• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:20 PM
KINA CHA FIKIRA: Elimu bila nasaha kwa wanafunzi ni bomu angamizi

KINA CHA FIKIRA: Elimu bila nasaha kwa wanafunzi ni bomu angamizi

Na WALLAH BIN WALLAH

BAADA ya udadisi wangu kutokana na tajriba ya miaka mingi katika taaluma ya ualimu kwa wasomi wa viwango mbalimbali madarasani, vitabuni, magazetini, redioni, runingani na mitandaoni, leo katika makala haya nimekuja kivingine vingine wasemavyo waswahili wa Manzese Darisalama Tanzania!

Kilichonichochea kuja kivingine vingine ni jinsi ninavyoona vituko vya wanafunzi wetu wa shule za sekondari wakikosa nidhamu na mwelekeo maishani hadi wanazua tabia za kutisha za kuchomachoma mabweni, maabara na ofisi za walimu wao shuleni!

Wakati mwingine wanafunzi hujijasirisha kujipa likizo na kuthubutu kuondoka shuleni kujiendea majumbani kwao bila ridhaa wala idhini za wakuu wanaopaswa kuwapa vibali na kanuni za kufuata shuleni!

Na wanapofanya vituko hivyo hudai na kujidai kwamba wamechoka kukaa shuleni!

Je, kinachowachosha na kuwasinya wasikae shuleni kwa muda waliopangiwa kusoma ni nini?

Sisi sote tunajua kwamba vijana wetu ambao ni wanafunzi wetu huenda shuleni kusoma!

Lakini hata kama ni kusoma, ndiyo wasome tu kila siku usiku na mchana kuanzia mwanzo wa muhula mpaka mwisho wa muhula bila buraha? Hilo ndilo swali!!

Ninajua kwamba watu wenye majibu ya haraka haraka watasema ati shuleni kuna michezo kidogo kidogo na burudani kama nyimbo, mashairi, ngoma, mijadala na maigizo.

Vyote hivyo vipo japo mara moja moja tu! Lakini shughuli kubwa shuleni ni kusoma na kusoma na kusoma huku kila mwalimu akiwania na kulilia kukamilisha silabasi!

Naomba tujiulize na kuwauliza walimu wetu wanaowajibika kuwafunza wanafunzi wetu, ‘Pindi mnapoingia madarasani kujaliza elimu ndani ya vichwa vya wanafunzi hawa, pia huwa mnapata mwanya japo kidogo kuwapa mawaidha na nasaha kuhusu mielekeo ya maisha na umuhimu wa kuishi kwa nidhamu na uadilifu?’

Je, mnajua kwamba gurudumu la gari likijazwa hewa zaidi na zaidi kila wakati kupita kiasi hupasuka?

Mnaelewa kwamba gunia likishindiliwa mahindi kupita kiasi huraruka na mahindi yote humwagika?

Ndugu wapenzi, tunapojaza na kujaliza masomo tu ndani ya vichwa vya wanafunzi wetu kila siku bila ya kuwapa mawaidha mazuri, nasaha na ushauri wa kujenga utu wao, tutarajie nini au matokeo gani?

Kama elimu ni mwangaza, tujue mawaidha ni busara!

Tafadhali tuwape wanafunzi wetu ushauri mwema na maneno mazuri yanayojenga fikra zao ili wajielewe na kuelewa maana na umuhimu wa elimu kuliko mihemko ya kupapia kusoma sana kukamilisha silabasi bila kutoa maelezo na maelekezo ya kuwajibika maishani.

Nasaha ndiyo dira ya malezi katika jamii! Tuwashauri wanafunzi wetu kila mara badala ya kuwajalizia elimu pekee vichwani!!!!!

You can share this post!

CRA yashauri kaunti kutengewa Sh370b mwaka 2022

Kinaya kandarasi za EACC zikitiliwa shaka

T L