• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 5:13 PM
Lugha kama chombo cha mawasiliano baina ya binadamu

Lugha kama chombo cha mawasiliano baina ya binadamu

NA MARY WANGARI

DHANA ya mawasiliano ni mchakato wa kuwasilisha taarifa kwa njia ya ubadilishanaji wa hisia, mawazo, matarajio, mitazamo, tabia, malengo, kupitia mazungumzo, ishara na maandishi.

Mawasiliano yanaweza kuelezwa vilevile kama ubadilishanaji wa taarifa unaoleta maana baina ya pande mbili au zaidi ambazo zinaweza kuwa viumbe hai au vinginevyo.

Kwa makusudi ya makala hii, tutadadavua kwa kina mawasiliano yanayotumia lugha kama chombo ambayo kimsingi ni baina ya binadamu.

Jinsi tunavyofahamu, lugha ni nyenzo muhimu sana katika mawasiliano ya binadamu.

Ni vigumu kukisia mawasiliano yangekuwa vipi lau hakungekuwa na lugha. Bila shaka, yangekuwa ya kuchusha na kupoteza muda mwingi huku watu wakijaribu kuelewana bila mafanikio.

Lugha ya ishara inayotumika aghalabu miongoni mwa bubu na viziwi pia inahitaji pia maarifa ya lugha hiyo yanayoeleweka baina ya wazungumzaji ili kufanikisha mawasiliano.

Isitoshe, lugha imewezesha uvumbuzi na maendeleo kisayansi na kiteknolojia ambapo tafiti na matokeo yake huweza kuwasilishwa na kuchapishwa ili kuwafikia wadau husika kwa utekelezaji.

Ni lugha pia inayowezesha binadamu kufurahia maendeleo kiteknolojia kama vile kuwasiliana kupitia jumbe za simu, kusogoa (chat) katika mitandao ya kijamii mathalan Facebook, Twitter, WhatsApp, Instagram miongoni mwa mingine.

Ni dhahiri hivyo basi kwamba umuhimu wa lugha katika kufanikisha mawasiliano miongoni mwa binadamu hauwezi ukasisitizwa vya kutosha.

Fasili ya Lugha

Wataalam anuai wameelezea dhana ya lugha kuptia mitazamo mbalimbali.

Kwa mukhtasari, lugha inaweza kufafanuliwa kama mfumo wa sauti za nasibu zilizokubaliwa na wanajamii ili zitumike katika mawasiliano na shughuli za kila siku kuelezea hisia, mahitaji, mawazo na matakwa yao.

Katika ufafanuzi huu, kuna viambajengo muhimu katika lugha vinavyojitokeza ambavyo tunaweza kufafanua jinsi ifuatavyo.

Viambajengo vya Lugha

Lugha ni mfumo – Ni muhimu kuelewa kwamba kila lugha ya binadamu imeundwa katika mifumo miwili mikuu ambayo ni: mfumo wa sauti na mfumo wa maana.

Kimsingi, lugha huundwa kwa sauti ambazo huunganishwa ili kuunda neno au sehemu ya neno, kisha maneno huungana kuunda miundo mikubwa zaidi yenye maana kama vile virai, vishazi, sentensi na aya.

[email protected]

You can share this post!

Brigid Kosgei sasa kuwa balozi wa kutangaza Stanbic Bank

Viambajengo muhimu katika lugha kama chombo cha mawasiliano