mtu akiniona asiniulize mambo ya shule. Mimi shule sikuwa vizuri angalau nilijisukuma sukuma nikafika kidato cha pili. Matokeo ya darasa la nane hayakuwa vizuri hata kidato cha pili nilipoachia sijui nilifikaje fikaje. Ilikuwa noma. Kidato cha kwanza sikusoma kabisa nashangaa nilijikuta kidato cha pili.

Aisee, eti eeh?

Ndio bwana lakini Alhamudhulilahi Mungu ni nani akikunyima huku anakujali kule. Aliniambia mwanangu eeh, wewe sio msomi wewe ni mwimbaji.

Kwa hiyo masomo yako yaliishia kidato cha pili. Ila sasa unaishi vizuri, unasukuma mashine nzito?

Nashukuru Mungu anasaidia najaribu tu.

Umefanya kazi na wasanii kadhaa, ni yupi unayeweza kusema ilikuwa rahisi?

Nafikiri Mr Seed, ilitokea tu alinipigia simu akaniomba nipitie studio hatukuwa na mazoea kabisa. Hatukuwa tumewahi patana na kawaida kama wasanii hatujuani huwa tunatumiana ngoma, lakini aliniomba nifike studio nikatia voko tukaunda ile hiti ya Dawa ya baridi.

Yule ambaye alikusumbua?

Siwezi kusema ni msumbufu lakini ambaye anapenda kufanya kazi zake zikiwa zimenyooka kwa kufuatilia kila kitu hadi muda wa kushuti ni Nadia Mukami. Ukichelewa hataki mambo kama hayo mtazenguana na unajua sasa sisi Wapwani tunavyojivutaga.

Kuna wimbo God Did, kidogo nidhani umemwibia DJ Khaleed kauli?

Hapana, ni wimbo unaozungumzia maisha yangu, nilipoanzia, watu walikuwa hawaniamini nilipokuwa mtaani lakini Mungu ni nani.

Zile stori za kuwepo na bifu kati yako na Otile Brown?

Hapana hatuna bifu tumeshafanya hadi ngoma pamoja. Sijui kwanini inadaiwa kuna bifu ila sioni kama nina noma naye tuko vizuri. Najua kulikuwa na vitu kama hivyo lakini sina noma naye.

Pia kulikuwa na madai uligoma kumlipa mbunifu mavazii fulani?

Aaah! Melina Gold, sema hatukuelewana bei ila ni ishu tuliyoimaliza zamani sana. Wajua Melina naye ana bei zingine zinaweza kukuchanganya akili kwa hiyo ndio ilikuwa ishu. Nilisaka huduma zake kwa ajili ya video fulani halafu tukashindana bei kidogo ila tulishatatua.

Una kazi umechelewa kuachia?

Eeh! Kuna kazi nilifanya naye nani yule wa Bongo, Nandy. Naye kaichelewesha kuitoa hadi inaniboesha.

Una mipango gani kwa sasa?

Kuendelea kuachia muziki tu ila kwa sasa nitakuwa naachia kwa kulingana na mudi ya mashabiki.

  • Tags

You can share this post!

‘Mhubiri’ Paul Mackenzie kuendelea kuzuiliwa...

Ugonjwa wa Covid-19 si tena janga la dharura kimataifa...

T L