• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 6:37 PM
Shule yapata darubini, vifaa vingine sayansi ikigeuzwa ‘somo mswaki’

Shule yapata darubini, vifaa vingine sayansi ikigeuzwa ‘somo mswaki’

NA MAUREEN ONGALA

SHULE ya Upili ya The Great Vonwald katika eneobunge la Kilifi Kaskazini inalenga kuwa kituo cha kutoa elimu ya sayansi ya sayari na unajimu kwa wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Hii ni baada ya shule hiyo kupata darubini kubwa ya kisasa inayotumia vioo na vilolo vya kisasa vilivyopinda.

Darubini hiyo ililetwa shuleni humo na wafadhili kutoka nchini Austria.

Kulingana na usimamizi wa shule hiyo, wanafunzi watapewa nafasi ya kujihusisha moja kwa moja na maswala ya mabadiliko ya tabianchi na kuchangia katika miradi ya kuangazia na kushughulikia maswala hayo shuleni na hata kwa jamii pana.

Shule hiyo ya mseto inasimamiwa na shirika moja lisilokuwa la serakali la GAPEKA Children’s Hope Centre.

Akizungumza na Taifa Jumapili, mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo Prof Gabriel Katana alisema shule hiyo inalenga kutoa mafunzo na nafasi za wanafunzi wa hata shule nyingine za upili na pia vyuo vikuu kuingia hapo kufanya utafiti wa maswala ya kisayansi.

“Swala kuu hapa ni kuwasaidia na kuwapa moyo wanafunzi wadogo kiumri wapate hamu ya kujua mambo mengi kupitia kutazama mwezi, nyota na sayari wakati wa asubuhi na mapema na usiku,” akasema.

Prof Katana alisema wanafunzi hao pamoja na jamii watakuwa katika nafasi nzuri ya kujua mengi kuhusu sayari na mambo kadhaa ambayo ni muhimu katika swala nzima la kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kulingana na Prof Katana somo la namna vioo na vilolo vilivyopinda hufanya kazi, hufundishwa katika Kidato cha Pili.

Aliendelea kusema kuwa masomo hayo ya sayari na unajimu ni muhimu sana.

Sasa wanafunzi watashuhudia wenyewe jinsi ya kusoma sayansi kwa undani kupitia kujifunza maswala ya angani.

“Hii itatusaidia kutupilia mbali kasumba na tabia ya kubagua masomo kwa madai kuwa masomo ya sayansi ni magumu,” akasema.

Kituo hicho cha kipekee kitatoa nafasi kwa wanafunzi kujua mambo ambayo yanachangia mabadiliko ya tabianchi pamoja na athari zake, ikiwemo kusoma na kutazama tabia ya nyota, miundo ya mwezi na mabadiliko ya mawimbi angani.

Prof Katana alisema kwa hayo yote, wanafunzi watapata nafsi nzuri ya kujua mapema athari za shughuli za binadamu ambazo zimechangia pakubwa madabiliko ya tabianchi na kuharibu mazingira.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Upili ya The Great Vonwald katika eneobunge la Kilifi Kaskazini Prof Gabriel Katana akiwafundisha wanafunzi wa masomo ya Fizikia na Kemia jinsi darubini inavyofanya kazi. Kifaa hicho kililetwa na wafadhili wao wa kutoka nchini Austria mnamo Novemba 16, 2022. PICHA | MAUREEN ONGALA

Baadhi ya uharibifu wa mazingira ambao umechangia pakubwa mabadiliko ya tabianchi ni pamoja na ukataji miti na uchomaji makaa kwa kiwango kikubwa ambao umesababisha hewa kuchafuka.

“Tunalenga kufanya kituo hiki kiwe ni cha kuwapa wanafunzi habari muhimu na sahihi kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kuwafanya kupenda sayansi na kuwa miongoni mwa wale ambao watasaidia kutoa suluhu kwa changamoto hizo kupitia miradi tofauti katika shule zao,” akasema.

Tayari baadhi ya shule za upili katika Kaunti ya Kilifi zimeonyesha nia ya kutaka kutembelea The Great Vonwald kuanza masomo yao ya sayansi.

Kila mwanafunzi katika shule ya upili atalipa Sh50 na wale wa vyuo vikuu watalipa Sh100.

The Great Vonwald School inaendeleza mipango pia ya kuhakikisha kuwa wanafunzi ambao wanapanga kukesha wakitazama sayari kwa siku kadhaa wanapata pahala pa kulala na chakula.

Kwa kuendelea kuafikia malengo yao katika kuimarisha na kuwafanya wanafunzi kupenda na kukumbatia sayansi, tayari baadhi ya wanafunzi wamefunzwa jinsi ya kutumia darubini hiyo na wako tayari kuwafunza wenzao.

“Shule yoyote inaweza ikawaleta wanafunzi waje kusoma kwani tayari wanafunzi wetu wako tayari kuwafundisha hao wengine jinsi ya kutumia darubini na hii itaendeleza pia mafunzo ya rika,” akasema.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bw Joseph Mwashigadi alitoa wito kwa shule katika kaunti ya Kilifi kutumia kituo hicho kuwafanya wanafunzi kupenda masomo ya sayansi.

“Wakati umefika ambapo ni lazima shule za upili zinafaa kuacha kutoa twasira ya kuwa sayansi ni ngumu kwa sababu ya uvivu wa baadhi ya walimu,” akasema.

Aliwataka wanafunzi kukumbatia masomo ya sayansi na kukoma kuwasikiliza baadhi ya watu.

“Watu wengi ambao hawakufanya vizuri katika masomo ya sayansi hueneza propaganda kuwa ni elimu mbaya na tena ni ngumu. Aliyeshindwa hawezi akaongoza mwenzake kuwa mshindi,” akasema.

Alisema ni jukumu la wanafunzi kujituma na kutambua kuwa sayansi ni bora.

Bw Mwashigadi ambaye ni mwalimu wa Fizikia na Kemia alisema kuwa atatumia darubini hiyo kuwasukuma wanafunzi kujielewa na kujua umuhimu wa sayansi na jinsi ilivyo rahisi tofauti na inavyodaiwa kuwa ni ngumu.

“Masomo ya sayansi hayahitaji mambo mengi, bora tu mwanafunzi aelewe kinachohitajika katika kile anachofanya,” akasema.

Shirika la GAPEKA linawasaidia watoto kutoka familia maskini kupata masomo ili kupigana na ujinga na umaskini katika jamii.

Hatua ya shule hiyo inawadia huku viongozi katika Kaunti ya Kilifi wakieleza kuwa idadi kubwa ya wanafunzi hakwepa masomo ya sayansi.

Pia wanafunzi wengi wanafanya vibaya katika masomo ya sayansi katika mitihani ya litaifa kwa sababu ya ukosefu wa maabara na vifaa vya kisasa katika shule zao.

Walisema hali hiyo inazidi kuwavunja moyo wanafunzi na wengi wao kuepuka masomo ya sayansi.

  • Tags

You can share this post!

Vibiritingoma waliovamia mitaani wafanya waume wengi...

Museveni adai wanaokula kuku huwa na mienendo hafifu

T L