NA MERCY KOSKEI
WAIGIZAJI mashuhuri Kate Actress na Philip Karanja almaarufu Phil Director, wametangaza kuachana baada ya miaka kadhaa ya ndoa.
Kupitia taarifa ya pamoja mnamo Jumanne, Septemba 19, 2023 wawili hao walifahamisha mashabiki wao kuwa wametengana.
“Tulifikia uamuzi wa kuvunja ndoa yetu kitambo sana na kwa sasa tumetengana rasmi. Tunaomba kwa unyenyekevu mtupe heshimu ya faragha kwa ajili ya watoto wetu,” taarifa yao ilielezea.
Kwa upande wake, Phil alijibu akisema kuwa licha ya wawili hao kutengana bado watasalia kuwa marafiki na washirika wa biashara.
“Hii ni mambo ya watu wawili, tunaomba mtupe nafasi ili tuweze kuendelea na maisha yetu bila stori mingi. Mimi na Kate tutabaki kuwa marafiki, kushirikiana kulea na washirika kibiashara,” alisema.
Wawili hao walifunga pingu za maisha Novemba 2017, katika hafla ya kipekee iliyohudhuriwa na marafiki wa karibu na familia pekee.
Hata hivyo, Aprili 2023, uvumi ulienea kwamba wanandoa hao walikuwa wameachana.
Kate aliwaacha wafuasi wake wakiwa wamechanganyikiwa baada ya kufuta picha za Phil kutoka kwa akaunti zake za mitandao ya kijamii.
Baadaye, kupitia Instagram, Kate alieleza mashabiki wake kuwa ndoa yake ilikuwa inaendelea vizuri.