• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 5:55 PM
MALENGA WA WIKI: Nyakundi ni mshairi na mhariri wa riwaya, tamthilia

MALENGA WA WIKI: Nyakundi ni mshairi na mhariri wa riwaya, tamthilia

DUKE Nyagwoi Nyakundi almaarufu mwalimu Nyakundi alizaliwa mwaka wa 1994 eneo la Ogembo, katika Kaunti ya Kisii.

Ni mtoto wa kwanza miongoni mwa watano wa Bw Enock Ondigi na mama Margaret Nyabonyi.

Nyakundi alianza masomo yake katika shule ya Olympic Junior Academy iliyoko Rionyiego, Nyamache.

Akiwa shule za msingi na upili alipenda sana somo la Kiswahili. Hii ilitokana na walimu na walezi wake wa Kiswahili waliompa matumaini na wosia kuwa anaweza kuandika mashairi.

Walimu hao walikuwa Bw Nicodemus, marehemu Bi Justina, Bw Oseko, Bi Mellen Kennedy na Bw Moronya ambaye ni naibu mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Tendere.

Wote walijizatiti kumpa maelekezo adhimu kuhusu utamu wa lugha ya Kiswahili. Nyakundi alifanya mtihani wake wa kidato cha nne 2013 na kisha kujiunga na Chuo Kikuu cha Kisii alikosomea shahada ya ualimu.

Alijikita katika somo la Kiswahili na dini humo chuoni ambapo kuanzia mwaka wa kwanza hadi wa nne, alikuwa kiranja wa wanafunzi waliosomea lugha ya Kiswahili.

Alikuwa akitenga muda wa kukitetea Kiswahili huku akipewa maelekezo kutoka kwa wahadhiri wake ambao ni Bw Gilbert Manyura na Dkt Opande Nilson. Baada ya kumaliza masomo yake, aliajiriwa kazi ya ualimu na kufunza shule mbalimbali kama vile mtakatifu Teresa Bogiakumu, shule ya upili ya Tendere na sasa yuko shule ya upili ya Amabuko, Keroka.

Mwalimu Nyakundi alivutiwa na usanii wake Ken Walibora. Hasa alivutiwa mno na riwaya ya Siku Njema, Ndoto ya Almasi, Ndoto ya Amerika na Nasikia Sauti ya Mama.

Alipata usaidizi mkuu kutoka kwa nduguye, ustadh Kiamboni.

Safari yake ya uandishi ilianza 2019 wakati Kaka Fred alipomkubali kama mwandishi. Mnamo mwaka 2020, walichapisha diwani ya hadithi fupi iitwayo Mwamba wa Dhahabu na hadithi nyingine. Diwani hii ilimfanya kujulikana na waandishi wengine kama vile Timothy Sumba, Chris Adungo, John Wanjala, Jibril Adam, Erick Momanyi – malenga wa Lutein, Kepha Onchaga, Angira O Angira, Millie Musimbi, Francisca Wambua, Dokta Ziro na wengine wengi.

Mbali na ushairi, Nyakundi huandika hadithi. Ingawa anajiona kinda katika safari hii, kamwe hachoki kutunga shairi kila siku. Mashairi yake hujikita katika maudhui ya ukiukaji wa haki za binadamu, ufisadi, elimu na mapenzi na maswala mengine ibuka. Yeye hutumia lakabu malenga Tembo mla nyama.

Mshairi huyu ametoa mchango mkubwa katika ukuzaji wa lugha ya Kiswahili kupitia utunzi na uandishi wa vitabu kama vile: Utando wa ushairi, Karakana ya ushairi, Tasnia ya ushairi, Bohari la ushairi, Wasifu wa Timothy Sumba, Barua kwa Moyo wangu na Hadithi Nyingine, Mwamba wa Dhahabu na hadithi Nyingine, Chipuo la Isimu jamii na miswada miwili iliyo jikoni (maswali na majibu ya Mapambazuko ya Machweo, na Chipuo la Sarufi ) itakayochapishwa hivi karibuni.
Mbali na utunzi na uandishi, mwalimu Nyakundi ni mhariri wa kazi za fasihi. Yeye ni naibu mhariri wa Chama Cha Waandishi wa Kiswahili, Kenya (CHAWAKI) katika kitengo cha mashairi kinachosimamiwa na John Wanjala.

Ingawa ametunga mashairi mengi, shairi analolipenda sana ni Nisamehe Mahabuba. Shairi hili la mahaba, lilimpendeza sana mshairi Pauline Kyovi Kea mwandishi wa hadithi ya Kila Mchezea Wembe.

Shairi hilo lasema hivi;-

Emmi mpenzi wangu, pokea huu waraka

Najua una machungu, lakini nipe dakika
Kasome kila kifungu, soma ukipumzika
Nisamehe mahabuba, imenifunza dunia.

Ndoani nimeteleza, matope nimejipaka

Kwa muda nimekutweza, kwangu ‘kawa takataka
Tembo ‘kakutelekeza, hadi ndoa ikanuka
Nisamehe mahabuba, imenifunza dunia.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Naam, Ruto anafanya vyema kuzima miungano ya...

NYOTA WA WIKI: Kaoru Mitoma

T L