• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Kituo cha kwanza kuchajia magari ya umeme Nakuru

Kituo cha kwanza kuchajia magari ya umeme Nakuru

NA MERCY KOSKEI

MAGARI yanayotumia nguvu za umeme yanaendelea kupata umaarufu nchini Kenya kwani madereva wengi katika miji tofauti wamekumbatia mfumo huo wa teknolojia usiotumia petroli.

Katika mji wa Nakuru, stesheni ya kuchajia magari na pikipiki za umeme imezinduliwa katika majengo ya maduka ya Westside Mall.

Stesheni hii itawafaa wamiliki wa magari ya umeme hasa wale wanaopitia mji wa Nakuru wakielekea sehemu tofauti tofauti kwani ni jiji ambalo liko kwenye ukanda wa Kaskazini.

Taifa leo Dijitali ilizuru kituo hicho na kutangamana na mfanyakazi mmoja, Bw Abraham Keter ambaye alifichua kuwa stesheni hiyo ilifunguliwa wiki mbili zilizopita.

Hata hivyo, Bw Keter alibainisha kuwa bado kituo hicho hakijapata umaarufu kwani madereva wengi mjini Nakuru wangali wanaendesha magari yanayotumia mafuta.

“Kufikia sasa ni magari mawilipekee yamechajiwa hapa. Madereva hao walikuwa wakisafiri kutoka jiji la Nairobi wakielekea Kisumu. Hakuna mkaazi wa Nakuru ambaye ameleta gari lake hapa, bado halijapata umaurufu Nakuru,” Keter akasema.

Alidokeza kuwa, kwa sasa kituo hicho kinatoa huduma bila malipo ili kuvutia wateja akiongeza kwamba hali hiyo huenda ikabadilika wakati wowote.

Kulingana na Keter, malipo ambayo madereva wanagharamika kwa sasa ni ada ya maegesho ambayo inasimamiwa na taasisi tofauti ndani ya maduka ya Westside Mall.

Keter alieleza kuwa kuchaji gari moja huchukua angalau masaa matatu.

Joseph Kemboi, mkaazi wa Nakuru, alisikitika kuwa wengi hawaelewi jinsi kituo hicho kinavyofanya kazi, kwani wengi hawajaona gari la umeme.

Hata hivyo, alipongeza  matumizi ya magari ya umeme akisema kuwa teknolojia hii itasaidia kupunguza uachiliaji hewa ya ukaa na hivyo kusaidia kukabiliana na tishio la mabadiliko ya tabianchi (climate change).

  • Tags

You can share this post!

Gaucho: Uhuru hajaninunulia gari

Gaucho amlilia Uhuru Kenyatta amjengee nyumba

T L