• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 9:50 AM
Maonyesho ya kahawa yaliyoleta pamoja zaidi ya wakulima 2,000

Maonyesho ya kahawa yaliyoleta pamoja zaidi ya wakulima 2,000

Na SAMMY WAWERU

UZALISHAJI wa kahawa nchini unaendelea kushuka licha ya serikali na wadauhusika kuweka mikakati maalum kuokoa sekta hii ambayo miaka ya awali iliiweka Kenya katika taswira ya ulimwengu.

Kulingana na takwimu za hivi punde, kiwango cha uzalishaji kwa sasa kinasimamia tani 36, 000 (uzani wa metric tons) kwa mwaka, chini kutoka tani 140, 000 (metric tons) kiwango kilichokuwa kikishuhudiwa miaka 20 na 30 iliyopita.

Data hizo za 2020/2021, zilifichuliwa katika Maonyesho ya Kitaifa ya Kahawa mwaka huu, Makala ya Nne, yaliyofanyika katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Mimea na Uimarishaji Mifugo (Kalro), kitengo cha Utafiti chenye makao yake makuu Ruiru, Kaunti ya Kiambu

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Meneja Mkuu wa New Kenya Planters Co-operative Union (KPCU), Timothy Mirugi, alisikitikia hatua ya wakulima wa kahawa kugeuza mashamba yao kuwa majengo na nyumba za kupangisha.

“Kiwango cha uzalishaji wa kahawa nchini kimeshuka kikilinganishwa na miaka 20 na 30 iliyopita,” Mirugi akasema. Wakulima wengi wameng’oa miti na misitu ya kahawa, ili kuwekeza katika miradi mingine ya maendeleo yenye mapato ya kuridhisha.

Bw Simon Kamau (aliyeshika maski), mkulima wa kahawa Kigumo, Kaunti ya Murang’a…Picha/SAMMY WAWERU

Upungufu wa uzalishaji Kenya, kulingana na afisa huyo umechangiwa na uongozi mbaya katika sekta ya kahawa uliokuwa ukishuhudiwa chini ya utawala wa KPCU ya kitambo kabla Rais Uhuru Kenyatta 2019 afanye mageuzi.

KPCU mpya ilibuniwa ili kuokoa wakulima, ambapo ilitwikwa majukumu ya kusaga kahawa na kuitafutia soko ndani na nje ya nchi. Waziri wa Kilimo, Peter Munya pia amekuwa akifanya mabadiliko, Mirugi akipongeza hatua hiyo katika kuleta afueni kwa wakulima.

Alisema New KPCU ambayo kwa sasa inafanya kazi na zaidi ya wakulima 50, 000 wa kahawa kote nchini, inawatafutia wateja wa moja kwa moja. Aidha, Mirugi alisema taasisi hiyo ya serikali inakabiliana na mabroka ili kuboresha soko la kimataifa.

Kabla mazao kuuzwa, wakulima wanashauriwa ikiwa wanaridhia bei iliyotajwa na madalali. Mikakati ya New KPCU pia imepiga marufuku uuzaji wa mazao ya kahawa kwa deni.

“Uwazi umeanza kushuhudiwa ambapo wakulima lazima wawe wakati wa kupima mazao yao na kusaga,” Mirugi akasisitiza. Hata ingawa serikali inatoa mikopo kwa wakulima wa kahawa isiyotozwa riba, afisa huyo analalamika wanachelea kuichukua.

Kwa jumla ya Sh3 bilioni, zilizotengewa New KPCU kama mkopo kwa wakulima, Sh151 milioni pekee ndizo zimesambazwa chini ya kipindi cha miezi sita iliyopita. “Wakulima wengi hawafahamu watakavyopata mkopo huo,” Mirugi akasema.

Dkt Elijah Gichuru, Mkurugenzi Mkuu Coffee Research Institute – Kalro na Mkurugunzi Mkuu Pest Control Products Board, Dkt Esther Kimani katika shamba la kahawa wakati wa maonyesho ya kahawa 2022 makala ya nne Ruiru, Kiambu…Picha/SAMMY WAWERU

Shirika hilo hata hivyo linawahamasisha kupitia viwanda vya kahawa na vyama vya ushirika (Sacco), likiwahimiza kuikumbatia kuboresha kilimo cha zao la kahawa. Mazao wanayouza ndiyo yanasimamia mikopo wanayochukua, na ada ya asilimia 3 pekee kutozwa.

Huku mashamba mengi yakitumika kuendeleza miradi mingine ya maendeleo, Kenya ina karibu Hekari 117, 000 (kipimo cha Ha) zinazokuzwa kahawa. Coffee Directorate, taasisi ya serikali ambayo pia ilitumia maonyesho ya kahawa 2022 kuonyesha bidhaa inazosindika kutoka kwa kahawa, pia ilizua wasiwasi kuhusu kushuka kwa kiwango cha uzalishaji.

Serikali ikiendelea na mikakati kufufua sekta ya kahawa nchini, Dkt Benson Apuoyo, Naibu Mkurugenzi anayesimamia Utafiti wa Mauzo na Uboreshaji Bidhaa, alieleza matumaini yake Mswada ulioko bungeni unaopendekeza taasisi hiyo kubadilishwa kuwa Bodi ya Kahawa Kenya utazaa matunda.

Afisa huyo alisema, bodi itasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha sekta ya kahawa nchini. “Tunafanya hamasisho la unywaji wa kahawa nchini,” Dkt Apuoyo akadokeza.

