NA MARGARET MAINA
Muda wa kuandaa: Saa 2
Muda wa mapishi: Dakika 40
Walaji: 3
Vinavyohitajika
Maelekezo
Katika bakuli lako la kwanza, mimina maziwa ya moto, maji fufutende na uyapasulie mayai ndani. Ongeza siagi iliyoyeyuka, hamira pamoja na sukari na chumvi.
Maji na maziwa vinahitaji kuwa moto kwani hutengeneza mazingira bora kwa hamira kuumuka.
Koroga vyote kwa pamoja.
Katika bakuli tofauti, changanya unga, zabibu kavu na rangi ya chakula. Mara baada ya viungo hivi vikavu kuchanganyika, tengeneza shimo kidogo katikati na umwagilie mchanganyiko wako wa maziwa na hamira. Changanya na mwiko na vikishachanganyika, endelea kukanda kwa dakika 15.
Kinyunya kinapaswa kuwa laini, lakini sio kushikamana na mikono yako. Ikiwa bado kinanata, kanda kwa dakika chache zaidi na utaona kikianza kuwa elastiki kama inavyohitajika.
Sehemu inayochukua muda ni kinyunya kuumuka. Huchukua takriban saa moja. Ukisubiri kinyunya kiumuke, unaweza kufanya kazi nyingine.
Baada ya kuumuka, gawanya kinyunya kiwe mipira 12 na uiweke kwenye chombo cha kuokea ulichopaka mafuta, na uache tena mipira hiyo ili kuumuka kwa dakika nyingine 30, yaani nusu saa.
Baada ya hayo, brashi sehemu ya juu na yai na uoke katika ovena kwa dakika 30 kwa sentigredi 180. Madhumuni ya kupaka yai ni ili juu ya skonzi kuwe na rangi ya kahawia.
Skonzi zikiiva vizuri, ziepue uache zipoe vizuri kisha pakua na uanze kula.