• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 9:50 AM
Fahamu chimbuko la Kiunga, mji wa Lamu Mashariki wenye historia ya zaidi ya miaka 1,000

Fahamu chimbuko la Kiunga, mji wa Lamu Mashariki wenye historia ya zaidi ya miaka 1,000

NA KALUME KAZUNGU

KWA anayeifahamu Lamu, Kiunga ni miongoni mwa miji maarufu ya jadi na ya asili inayotambulika hasa kwa shughuli za uvuvi.

Mja anaposikia neno ‘Kiunga’ mara nyingi fikra zake hukimbilia suala la muunganiko, iwe ni wa watu, pande mbili au mahali pamoja na kwingine.

Mji wa Kiunga wa Lamu hupatikana karibu na mpaka wa Kenya na Somalia.

Kwa mujibu wa kamusi aidha, Kiunga lina maelezo au maana zaidi ya moja.

Kwanza, Kiunga ni eneo au mahali nje ya mji.

Pili, Kiunga limeelezwa kuwa shamba lenye miti mbalimbali ya matunda.

Tatu, Kiunga ni samaki anayefanana na pono mwenye rangi nyekundu na kijivu tumboni na nyekundu na kahawia mgongoni.

Je, maelezo haya yote ni sawa au ni yenye kushabihiana na Kiunga ya Lamu?

Taifa Jumapili ilizama chini kuchanganua na kuchambua chimbuko au asili ya mji wa Kiunga na kwa nini hasa waja wakaafikia eneo hilo kuitwa Kiunga.

Kulingana na mwanahistoria na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu, Mohamed Mbwana Shee, Kiunga ni mji wa zamani ambao jina la asili ni Mwana-Mchama (Mwana-Mtama).

Mohamed Mbwana Shee ambaye ni Mwanahistoria na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu. Pia yeye ni Mwanaharakati wa Muungano wa Shungwaya Welfare Association ambao hutetea sana haki za jamii ya Wabajuni wa chimbuko la Kiunga, Lamu Mashariki. PICHA | KALUME KAZUNGU

Wakazi kindakindaki wa mji wa Mwana-Mchama ni Wabajuni, zamani wakiitwa Washungwaya.

Zaidi ya miaka 1,200 iliyopita, Wabajuni walivamiwa na Wagalla katika vita vikali ambavyo walishindwa, hivyo kuondokea eneo lao la Mwana-Mchama na kutorokea maeneo ya visiwani, hasa Myabogi inayopatikana Faza, Lamu Mashariki.

Miaka michache baada ya Wabajuni kuondoka Mwana-Mchama, Wagalla, ambao ndio walioshinda vita hivyo, waliafikia kuondokea eneo hilo, hivyo kuwapa fursa nyingine tena Wabajuni kurudia mji wao wa asili.

Hapo ndipo jamii ya Wabajuni ambayo ilikuwa imetapakaa sehemu mbalimbali za visiwa vya Lamu ilipoanza kuitana na kukusanyika tena Mwana-Mchama na kubuni mji mpya ambao sasa unaitwa Kiunga.

Ikumbukwe kuwa kitega uchumi cha jadi cha jamii hiyo ni ukulima na pia ufugaji kwani waliweza kuendeleza biashara ya ngozi, hasa kati ya Kenya na mataifa ya nje.

Kushindwa kwa Wabajuni na Wagalla kuliisukuma jamii hiyo kukosa kuendeleza shughuli zao za kilimo kwani walikokimbilia kulikuwa ni visiwa tu.

“Hilo lilitunyima fursa ya kuendeleza ukulima na ufugaji. Visiwa havikuweza kukimu kilimo au ufugaji isipokuwa uvuvi tu. Baada ya Wagalla kuondoka eneo la Mwana-Mchama ambalo lilikuwa nchi kavu au barani, ndipo tukaafikia kuitana na kubuni mji mpya. Tendo hilo la kuitana sisi Wabajuni na kukutana au kuungana tena mahali pamoja ndipo tukapaita mahali hapo Kiunga kwani palituunganisha upya,” akasema Bw Mbwana.

Naye mzee wa Lamu na mwenye asili ya Kiunga, Bw Said Seif, alieleza asili ya Kiunga kuwa eneo au mahali nje ya mji, sawasawa na inavyoelezwa katika kamusi.

Kulingana na Bw Seif, Mwana-Mchama, ambao ndio ulikuwa mji mkuu na asilia wa Wabajuni kwa sasa umesalia kuwa magofu tu.

Wazee wa Kiunga, Said Seif (kushoto) na Muhashiam Famau wakati wa majadiliano kuhusu historia ya mji wao wa Kiunga ulioko Lamu Mashariki. Mji huo ambao watu wake wa asili ni Wabajuni una historia ya Zaidi ya miaka 1,200. PICHA | KALUME KAZUNGU

Anasema mji wa sasa wa Kiunga ni mpya na ni mtaa tu ulioko nje ukilinganishwa na mji wa jadi wa Mwana-Mchama.

“Kiunga ya sasa ni mtaa au mji mpya tu uliobuniwa nje ya Mwana-Mchama. Tukiwa ndani ya magofu ya Mwana-Mchama, tunaiona Kiunga kuwa mji ulioko kule, nje kabisa.  Yaani ni mahali nje ya mji wetu wa jadi wa Mwana-Mchama ambao tulitoroshwa wakati wa vita vya Wagalla zaidi ya miaka 1,000 iliyopita,” akaeleza Bw Seif.