Alifichua kuwa vituo viwili vimezinduliwa katika Chuo Kikuu cha Egerton na Kenyatta (KU), vinavyolenga vijana katika uhamasishaji wa matumizi ya kahawa nchinini. Kenya huuza asilimia 95 ya kahawa katika masoko ya kimataifa, hii ikiashiria kuwa asilimia 5 pekee ya zao hilo ndiyo hutumika nchini.

Maonyesho ya kahawa 2022, Ruiru Coffee Fair and National Coffee Conference, yalihudhuriwa na zaidi ya wakulima 2, 000 kutoka sehemu mbalimbali za nchi. Karibu kampuni 45 na viwanda vinavyotengeneza pembejeo za kahawa, mashine na vifaa, zilishiriki.

Damaris Mutindi, afisa anayeshughulikia mauzo Agribase Bioscience International Ltd, wakati wa maonyesho ya kahawa Ruiru, Kiambu…Picha/ SAMMY WAWERU.

Wakulima walitumia jukwaa hilo kulalamikia bei ghali ya fatalaiza. “Tumeona jitihada nyingi zinalenga kuboresha soko, japo mapato yote yanaishia kwa mbolea,” akateta Simon Kamau.

Kamau, 30, ana mikahawa 250 eneo la Kigumo, Kaunti ya Murang’a. Mfuko wa kilo 50 wa fatalaiza umepanda kutoka Sh2, 500 hadi zaidi ya Sh6, 000. Wangegi Ngathu, mkulima Kiambu anayekuza mikahawa 1, 300 alisema mfumko huo wa bei unatishia kilimo cha kahawa nchini.

“Wakulima wengi nchini wanatumia pembejeo zetu kadha. Tunahimiza serikali ifanye hima kushusha gharama ya pembejeo na bidhaa za kilimo,” akasema Nelson Maina, Mkuu wa Mauzo, Elgon Kenya, kauli iliyotiliwa mkazo na Damaris Mutindi, afisa anayeshughulikia mauzo Agribase Bioscience International Ltd.

Ushuru wa juu unaotozwa pembejeo za kilimo, malighafi pamoja na janga la Covid-19 umechangia ongezeko la bei. Ni hali inayoshuhudiwa karibu kila pembe ya ulimwengu, virusi vya corona vikitajwa kuchangia kwa kiasi kikuu.

Aidha, sekta ya kilimo kwa jumla imeathirika. Mabadiliko ya tabianchi (climate change) vilevile yamechangia kushuka kwa kiwango cha uzalishaji wa kahawa nchini.

Katika maonyesho ya mwaka huu, Taasisi ya Utafiti wa Kahawa – Kalro ilisema inafanya kila iwezalo kuibuka na mimea na mbegu zitakazostahimili athari za mabadiliko ya hali ya anga.

“Mikakati hiyo inajumuisha mikahawa itakayostahimili changamoto za magonjwa na wadudu, mimea iliyoimairishwa (tissue culture na kupandikiza miche na mikahawa shambani,” akaelezea Dkt Elijah Gichuru, Mkurugenzi Mkuu.

Naye Dkt Esther Kimani, Afisa Mkuu Mtendaji Pest Control Products Board, alihimiza wakulima kuwa makini kwa dawa wanazotumia kukabiliana na kero ya magonjwa na wadudu. Akisisitiza kuhusu uboreshaji wa kahawa nchini, Dkt Esther alisema wakulima wanapaswa kukumbatia dawa salama, kama vile zile hai na mifumo ya teknolojia ya kisasa.

“Lazima tuwe makini na chakula chetu,” akasema, akiongeza kuwa bodi anayosimamia i kipau mbele kupiga msasa viwanda vya kuunda dawa na maduka ya pembejeo kupitia usajili na utoaji leseni.

Kufuatia mikakati na sheria za Bodi hiyo ya Kudhibiti Matumizi ya Dawa Dhidi ya Wadudu, Dkt Esther alidokeza kwamba kufikia sasa visa 10 vya utengenezaji na uuzaji wa dawa bandia na ghushi vimeandikishwa na wahusika kufikishwa kortini.

“Tunafanya kazi kwa karibu na kushirikiana na Idara ya Uchunguzi wa Jinai na Uhalifu – DCI.” Wakulima waliohudhuria maonyesho hayo ya kahawa, walishauriwa kuwa na mazoea ya kupima kiwango cha asidi na alkali (pH) cha mashamba yao, Sophie Mwaniki, kutoka Crop Nutrition Laboratory Services akisema hatua hiyo itawasaidia kujua rutuba inayohitajika kuboresha mazao.

Waziri wa Kilimo, Ufugaji na Samaki Kiambu, CEC, Joseph Kamau pia alihudhuria akiahidi kuwa serikali ya kaunti hiyo imeweka mikakati bulibuli kupiga jeki ukuzaji wa kahawa Kiambu.

Maonyesho hayo yaliandaliwa na kufadhiliwa na BASF, kwa ushirikiano na Kenya Coffee Platform na Nation Media Group.

Bw Nelson Maina, Mkuu wa Mauzo, Elgon Kenya wakati wa maonyesho ya kahawa Ruiru, Kiambu…Picha/ SAMMY WAWERU.

You can share this post!

Aubameyang aongoza Barcelona kuzamisha Bilbao katika La Liga

MCA asikitishwa na wakulima kuendelea kuasi kahawa

T L