• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 6:07 PM
NiE: Mkataba wa NMG na KIWASCO unavyopiga jeki elimu Kisumu

NiE: Mkataba wa NMG na KIWASCO unavyopiga jeki elimu Kisumu

NA CHRIS ADUNGO

KAMPUNI ya kusambaza maji na kushughulikia usafi ya kule Kisumu, KIWASCO ilishirikiana na shirika la Nation Media Group kufadhili shule kadhaa za Kaunti ya Kisumu katika mradi wa Newspapers in Education (NiE).

Mradi huo wa NiE unahusisha matumizi ya magazeti kuchangia kuimarisha uraibu wa kusoma na kuchangia kuboresha matokeo ya shule kwenye mitihani ya kitaifa.

Kampuni hiyo inafanya ufadhili kwa mwaka wa pili mfululizo. Mwaka uliopita wa 2022, ufadhili huo ulishirikisha shule tano ambazo zilikuwa Kindu Primary, Kianja Primary, Ong’adi Primary, AIC Obwolo na Okok Mixed Secondary.

Shule hizo zilipata ufanisi mkubwa katika matokeo ya mtihani wa kitaifa. Mfano, shule ya Kindu Primary iliimarika katika Kiswahili kutoka alama wastani 39.78 hadi 49.0 na Kiingereza kutoka alama 43.22 hadi 50.0. Shule ya Kianja Primary iliimarika katika Kiswahili kutoka alama 49.0 hadi 50.1 na Kiingereza kutoka 48.0 hadi 49.0. Shule ya Ong’adi iliimarika katika Kiswahili kutoka 39.22 hadi 46.0 na Kiingereza kutoka 44.6 hadi 48.1.

Mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Kindu avaa shati-tao la Taifa Leo alilotuzwa baada ya kujibu maswali ambayo gwiji Nuhu Zuberi Bakari alimuuliza kwenye hafla ya kuvumisha mradi wa Newspapers in Education (NiE) jijini Kisumu mnamo Februari 16, 2022. Kampuni ya Nation Media Group inashirikiana na Kampuni ya kusambaza maji na kushughulikia usafi ya kule Kisumu, KIWASCO kuhakikisha shule kadhaa zinapata magazeti. PICHA | TONNY OMONDI

Shule ya upili ya AIC Obwolo iliimarika katika Kiswahili kutoka 3.2 hadi 3.5 na Kiingereza kutoka 3.0 hadi 4.0. Ile ya Okok Secondary iliimarika katika Kiswahili kutoka 2.0 hadi 4.0 na Kiingereza kutoka 3.0 hadi 4.0.

Mwaka huu, KIWASCO iliongeza ufadhili kutoka shule tano hadi nane. Shule zilizoongezwa ni Obwolo Peimary, Rae Kajulu Primary na Kindu Secondary.

Mhasibu mkuu wa KIWASCO Bwana Nicholas Moseti, aliyeongoza ujumbe wa KIWASCO aliwarai wanafunzi waliofadhiliwa mwaka huu kuwaiga wenzao wa mwaka 2022.

“Wanafunzi wa mwaka jana walidhihirisha kinaganaga kuwa ufadhili tuliotoa ulistahili. Nanyi, ninawasihi muwaige au hata kuwapiku na kupata alama za juu za kuingia vyuoni na shule za upili. Hatutasita kusimama na mradi wa aina hii wa kubadilisha vizazi,” akasema Bw Moseti.

Shirika la Nation Media Group liliwakilishwa kikamilifu na Bw Clifford Machoka ambaye ni Afisa Mkuu wa Uhusiano Mwema wa NMG na Bw George Kihuria ambaye ni Mkuu wa Idara ya Usambazaji wa Magazeti ya NMG. Wengine walikuwa ni mshirikishi Danstone Bobea, mtangazaji Lofty Matambo na wakuu wa shirika hili, tawi la Kisumu.

Waliwahimiza walimu na wanafunzi wa shule hizo kuyakumbatia magazeti hayo na kuchota yaliyomo ili kuimarika kikamilifu katika mitihani ya kitaifa.

  • Tags

You can share this post!

Askari wasababisha vifo vya watu 4 wakikimbizana na...

Rosa Buyu: Marufuku ya muda kwa wabunge wa Azimio ni njama...

T L