• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Mambo ya msingi kufahamu katika uandishi wa insha bora

Mambo ya msingi kufahamu katika uandishi wa insha bora

Na ENOCK NYARIKI

KWA mara ya kwanza kabisa, mitihani ya Kidato cha Nne na Darasa la Nane ambayo hufanywa katika mwezi wa Kumi na Kumi na mmoja, itafanywa Machi mwaka huu. Kutoka sasa hadi mwezi wa Machi zimesalia siku idadi za kubukua. Kubukua kwa maana mbili muhimu.

Kwanza, kusoma kwa bidii hususan mtihani unapokaribia. Pili na muhimu sana kwa mujibu wa makala haya, ni kusoma kwa makini. Kile ambacho watahiniwa wanahitaji zaidi wakati huu ni kusoma kwa makini na kwa mazingatio.

Katika makala haya, nitayaangazia mambo ya msingi kuhusu uandishi wa insha ambayo wanafunzi wanapaswa kuyamakinikia wanapoendelea kujiandaa kwa mitihani yao.

Insha ni sehemu muhimu sana katika somo la Kiswahili maadamu huchangia asilimia arubaini ya jumla ya alama. Wanafunzi wengi hupata alama za wastani katika somo la Kiswahili kwa sababu ya kupata alama duni au za wastani katika karatasi ya insha.

Baadhi ya mambo ambayo huchangia alama duni katika insha ni ya msingi mno na yanaweza kuepukwa na watahiniwa iwapo wataanza kuyamakinikia kuanzia sasa.Nimeyaita mambo hayo ya msingi kwa sababu mbili kuu.

Kwanza, ni mambo ambayo wanafunzi wanayafahamu kwa sababu walimu wao huyasisitiza wakati baada ya mwingine. Hata hivyo, inawezekana kwamba baadhi ya wanafunzi huyapuuza au kuyasahau.

Pili, ijapokuwa baadhi ya vipengele hivyo havituzwi alama au hutuzwa alama chache mno wakati wa usahihishaji, ni muhimu katika kuvutia usahihishaji wenyewe.

Hati au maandishi kwa mfano huchangia pakubwa takribani alama zote anazotuzwa mtahiniwa katika insha ingawa ukichunguza kwa makini usahihishaji wa insha, alama anazotuzwa mwanafunzi kwa sababu ya kuandika kwa hati bora hazizidi mbili.

Hati au maandishi ni muhimu kwa sababu huteka mawazo ya mtahini na kumfanya aendelee kuisoma insha mpaka mwisho wake. Kuyatafuta mawazo mazuri katika insha yenye hati au maandishi mabaya ni sawa na kukitafuta kito au kitu cha thamani kwenye rundo la vitu vingine ambavyo si vya thamani.

Anayetafuta kito chenyewe huenda asiumakinikie utafutaji hasa pale ambapo hana hakika kuwa kinachotafutwa kimo miongoni mwa vitu hivyo. Kwa hivyo, insha ya mwanafunzi inaweza kulenga mada, ikawa na mtiririko unaofaa na kubeba mawazo mazito lakini iwapo maandishi yake ni mfano wa makosi ya mpiga ramli, huenda kwa bahati mbaya akaishia kupata alama zisizoridhisha.

Ni muhimu watahiniwa kwa msaada wa walimu wao kuyapiga msasa maandishi yao. Kwamba hati nzuri inapaswa kufunzwa katika madarasa ya chini ni kasumba ambayo watahiniwa na walimu wao wanapaswa kuiepuka. Iwapo hati haikuwekewa msingi katika madarasa ya chini, bado upo muda wa kuirekebisha katika madarasa ya juu.

Maandishi

Maandishi bora ni dhana inayokumbatia mambo mbalimbali muhimu ila tutayaangazia machache. Kwanza ni uchongaji mzuri na uimarishaji wa baadhi ya herufi ambazo huandikwa zikiwa zimeegemea upande; kuzitomelea zile zinazohitaji kutomelewa kwa mfano ‘i’ na kuweka vijistari vya mlalo kwenye herufi kama vile ‘t’ na ‘T’; kutofautisha baina ya herufi ndogo na kubwa n.k.

Pili, kutenga nafasi ya kutosha baina ya maneno kwenye msitari mmoja. Tatu, kutenga nafasi ya kutosha katika aya. Jambo jingine muhimu kuhusu hati au maandishi na ambalo ni muhimu sana ni unadhifu.

Watahiniwa wajiepushe kufutafuta kazi zao hasa wale wanaotumia wino kuandika insha. Linapotokea kosa ambalo halikukusudiwa, sharti mwanafunzi alirekebishe kwa kupiga kijistari kimoja cha mlalo juu ya neno ambalo linapaswa kufutwa kwa kutumia rula.

Epuka ‘kuisuguasugua’ kazi yako kwa sababu jambo hilo litaifanya kutopendeza.Jambo jingine la msingi kuhusu uandishi wa insha ni kuyadariji au kuyapanga mawazo kabla ya kuanza kuandika.

Nimelitumia neno ‘mawazo’ hapa kwa maana mbili kuu. Kwanza, kujiandaa kisaikolojia kabla ya kuanza kuandika ili kukabili shauku ambayo aghalabu huwakumba wanafunzi wote wanapokabiliana na karatasi yoyote kwa mara ya kwanza. Shauku hiyo na pupa ya kuandika hakika huwa chanzo kimojawapo cha kutozingatiwa kwa unadhifu wakati wa kuandika.

Nitaiangazia hoja hii kwa kina katika makala kuhusu namna ya kukabili kizuizi cha uandishi katika uandishi wa insha. Pili, mawazo ni jumla ya hoja zinazohitajiwa wakati wa kuandika insha au mpangilio maalumu katika uandishi wa insha. Ijapokuwa kila insha huhitaji mpangilio maalumu, neno hili katika muktadha huu limelenga insha za masimulizi.

Mkakati kabambe kuhusu namna ya kuanza na kumalizia insha ya masimulizi ni muhimu sana. Kutokuwa na mkakati kama huo ni chanzo cha miisho hafifu ya insha.

MAKALA YATAENDELEA…

You can share this post!

Serikali yaanza operesheni ya kuzima ujangili Kapedo

NDIO! HAPA WIZI TU