Baada ya mji mpya wa Kiunga kubuniwa na kukita mizizi, mkoko ulialika maua kwani masaibu ya Wabajuni yalijirudia na kuendelea tena hadi kusheheni kabisa eneo hilo si haba.

Punde Kenya ilipopata uhuru mnamo 1963, kundi la waasi wa Kisomali lililojulikana kama ‘Shifta’ lilianza kuhangaisha eneo zima la Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

Tarehe 14 Julai, 1964, Wabajuni wa Kiunga wakavamiwa na magaidi hao wa Shifta kwani vita vya majangili hao tayari vilikuwa vimekithiri kwenye eneo hilo la Ukanda wa Kaskazini Mashariki mwa Kenya, hasa kati ya mwaka 1963 na 1967.

Ni kutokana na uvamizi huo ambapo miji karibu 40 ya Wabajuni wa asili ya Kiunga ilivunjika au kusambaratika kabisa.

Bw Muhashima Famau, ambaye pia ni mzee wa Lamu anasema serikali ya Kenya iliingilia kati na kutumia polisi wa kutuliza ghasia (GSU) kukabiliana na magaidi wa Shifta, ambapo jamii ya Wabajuni ililazimishwa kuhama makwao ilhali nyumba na mali ikiharibiwa kabisa.

Miongoni mwa miji asili na tajika ya Wabajuni iliyosambaratika ni Kiunga, Ishakani, Mwambore, Rubu, Simambae (Sendeni), Mvundeni, Ashuwei, Stesheni, Mkokoni, Matironi, Itembee, Mwadhi, Kiduruni, Vitingoni, Kiangwe, Ndununi, Mararani, Mangai, Basuba, Milimani, Baure na Bodhei, yote ikipatikana Lamu Mashariki.

Miji ya Wabajuni ya Lamu Magharibi iliyosambaratika kutokana na vita vya Shifta wakati huo ni Kililana, Mashunduani, Bar’goni, Mokowe, Koreni, Mkunumbi, Ndambwe, Mapenya, Dide Waride, Witu, Chalaluma, Moa, Sendemke, Kibokoni, Pandanguo, Kiongwe, Kipini na Katsaka Kairu.

Ni kifuatia hali hiyo ambapo Wabajuni wa Kiunga walitawanyika karibu eneo zima la Lamu, Pwani na Afrika Mashariki.

Kuna wale waliotoka Kiunga na Ishakani na kutorokea kuishi nchi jirani ya Somalia.

Wengine wengi zaidi walielekea kuishi visiwa vya Faza na Pate, ambapo walibuni miji inayotambulika leo kama Shanga, Shanga-Ishakani, Shanga-Rubu na Mtangawanda.

Pia kuna wale waliohamia kisiwa cha Lamu (Amu) ilhali wengine wakibuni makao kisiwa cha Manda hadi wa leo.

Kuna Wabajuni wengine wa asili ya Lamu-Kiunga ambao walihamia miji ya Ngomeni, Watamu, na Malindi, yote ikiwa Kaunti ya Kilifi.

Pia kuna waliohamia kuishi Mombasa.

Kundi lingine la Wabajuni wa asili ya Kiunga lilihamia eneo la Muheza huko Tanga, Tanzania ilhali wengine wakiishia Zanzibar na pia Uganda.

Kwa mujibu wa wazee wa Lamu, Wabajuni wao hujichukulia kuwa wakimbizi wa kwanza kabisa wa ndani kwa ndani (IDPs) nchini Kenya na eneo zima la Ukanda wa Afrika Mashariki, chimbuko lao likiwa ni mji wa Kiunga.

Ombi lao ni kwamba serikali iwazingatie kwa kutafuta mwafaka utakaohakikisha Wabajuni wote wa asili ya Kiunga wanakusanywa na kusaidiwa kurejea makwao ili kuendeleza vijiji vyao vilivyosambaratika.

Wasiwasi wao ni kwamba ikiwa hali itaendelea hivyo, huenda jamii ya Wabajuni ikose kabisa uhalisia wao.

Kupitia Muungano wa Shungwaya Welfare Association, ambao unatambulika kuwa mama wa Wabajuni na unaoongozwa na Bw Mbwana, juhudi tayari zinaendelea kuisukuma serikali kuifidia jamii hiyo na pia Wabajuni kusaidiwa kurejelea makazi yao ya jadi.

 “Twamshukuru mzee wetu na mwanaharakati, Mohamed Mbwana Shee na wengineo kwa kuendeleza shinikizo za serikali kutufidia sisi Wabajuni wa Kiunga. Sisi ndio wakimbizi wa kwanza wa ndani kwa ndani hapa nchini na Afrika Mashariki. Inahuzunisha kwamba hadi sasa serikali haijasikia kilio chetu. Twataka fidia kutokana na madhila tuliyokumbana nayo wakati wa vita vya Shifta. Isitoshe, serikali itusaidie kutusafirisha na kuturudisha eneo letu la Kiunga. Punde hilo likitendeka, Wabajuni pia watajihisi na kujivunia kuwa Wakenya kama wengine,” akasema Bw Famau.

  • Tags

You can share this post!

Hatimaye Wapokomo wapata toleo la Biblia kwa lugha yao

Wakazi Tana River walalamikia kaunti kutafuna pesa za umma

T L