• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
MAPISHI KIKWETU: Sambusa za kuku

MAPISHI KIKWETU: Sambusa za kuku

NA MARGARET MAINA

[email protected]

SAMBUSA ya kuku kwa kawaida huwa na mchanganyiko wa viungo na huwa na ladha ya kipekee.

Unaweza kutumia mchanganyiko wa nyama iliyoyosagwa ya kuku, mboga mboga, na viungo kama vile zaatari, kari, na pilipili.

Muda wa kuandaa: Dakika 20

Muda wa mapishi: Dakika 20

Walaji: 3

Vinavyohitajika

Kwa kinyunya

  • vikombe 2 vya unga wa ngano
  • vijiko 4 vya mafuta
  • vijiko 8 vya maji
  • chumvi ½ kijiko

Kwa kujaza

  • mafuta kijiko 1
  • kitunguu maji 1 kilichokatwa vizuri
  • punje 2 za vitunguu saumu; pondaponda
  • kilo 1 ya nyama ya kuku iliyosagwa
  • viazi 2; kata vipandevipande
  • njegere ½ kikombe
  • ½ ya kijiko kidogo cha tangawizi iliyokunwa
  • ½ ya kijiko cha paprika
  • ½ kijiko cha zaatari
  • ½ kijiko cha poda ya kari
  • chumvi
  • ½ ya kijiko cha pilipili nyeusi
  • pilipili
  • majani ya giligilani
  • mafuta ya kutosha kwa kukaanga

Maelekezo

Kuandaa kinyunya

Changanya unga, chumvi, na mafuta kwenye bakuli kubwa, na tumia vidole vyako kusugua mafuta kwenye unga hadi uwe chembechembe.

Ongeza maji, huku ukichanganya mpaka unga uwe laini. Kisha kanda kwa muda wa dakika 10 au mpaka uwe laini na elastiki au nyumbufu.

Funika kwa kitambaa cha plastiki kwa dakika 30.

Vya kujaza kwenye sambusa

Katika sufuria kubwa, pasha mafuta juu ya moto wa kati. Ongeza vitunguu na kaanga hadi vitunguu viwe na rangi ya hudhurungi, kama dakika tatu.

Ongeza kitunguu saumu kilichopondwa na upike hadi kiwe chenye harufu nzuri, kama sekunde 30 hivi.

Ongeza nyama iliyosagwa ya kuku na upike mpaka iwe na rangi ya kahawia. Ongeza viazi vilivyokatwa, njegere za kijani, tangawizi iliyokunwa, paprika, zaatari, poda ya kari, chumvi, na pilipili nyeusi.

Koroga na uache chakula kiive. Aidha hakikisha viazi vimeiva na nyama iko tayari, kama baada ya dakika 10. (Ongeza maji kama inahitajika).

Ondoa sufuria kutoka kwa moto na uache chakula hiki kipoe.

Kukusanya sambusa:

Gawanya kinyunya katika sehemu nane sawa, kisha tengeneza kila sehemu iwe kama mpira na uifanye kuwa diski.

Kata kila diski katikati ili kutengeneza miduara miwili. Chukua mduara mmoja na ukunje kwa umbo la koni, ukifunga kingo na maji.

Jaza koni na vijiko 1-2 vya kuku na njegere ili kujaza.

Funga mwisho wa koni kwa kutumia maji kwenye kingo na kuzishikanisha pamoja.

Rudia mchakato na unga uliobaki na kuyajaza.

Kukaanga sambusa:

Koni za sambusa kabla ya kutumbukizwa kwa mafuta yaliyochemka. PICHA | MARGARET MAINA

Pasha mafuta ya kutosha kwenye sufuria na kukaanga kwenye moto wa kati.

Mara tu mafuta yanapokuwa moto, ongeza sambusa chache kwa wakati mmoja na kaanga hadi ziwe na rangi ya dhahabu pande zote mbili.

Ondoa samosa kutoka kwa mafuta na uziweke kwenye taulo za karatasi.

Pakua na ufurahie.

  • Tags

You can share this post!

Fahamu kwa nini unapaswa kula dengu mara kwa mara

MAPISHI KIKWETU: Skonzi zilizotiwa zabibu kavu

T L